DC Shaka akemea mauaji ya mfanyabiasha Dumila, polisi waendelea na uchunguzi

Kilosa. Wakati Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro likiendelea kuchunguza tukio la mauaji ya mfanyabiasha wa huduma za miamala ya kifedha katika mji wa Dumila, Mana Selemani (50), Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amelaani mauaji hayo na amewataka wananchi kuwa na imani na jeshi hilo na kutoa ushirikiano ili kufanikisha kuwakamata kwa wahusika wote.

Shaka ametoa rai hiyo leo Juni 23, 2025 ikiwa ni siku moja baada ya mfanyabiasha huyo kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika kisha kuporwa begi alilokuwa amebeba usiku ya kuamkia Juni 22, 2025 akiwa njiani, muda mfupi baada ya kufunga kibanda chake cha biashara eneo la Dumila, Wilaya ya Kilosa.

“Tangu juzi usiku tukio hili lilipotokea, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimefika eneo la tukio na vinaendelea na uchunguzi, naamini jeshi letu la polisi ambalo lina weledi wa kutosha wa kufanya uchunguzi vitafanikisha kubaini waliofanya mauaji haya.

“Ni tukio baya na la kusikitisha lakini niwaambie tu wananchi wa Dumila na wilaya nzima ya Kilosa, msiwe na hofu. Endeleeni na shughuli zenu za kujiingizia kipato, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viko kazini,” amesema Shaka.

Ameongeza: “Wale wote waliohusika kula njama na hata kutekeleza mauaji haya, nawaambia huko waliko hawako salama. Hii nchi ina mtandao mkubwa wa kiusalama na jeshi letu lina vifaa na weledi wa kutosha hata kama hao watu watakuwa wamejificha pangoni wakae wakijua muda si mrefu tutawakamata tu.”

Shaka amelaani tukio hilo na kuwapa pole ndugu na familia ya marehemu huku akiwataka kuwa na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu ambacho wamempoteza mpendwa wao lakini kuliamini jeshi la polisi wakati likiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Kwa upande wake, mtoto wa marehemu, Zulfa Mana amesema baada ya mwili wa baba yake kufanyiwa uchunguzi polisi waliwakabidhi mwili na jana Juni 22, 2025 jioni walifanya maziko huko huko Dumila wilayani Kilosa.

Amesema kama familia mpaka sasa hawafahamu nani aliyehusika kumuua baba yao na hawajapata taarifa kama kuna mtu ama watu waliokamatwa kuhusiana na mauaji hayo.

“Tulifanikiwa kumpuzisha mzee jana jioni, na bado hatujapata taarifa kama kuna waliokamatwa, tumeliachia Jeshi la Polisi lenye dhamana na weledi wa kuchunguza tukio hili na wanaendelea na uchunguzi, naamini watakafanikiwa kuwakamata waliohusika katika tukio hili,” amesema Zulfa.

Mapema Juni 22, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu tukio hilo la mauaji ya mfanyabiasha huyo na kuwaomba wananchi wema mwenye taarifa za mtu au watu waliohusika na mauaji hayo watoe taarifa ili kusaidia kuwakatwa kwa watuhumiwa hao.

“Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linatoa wito kwa wananchi wote kuendelea kushirikiana nasi katika uchunguzi wa tukio hili ambao tumeuanza na hivyo tunawaomba watupe taarifa endapo watakuwa na tetesi ama fununu za walipo walipo watuhumiwa hawa, majina yao ama njia nyingine yoyote itakayosaidia kuwakamata watuhumiwa hawa,” alisema Kamanda Mkama.

Related Posts