Kama vyuo vyetu havina lengo hili, tumefeli

Arusha. Kwa takriban miaka 50 nimefundisha katika vyuo vikuu hapa Tanzania, Kenya, Marekani na Finland.

Katika safari hii, nimekuwa nikijenga hoja hasa katika somo la falsafa na maadili,na kufanya kufanya utafiti mwingi na kusoma mawazo ya wataalamu mbalimbali, na hata kubadilishana mawazo na watu wa kawaida kabisa.

Kote humo  nimekuwa najiuliza: hivi elimu ya juu inapaswa kulenga kitu gani katika maisha ya wahitimu wake? Mhitimu wa chuo kikuu anapaswa awe mtu wa aina gani?

Katika kujiuliza maswali haya kwa muda mrefu, nilipata bahati siku moja kusoma makala iliyoandikwa na Dean Brackley, mchungaji wa Shirika la Wajesuiti kuhusu nafasi ya vyuo vikuu katika nchi ya El Salvador iliyopo Marekani ya Kati.

Mwandishi huyu alielewa vizuri sana umaskini wa ajabu uliyoitafuna nchi hiyo zama hizo za miaka ya 1980 na kuendelea.

Umaskini wa nchi hiyo ulikuwa ukiongezeka siku hadi siku, ilhali watu wachache wakiendelea kuogelea katika utajiri wa kutisha.

Ikatokea kwamba mwezi Novemba 1989, kikundi fulani cha wanajeshi kilivamia chuo cha Amerika ya Kati, (University of Central America, El Salvador) na kuwapiga risasi viongozi sita wa chuo hicho.

Ilidaiwa kuwa  viongozi hao walihamasisha wanafunzi wapige vita umaskini wa nchi yao na wapinge mwenendo wa wachache kuwa matajiri sana wakati walio wengi wakikaangwa na umaskini.

Kutokana na mauaji hayo ya kikatili, na kutokana na umaskini mkubwa uliyoitesa nchi hiyo, mwandishi Brackley akaandika: ‘’Chuo kikuu ni mahali pa kupika wahitimu ambao huuliza maswali yanayohusu mustakabali wa nchi yao, na ambao watakuwa tayari kujitoa mhanga kwa ajili ya watu wao wanaoteswa na umaskini.’’

 Akaendelea: ‘’Roho ya chuo kikuu inapaswa kuwa nje ya chuo hicho, yaani sababu ya kuwepo kwa chuo kikuu,  ni kuwahamasisha wanafunzi waulize maswali haya mara kwa mara: watu wetu vijijini wanaishije? Kwa nini umaskini upo? Kwa nini unaongezeka? Sisi kama wahitimu wa chuo kikuu tufanye nini kupunguza hata kutokomeza umaskini katika nchi yetu?’’

Akaongeza tena: ‘’Kila chuo kikuu kinapaswa kupambana na hali ya udhalilishaji wa wale wanaoishi katika umaskini. Chuo kikuu kina wajibu wa kujenga utu katika jamii kwa sababu wanachuo ni wataalamu wa kuuliza maswali ya msingi katika jamii.’’

Wanachuo wanapaswa kuwa wataalamu wa kujenga hoja, kujibu hoja, kuibua hoja mpya, na kuepa kuongozwa na hoja hafifu.

Brackley anaendelea kusema: ‘’ Chuo hakipaswi kuwa chama cha siasa, wala hakitafuti madaraka ya uongozi. La hasha.’’

Badala ya kutafuta umaarufu wa kisiasa au wa kiuongozi, chuo kikuu kinapaswa kujikita kama chachu ya mabadiliko yaletayo haki katika jamii. Hii ndiyo maana ya chuo kikuu kuwa na roho yake nje ya chuo hicho (a university with its center outside itself).

Chuo hicho kinapaswa kujua fika maisha ya watu maskini na kupinga hali hiyo kwa nguvu zake zote.

Wahitimu wa chuo cha aina hiyo hutafuta ukweli na kwenda mbali zaidi kwa kuuweka wazi unyonyaji wa wasiojitambua kuwa wanyonyaji na kuweka wazi uongo unaosemwa na wale wanaojidai kwamba wanawatetea wananchi, lakini ukweli ukijulikana kwamba wao wapo kwa masilahi binafsi.

