Makalla ataja mambo sita watakayofanya uchaguzi mkuu 2025

Mpwapwa. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla ameainisha mambo sita yatakayofanyika katika uchaguzi mkuu ikiwemo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kumtangaza mgombea atakayeshinda kwa haki.

Mambo mengine ni utekelezaji wa Ilani ya CCM, kupeleka wagombea wenye sifa, kuheshimiana kwa kutumia utaratibu wa 4R, kutokuwa na kampeni za kubeza wala matusi vyama vingine na kulinda amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Makalla ameyasema hayo leo Jumatatu Juni 23, 2025 wakati akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.

Ziara hiyo ni katika utaratibu wa kiongozi huyo kuelekea uchaguzi mkuu, kuzungumzia mwelekeo na kukumbushana mafanikio yaliyopatikana.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Makalla amesema hivi karibuni wamezindua ilani ya uchaguzi ambayo wataanza kuitekeleza baada ya kupitisha bajeti Juni 24, 2025 na hivyo kuanza utekelezaji wa ilani hiyo.

Amesema baada ya marekebisho ya sheria za uchaguzi, chama chake kinaamini kuwa kutakuwa na uchaguzi mkuu wa haki na huru.

“Basi tunaamini kwa uwepo wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na tunaamini kwamba atakayeshinda kwa haki atangazwe mshindi. Pia, tumefanya mabadiliko katika utaratibu wa uteuzi wagombea ndani ya chama,” amesema.


Makala amesema katika utaratibu huo kutakuwa na waombaji wengi lakini chama kitarejesha majina matatu ya watu wenye sifa kuwania ubunge na udiwani, watakaopigiwa kura na wanachama wa chama hicho ili kupata mgombea mmoja.

Kuhusu kampeni, Makalla amesema kwa kutumia 4R za Rais Samia, watashiriki katika kampeni za kuheshimiana, za kistaarabu kwa kuwa kutakuwa na Ilani ya Uchaguzi itakayotumika kuomba kura.

“Kutakuwa hakuna haja ya kubeza wala kutukana vyama vingine. Wenye ufundi wa kutukana matusi watapimwa na wananchi,” amesema.

Kwa upande wa amani, kiongozi huyo amewahakikishia Watanzania amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi na kuwataka kuwakataa watakaoeneza chuki.

Amesema uchaguzi uko kwa mujibu wa Katiba ya nchi na kuwataka Watanzania kutumia haki yao hiyo kwa kupiga kura katika uchaguzi na kupuuza uamuzi wa Chadema wa No reforms, no election kwa kuwa mabadiliko ya sheria za uchaguzi  yaliyokuwa yakitakiwa yalishafanyika.

Aidha, Makalla amesema CCM kinadhamana na wajibu wa kuwatumikia Watanzania na kuwa maendeleo ni hatua kama kuna changamoto hakuna chama kitakachotatua zaidi ya CCM, hivyo akawaomba wakazi wa wilaya hiyo kuwapa dhamana tena kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Baadhi ya wachungaji na waumini wa madhehebu mbalimbali ya Dini Mkoa wa Mbeya , walioshiriki kongamano la kuombea uchaguzi na Rais Samia Suluhu Hassan  katika ukumbi wa Mkapa jijini Mbeya.Picha na Hawa Mathias.



“Wasije wakadhani kama kuna changamoto zilizobakia kutakuja chama kingine kinaweza kuja kufanya, chama kinachoweza kuahidi na kutenda hakuna kikingine zaidi ya CCM. Tunawaahidi kama kuna mambo hajakamilika yatakamilika katika Ilani ya mwaka 2025,”amesema.

Makalla amesema miaka yote Mkoa wa Dodoma ni ngome ya CCM na kuwa wamelinda heshima hiyo kwa mara zote kuhakikisha majimbo yote yamekuwa chini ya CCM.

Amesema alipofika kwenye mkutano huo na kukutana na wingi wa watu anaamini kuwa Dodoma itaendelea kuwa ni kuwa ngome ya CCM wakati wa uchaguzi mkuu.

Mbunge wa Mpwapwa (CCM), George Malima amesema mafanikio mengi yamepatikana katika Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara na madaraja.

“Alivyoingia madarakani Rais Samia (Rais Samia Suluhu Hassan) upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Mpwapwa ulikuwa asilimia 45 lakini sasa ni asilimia 75,”amesema Malima.

Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto za barabara ya kutoka Kongwa hadi Mpwapwa, daraja la Godegode ambalo tayari limeshatengewa fedha za ujenzi na vituo vya afya ambapo kata nne hazina miundombinu hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Dk Sophia Kizigo amesema wakati Rais Samia anaingia madarakani kata nyingi zilikuwa hazina shule za sekondari lakini kwa muda wa miaka miwili na nusu aliyokaa Mpwapwa ameshuhudia ujenzi wa shule za sekondari 11 pamoja na Chuo cha Elimu ya Ufundi Stadi (Veta).

Related Posts