ATE yajitosa kukuza ujuzi ajira zenye staha

Dar es Salaam. Katika kukabiliana na pengo la ujuzi, Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi Tanzania (Tucta) na Muungano wa Soko la Ajira la Denmark, imeweka mkakati madhubuti wa ukuzaji wa ujuzi kwenye ajira zenye staha.

Mkakati huo umebainishwa katika kongamano la waajiri lililofanyika Juni 22, 2025 likitanguliwa na mkutano mkuu wa 66 wa ATE), uliofanyika Juni 18, 2025 jijini hapa.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Suzanne Ndomba-Doran amesema kongamano hilo pamoja na mambo mengine limejadili kuwezesha na kubadilishana uzoefu na mbinu bora sambamba na mafunzo, mfano mafunzo ya ufundi na mahitaji ya uundaji wa ajira zenye staha, ushirikishwaji wa kijinsia na mabadiliko ya kijamii na ya haki.

Amesema kupitia midahalo ya kijamii na ushirikiano wameweza kuboresha ushirikiano wa waajiri, wafanyakazi na Serikali ili kuimarisha mifumo ya kazi yenye staha hasa kwa vijana na ukuzaji wa ajira.

“Mwaka  2024, ATE kwa kushirikiana na Tucta na msaada kutoka Danish Industry (DI) na Wakala wa Maendeleo wa Vyama vya Wafanyakazi wa Denmark (DTDA), tulihitimisha mradi wa miaka mitatu uliolenga kukuza ujuzi na ajira kwa vijana.

“Mpango huo ulishughulikia kutokuwa na uwiano kati ya ujuzi na mahitaji ya soko la ajira, ukilenga kuimarisha uwezo wa kuajiriwa kwa vijana wa Kitanzania,” amesema na kuongeza kuwa kupitia mradi huo, vijana 1,098 walipatiwa mafunzo katika fani nne.

Amesema: “Katika nchi ambayo inasukuma maendeleo ya viwanda, kuna haja ya dharura ya taasisi za mafunzo ya ufundi stadi kuendeleza nguvu kazi yenye ujuzi ambayo inakidhi kwa urahisi matarajio yanayoendelea kukua ya waajiri.”

Suzanne amegusia namna kwa muda mrefu kile ambacho wanafunzi hujifunza na kile ambacho viwanda vinahitaji kutokuendana na maarifa ya kiutendaji au ujuzi waliojifunza.

Mkurugenzi huyo amesema moja ya malengo ya kongamano hilo ni kuoanisha ujuzi na maarifa ya wafunzwa na matarajio ya mwajiri.

Katika kongamano hilo, Serikali na vyama vya wafanyakazi vilitoa mapendekezo ya vitendo kwa ajili ya kuboresha ukuzaji wa ujuzi na ujifunzaji unaozingatia kazi.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Dk Yose Mlyambina amesema sheria mpya za kazi zinakwenda kuboresha na kuongeza ufanisi licha ya kwamba bado hazijaanza kutumika.

Amesema marekebisho ya Sheria ya Kazi ya Mwaka 2025 yamezingatia pande zote, waajiri na waajiriwa.

Related Posts