Shinyanga. Kijana mmoja, mkazi wa Mtaa wa Tambukareli, manispaa ya Shinyanga, Bernado Massanja (24) ameuawa kwa kuchomwa kisu maeneo ya kifuani, upande wa kushoto, wakati wakigombania abiria.
Kijana huyo aliyekuwa akifanya kazi kama bodaboda, anadaiwa kuuawa na mwenzake wakati wakigombania abiria ili kujiingizia kipato. Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta mhusika katika tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akitaja chanzo cha tukio hilo kuwa ni ugomvi wa bodaboda kugombania abiria katika kata ya Ndembezi iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
Akizungumza kwa njia ya simu leo Juni 23, 2025, Kamanda magomi amewataka wananchi kutokujichukulia sheria mkononi, na kama mtu akikosea afikishwe kwenye vyombo vya sheria ili achukuliwe hatua.
“Nilipigiwa simu na mwenyekiti wa Mtaa wa Tambukareli, Tabitha Constantine akinipa taarifa ya kijana kuchomwa kisu na kijana mwenzie, tulifika eneo la tukio, ni kweli lakini aliyefanya tukio hilo alikimbia na bado tunamsaka,” amesema Kamanda Magomi.
Ameongeza: “Katika uchunguzi wa awali tuliofanya, tumegundua vijana hawa ambao ni bodaboda walikuwa wanagombania abiria. Kijana mmoja aliyefahamika kwa jina moja la ‘Kulwa’ alichomoa kisu na kumchoma mwenzie kifuani upande wa kushoto ambaye ni Bernado Massanja (24) na kupoteza maisha,” amesema Magomi.
Kamanda huyo ametoa wito kwa vijana kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani kufanya hivyo kunawaingia kwenye makosa ya jinai kama uuaji au makosa mengine yanayowaingiza matatani.
“Mwili wa marehemu ulichukuliwa kwa ajili ya uchunguzi baadaye utakabidhiwa kwa familia kuendelea na taratibu za mazishi,” amesema Kamanda Magomi.
Akizungumzia tukio hilo, shangazi wa marehemu ambaye pia ni kiongozi wa Mtaa wa Tambukareli, Maria Laurent ameeleza namna walivyopata taarifa kuhusiana na tukio alilofanyiwa Bernado ambapo ilikuwa ni mida ya usiku walipopokea taarifa hizo.
“Ilikuwa saa 7 usiku, nilipigiwa simu na mama yake nikiwa kwangu, nikaambiwa Bernado kachomwa kisu, nilipofika eneo la tukio ambapo ndipo huwa anakaa na vijana wenzake, nikakuta amefariki, ndipo tukapiga simu polisi kwa ajili ya hatua nyingine,” amesema shangazi huyo wa marehemu.
“Saa 5 usiku nilisikia kuna ugomvi na mmoja kachomwa kisu, tulivyotoka tukakuta aliyefanya tukio hilo amekimbia. Kama nzego tulifanya juhudi za kumkamata lakini hatukufanikiwa, akawa ametoweka,” amesema jirani wa marehemu, Massanja Samson.
“Nilifuatwa nyumbani na vijana watatu ambao ni bodaboda, wakaniambia kuna mwenzao amechomwa kisu. Nilipofika eneo la tukio, nikakuta ni kweli, ndio nikachukua hatua ya kutoa taarifa polisi, walikuja na kuchukua mwili kwa ajili ya kuchunguza,” amesema mwenyekiti wa serikali ya mtaa, Tabitha Constantine.