Dar es Salaam. Kampuni ya Mofat Company Limited, iliyopewa zabuni ya kuendesha mradi wa mabasi yaendayo haraka awamu ya pili, inatarajia kutoa ajira zaidi ya 1,000.
Kampuni hiyo ya Kitanzania imeingia mkataba wa miaka 12 na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) ili kuendesha mradi huo wa awamu ya pili kuanzia Gerezani hadi Mbagala. Ujenzi wa miundombinu umeshakamilika na kinachosubiriwa ni mabasi ili huduma zianze kutolewa.
Juni 3, 2025, Mtendaji Mkuu wa Dart, Dk Athuman Kihamia alisema wameingia mkataba na Mofat Company Limited: “Kuanzia Juni, na ni mkataba wa miaka 12 ili kuendesha mradi wa njia ya Mbagala.”
Alisema kampuni hiyo ni ya wazawa ambao wanatarajia kuanza Agosti 2025: “Wataingiza mabasi 255 yanayotumia gesi,” alisema.
Katika mazungumzo na gazeti dada la The Citizen, Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa Mofat, Mabrouk Masasi, amesema tayari wametangaza nafasi 423 za ajira kwa ajili ya maandalizi ya kuanza huduma Septemba mosi, 2025.
“Tumeanza kuajiri. Kati ya nafasi hizo, 255 ni kwa madereva, 158 kwa wasaidizi wa vituo, na zilizobaki ni kwa mafundi na wafanyakazi wa kusaidia shughuli mbalimbali,” amesema Masasi.
Hii ni sehemu ya kwanza ya mchakato wa ajira, ambapo Mofat inatarajia kuajiri jumla ya wafanyakazi takriban 1,100 mara shughuli zitakapoanza kikamilifu. Nafasi zaidi zitatangazwa kadri mabasi yatakavyowasili.

Kampuni hiyo inatarajia kuanza kupokea awamu ya kwanza ya mabasi 255 Agosti, huku mabasi yote yakitarajiwa kuwa yamewasili kufikia mwishoni mwa Septemba.
“Huduma zitaanza rasmi Septemba mosi, mara tu mabasi yakianza kuwasili,” amesema.
Maandalizi mengine yanaendelea, ikiwa ni pamoja na kufunga mageti ya tiketi za kielektroniki, mafunzo kwa madereva, na kuunganisha mifumo mbalimbali. Mabasi yote yatahifadhiwa katika kituo cha Mbagala.
Kampuni hiyo imejifunza kutokana na changamoto za awamu ya kwanza, na sasa inalenga kutumia teknolojia ya kielektroniki kuendesha shughuli zote, ikiwemo ukusanyaji wa nauli.
“Tunahamia kwenye mifumo ya kidijitali. Mfumo wa kielektroniki utasaidia kusimamia vizuri shughuli za mabasi,” amesema Masasi.
Ili kufanya uendeshaji kuwa madhubuti, kampuni hiyo imeshirikiana na wataalamu wa Dart wenye uzoefu wa zaidi ya miaka 20.
Kwa mujibu wa Masasi, kutokana na mpango wa kuendesha mabasi 255 kwa awamu tatu, zaidi ya madereva 750 watahitajika, na jumla ya wafanyakazi itafikia 1,100. Madereva watafanya kazi kwa zamu ya saa nane kwa kuzingatia sheria za kazi.
Wakati Mofat ikipewa zabuni hiyo, Dk Kihamia alisema awamu ya kwanza, njia ya Kimara–Morocco–Kivukoni na Gerezani, itaendeshwa na Kampuni ya Emirates National Group (ENG) kwa kipindi cha miaka 12 na inatarajia kushusha mabasi 177.
Ujio huo wa mabasi ni miongoni mwa ahadi alizotoa Rais Samia katika salamu zake za Mwaka Mpya, Desemba 31, 2024, aliposema katika mwaka 2025 miongoni mwa miradi itakayotekelezwa kwa njia ya ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) ni wa BRT.
Alieleza Serikali itatoa kipaumbele kutekeleza miradi ya kupunguza msongamano katika majiji, likiwamo la Dar es Salaam, kwa kutekeleza awamu ya tatu na ya nne ya miundombinu ya barabara za mwendokasi na kuanza huduma kwenye awamu ya pili kwa njia ya Mbagala.