Ukiwaza kwa kina jambo hili utaona ni kweli kwamba uongo mkubwa unatumika na walio nacho kuwadanganya wasio nacho kwamba wapo kwa ajili yao.

Wanachuo thabiti hawana budi kuufichua uongo huu, na ndiyo maana wale viongozi sita waliuawa. Kosa lao lilikuwa kuufichuo uongo na ulaghai unaotumiwa na walafi wa mali za umma.

Hawa wahitimu wanaothubutu kuwa watetezi wa wanyonge wanaufichua ukweli kutokana na utafiti wao, tafakari zao na upendo wao kwa wale wanaoelemewa na mzigo wa umaskini. Katika nchi zilizo na demokrasia ya kweli, mabadiliko mengi huanzia katika vyuo vikuu. Vijana wa Gen Z wa Kenya walisababisha kuondolewa kwa muswada wa sheria ambayo ingefanya maisha ya wananchi yawe magumu zaidi.

Hivi majuzi wanachuo  Marekani waliandamana  kupinga hali ya vita katika ya Israel na Palestina. Yaani maana ya chuo kikuu inaonekana pale wahitimu wake wanapojishughulisha na ukosefu wa haki katika jamii.

Mwalimu Julius Nyerere alisema: ‘’ Wanakijiji maskini hutoa kodi zao kumwelimsha mwanafunzi wa chuo kikuu ili baada ya kuhitimu arudi kijijini humo kuwakwamua watu wake waondokane na umaskini. ‘’

Je, hivi ndivyo ilivyo sasa? Je, elimu ya chuo kikuu hapa kwetu inamtayarisha mhitimu atambue umaskini wa watu wake kisha uapige vita kwa nguvu zake zote? Tuna kazi kubwa mbele yetu.

Katika chuo kimoja ninachofundisha sasa kimtandao huko Marekani, kila mwanafunzi kabla ya mahafali anapaswa kujifunza kozi mbili au tatu zinazowapeleka mtaani na kujifunza maisha ya watu wa kawaida, hasa maskini. Katika somo hilo, wanafunzi hukaa darasani kwa saa chache na hupata muda mrefu mitaani wakiongea na watu wa kipato cha chini, kusikiliza maoni yao, na kuandika ripoti inayoonyesha  jinsi watu maskini wanavyoishi.

Walimu wanaofundisha somo hilo huwaambia wanafunzi kwamba hao maskini ndio walimu wao, na kwamba walimu na wanafunzi wawasikilize maskini wakiwafundisha maana ya kuishi kutwa bila chakula, maana ya kukosa matibabu kwa sababu hawana hela za matibabu, maana ya kunyanyaswa mtaani na matajiri.

 Siku moja maskini akamuuliza mwanafunzi huyo wa chuo kikuu: unajua maana ya kuishi kutwa tumbo likiwa limejaa hewa tu?  Hivi huyu mtu aitwaye njaa, wewe unamfahamu?

Huyo mwanafunzi aliripoti darasani kwamba atajitoa mhanga kutetea maskini kwa nguvu zake zote.

Huyo ndiye mhitimu tunayemtaka, huyo ndiye mwanafunzi anayestahili kupewa shahada ya chuo kikuu.

Huyu ndiye mwanafunzi aliyetabiriwa na Mwalimu Nyerere. Brackley anaongeza: ‘’Mwanafunzi wa aina hii, si tu atawasaidia maskini wapate chakula, atakwenda mbali zaidi na kupambana ili maskini huyo aondokane na umaskini.’’
Mhitimu wa aina hii anatambua kwamba anachohitaji maskini si kupewa ugali tu, bali ni kupewa uwezo wa kujitafutia ugali yeye mwenyewe.

Katika elimu yetu ya sasa mhitimu wa chuo kikuu si wa staili hii. Ni mtu wa kuukimbia umaskini yeye na familia yake, si mhitimu wa kuwawezesha maskini wajitegemee. Tunapaswa kuondokana na janga hili.

Related Posts