Arusha. Wakati Serikali ikijizatiti katika matumizi ya teknolojia, matumizi ya mifumo ya Tehama isiyo salama au isiyo na ubora unaohitajika yanatajwa kuwa chanzo cha vihatarishi katika ulinzi wa taarifa binafsi.
Aidha, wakati Tanzania ikielekea kwenye uchumi wa kidijitali, imetakiwa kuhakikisha kuna uaminifu kati ya mtumiaji wa teknolojia na mtoa huduma katika usalama wa kimtandao.
Hayo yameelezwa leo, Jumatatu Juni 23, 2025, na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dk Emmanuel Mkilia, wakati akifungua mafunzo ya kupunguza madhara ya vihatarishi katika ulinzi wa taarifa binafsi.
Mafunzo hayo ya siku tatu yameanza leo mkoani Arusha, yakihusisha waratibu na wasimamizi wa vihatarishi, wajumbe wa bodi, wakuu wa idara na vitengo, maofisa Tehama, na wakaguzi wa ndani na nje kutoka taasisi za umma na binafsi.
Mkurugenzi huyo amesema kwa sasa kuna changamoto kubwa ya kulinda taarifa binafsi na faragha za watu katika taasisi mbalimbali, kutokana na kukua kwa teknolojia ambayo ina taarifa nyingi za watu.
Amesema mafunzo hayo yanalenga zaidi kuhakikisha kila taasisi inatambua vihatarishi vinavyoweza kusababisha zisifikie malengo yake na kuzingatia ulinzi wa taarifa binafsi, kwani katika dunia hii ya kidijitali inayobadilika kwa kasi, taarifa hizo ziko hatarini.
“Kupitia mafunzo haya tutapata uelewa wa kutosha jinsi taasisi zetu zinalinda taarifa binafsi na faragha. Tunahitaji kuhakikisha kila taasisi inakuwa na utaratibu mzuri wa kukagua maeneo yenye hatari, kuwa na uwezo wa kutambua vihatarishi na kuchukua hatua stahiki.
“Tehama ni nyenzo mojawapo katika kuhakikisha taasisi inafanya majukumu yake ipasavyo, lakini kama haitakuwa salama, Tehama hiyohiyo itakuwa sababu ya kuleta athari. Ukosefu wa sera madhubuti na usimamizi wa taarifa binafsi ni miongoni mwa vihatarishi,” amesema.
Mkurugenzi huyo amesema moja ya majukumu ya tume hiyo ni kuhakikisha taasisi yoyote inayokusanya na kuchakata taarifa imetengenezewa mazingira dhabiti kuhakikisha taarifa hizo ziko salama.
“Katika kupambana na hayo, ni lazima kufanyika kwa tathmini za vihatarishi mara kwa mara ili kuvidhibiti, kusimamia sera na taratibu za ulinzi wa taarifa binafsi, kuhakikisha mifumo ya kielektroniki inalindwa na teknolojia za kisasa, na kutoa mafunzo ya ndani,” amesema.
Awali, Mkurugenzi wa Usajili na Uzingatiaji, Mhandisi Stephen Wagwe, amesema mafunzo hayo ya siku tatu yamelenga kuongeza uelewa na ujuzi wa namna bora ya kulinda taarifa binafsi kwa kuzingatia usimamizi wa vihatarishi na utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44, kanuni zake pamoja na miongozo ya PDPC.
Amesema kupitia mafunzo hayo, washiriki wataangalia vihatarishi vilivyopo katika utekelezaji wao wa majukumu ya kila siku.
“Sheria ilitungwa mahsusi kwa ajili ya kuhakikisha tunalinda faragha ya wananchi, lakini pia tunatunza na kulinda taarifa zake, kwani taarifa za mtu zinaweza kumpelekea kupata hatari katika sehemu moja au nyingine. Taasisi mbalimbali zinachukua taarifa zetu kwa ajili ya kutuhudumia,” amesema.
Ameongeza:“Kupitia mafunzo haya, tutawakumbusha kuhusu sheria hii, misingi nane ya taarifa binafsi na masuala mengine ili kuzuia na kupunguza vihatarishi.”