Chadema kukabana kwa hoja mahakamani leo kesi ya mgawanyo wa rasilimali

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, leo Jumanne Juni 24, 2025, inatarajiwa kusikiliza kesi ya msingi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali inayokikabili Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kesi hiyo imefunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Taifa, Zanzibar; Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, ambao ni wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kutoka Zanzibar.

Wadaiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema, mdaiwa wa kwanza, na Katibu Mkuu wa Chadema, mdaiwa wa pili.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa leo na wadai watatoa hoja zao za msingi kufafanua malalamiko yao kabla ya wadaiwa nao kujibu hoja hizo.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, mawakili wa pande zote watakuwa katika mchuano wa hoja za kiushahidi au kisheria.

Wadai watakuwa na kibarua cha kujenga hoja na kufasiri sheria kuishawishi Mahakama ikubaliane na madai yao, huku wadaiwa wakipambana kupangua hoja hizo kwa kutumia sheria hizohizo.

Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote, itapanga tarehe ya hukumu.

Wadaiwa wanaingia katika usikilizwaji wa kesi hiyo wakiwa na kumbukumbu chungu ya uamuzi wa mahakama hiyo uliowaathiri katika harakati zao za awali kupambana na kesi hiyo.

Wadai, mbali na kesi hiyo ya msingi, pia walifungua shauri dogo la maombi ya zuio dhidi ya wadaiwa, wakiomba mahakama itoe amri ya kuwazuia kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka kesi yao ya msingi itakaposikilizwa, ambalo lilisikilizwa na kuamuliwa.

Wadaiwa walijipanga kumaliza kesi hiyo katika hatua za awali kabla ya kufikia hatua ya usikilizwaji wa madai ya msingi kwa mbinu za kiufundi.

Wadai waliweka mapingamizi ya awali dhidi ya kesi ya msingi na dhidi ya shauri dogo la maombi ya zuio la muda, wakibainisha sababu tisa za kisheria kutaka kesi hiyo itupwe bila kusikilizwa.

Hoja za mapingamizi hayo zilijikita katika mamlaka ya mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo, haki ya wadai kufungua kesi hiyo, matumizi ya sheria walizotumia kufungua kesi hiyo na uhalali wa kumuunganisha Katibu Mkuu.

Waombaji (wadai) nao waliibua pingamizi la awali dhidi ya kiapo kinzani cha wadaiwa kilichojibu kiapo cha wadai kilichounga mkono maombi hayo ya zuio la muda.

Katika pingamizi hilo, waombaji waliibua hoja tano za pingamizi, pamoja na mambo mengine kuhusiana na kasoro za kisheria kwenye kiapo hicho kinzani cha wajibu maombi (wadaiwa katika kesi ya msingi).

Mei 12, 2025, Jaji Mwanga alielekeza pingamizi la Chadema dhidi ya kesi ya msingi lisikilizwe kwa njia ya maandishi na akapanga kutoa uamuzi wa pingamizi hilo Juni 10, 2025.

Pia, Jaji Mwanga aliamuru mapingamizi yote, yaani pingamizi la Chadema dhidi ya maombi hayo ya zuio na pingamizi la wadai dhidi ya kiapo kinzani cha wajibu maombi pamoja na shauri lenyewe la maombi ya zuio, yasikilizwe tarehe hiyo kwa mdomo.

Usikilizwaji wa mapingamizi hayo dhidi ya maombi ya zuio la muda pamoja na maombi hayo yenyewe ulitegemea uamuzi wa pingamizi hilo la wadaiwa dhidi ya kesi ya msingi.

Kukubalika kwa pingamizi la wadaiwa dhidi ya kesi ya msingi kungeifanya kesi hiyo kutupiliwa mbali na huo ungekuwa mwisho wake.

Hivyo, hata shauri la maombi ya zuio lingekosa miguu ya kusimama mahakamani bila kuwepo kesi ya msingi, bali nalo lingekufa kifo cha asili.

Hata hivyo, Mahakama katika uamuzi wake wa Juni 10, 2025, ililitupilia mbali pingamizi la wadaiwa dhidi ya kesi ya msingi, uamuzi uliosababisha kesi hiyo kuendelea kuwa hai na halali mahakamani hapo.

Baada ya uamuzi huo, mahakama iliendelea na usikilizwaji wa pingamizi la wajibu maombi katika shauri dogo la maombi ya zuio pamoja na pingamizi la waombaji dhidi ya kiapo kinzani cha wajibu maombi.

Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote, ilikubaliana na hoja za wajibu maombi kuwa aya moja katika kiapo cha waombaji kilichounga mkono shauri la maombi ya zuio ilikuwa na kasoro, na ikaamuru aya hiyo iondolewe katika kiapo hicho.

Hata hivyo, kuondolewa kwa aya hiyo moja hakukuathiri uimara wa kiapo hicho, bali kiliendelea kusimama na kuwa na ustahilifu.

Lakini kwa upande mwingine, mahakama ilikubaliana na hoja za pingamizi la waombaji dhidi ya kiapo kinzani cha wajibu maombi kuwa kilikuwa na kasoro za kisheria zisizoweza kurekebishika, na ikakiondoa kiapo kinzani chote mahakamani.

Kwa uamuzi huo, maombi ya waombaji katika shauri la maombi ya zuio hayakuwa yamepingwa, kwani wajibu maombi (wadaiwa) hawakuwa na haki ya kupinga chochote kuhusiana na masuala ya kiushahidi isipokuwa tu kwa hoja za kisheria.

Katika mazingira hayo, wakili wa wadaiwa/wajibu maombi, Jebra Kambole, aliamua kujitoa katika kesi hiyo na kuiomba mahakama iahirishe usikilizwaji wa shauri dogo la maombi ya zuio ili kutoa nafasi kwa wadaiwa/wajibu maombi kupata wakili mwingine.

Hata hivyo, mahakama haikushawishika na hoja zake, hivyo iliendelea na usikilizwaji wa shauri hilo la maombi ya zuio upande mmoja na ikaotoa uamuzi wake.

Katika uamuzi huo, mahakama ilikubaliana na hoja za maombi ya waombaji na ikatoa amri kuwazuia wadaiwa kujishughulisha na shughuli zozote za kisiasa mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.

Pia, mahakama ilipiga marufuku wajibu maombi na watu wengine wowote wanaofanya kazi kwa niaba au kwa maelekezo ya wadaiwa kutumia kwa namna yoyote mali za chama hicho mpaka kesi ya msingi itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Katika kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025, wadai wanadai kuwa kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Pia wanadai kuwa kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia, pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga Muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivyo, wanaomba mahakama hiyo iamuru kuwa wadaiwa wamekiuka Katiba ya chama hicho na kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258, Marejeo ya mwaka 2019 na iwaelekeze kuzingatia sheria hiyo na Katiba yake.

Pia wanaiomba mahakama hiyo itamke kuwa ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.

Amri nyingine wanazoziomba ni kusitishwa kwa muda kwa shughuli zote za kisiasa hadi hapo kutakapokuwepo na utekelezaji wa maagizo ya mahakama; amri ya zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi wadaiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika.

Vilevile, wanaiomba mahakama iamuru wadaiwa walipe gharama za kesi hiyo na itoe nafuu nyingine yoyote ambayo itaona inafaa kuzitoa.

Related Posts