Qatar yafunga anga kwa muda kujihami tishio mashambulizi ya Iran 

Doha. Serikali ya Qatar imesema imefunga anga lake kwa muda kama sehemu ya hatua zinazochukuliwa kufuatia matukio yanayoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar iliyochapishwa kwenye X imeeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama wa wananchi wake na wageni.

Taarifa zingine zimeeleza ndege zimeelekezwa kutua Bahrain.
Kufungwa kwa anga ya Qatar kunajiri wakati Iran imerudia vitisho vyake vya kulipiza kisasi dhidi ya Marekani kufuatia mashambulizi kwenye maeneo yake ya nyuklia.

“Mamlaka husika za Qatar zinatangaza kusitishwa kwa muda kwa safari za anga katika anga ya nchi, ili kuhakikisha usalama wa raia, wakazi na wageni,” imeeleza  taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje.
Hatua hiyo inakuja “kama sehemu ya hatua za tahadhari zilizochukuliwa kutokana na hali inavyoendelea katika eneo,” taarifa hiyo imeongeza.

Hili linakuja baada ya Uingereza na Marekani kutoa tahadhari kwa raia wao walioko Qatar kutulicha ndani ya makazi yao kutokana na kuongezeka kwa mvutano katika Mashariki ya Kati.

“Kufuatia tahadhari ya usalama ya Marekani kwa raia wake walioko Qatar, kwa tahadhari ya hali ya juu, tunapendekeza raia wa Uingereza walioko Qatar wabaki ndani hadi taarifa nyingine itakapotolewa,” amesema Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza katika taarifa yake.

Ubalozi wa Marekani nchini Qatar ulituma barua pepe kwa raia wa Marekani walioko nchini humo ukiwashauri wabaki ndani hadi taarifa nyingine itolewe.

Ujumbe huo umesema kuwa pendekezo hilo ni “kwa tahadhari ya hali ya juu” na haukutoa maelezo zaidi.

Haya yanatokea wakati eneo hilo likiwa katika hali ya wasiwasi kwa kuhofia uwezekano wa Iran kulipiza kisasi dhidi ya masilahi ya Marekani katika Mashariki ya Kati baada ya Washington kushambulia maeneo ya nyuklia ya Iran siku ya Jumapili, na hivyo kuingia moja kwa moja kwenye mzozo wa Iran na Israel.

Israel na Iran waliendelea kurushiana makombora siku ya Jumatatu, ambapo Israel ilishambulia kituo cha nyuklia cha Fordow na Gereza la Evin la Iran, huku mashambulizi dhidi ya Israel yakipelekea kukatika kwa umeme katika baadhi ya miji ya kusini.

Qatar imesema siku ya Jumatatu kuwa hali ya usalama nchini humo iko imara kufuatia tahadhari zilizotolewa na balozi kadhaa kwa raia wao kuwa waangalifu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Majed Al Ansari amesema kupitia X kwamba tahadhari hizo hazionyeshi kuwepo kwa tishio mahususi.

“Tunapenda kuwahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama katika nchi bado ni tulivu,” alisema.

“Mamlaka husika zinafuatilia kwa karibu hali ilivyo na zipo tayari kuchukua hatua zote muhimu ili kuhakikisha usalama wa raia, wakazi na wageni,” ameongeza.

Related Posts