Dar es Salaam. Kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali inayokikabili Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), iliyokuwa imepangwa kusikilizwa leo, Jumanne, Juni 24, 2025 imekwama.
Kesi hiyo imefunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Taifa- Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, ambao ni wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kutokea Zanzibar.
Wadaiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema, mdaiwa wa kwanza na Katibu Mkuu wa Chadema, mdaiwa wa pili.

Mahakama hiyo ilikuwa imepanga kusikiliza kesi hiyo leo, kwa wadai kutoa hoja kufafanua madai yao ya msingi na wadaiwa nao kujibu hoja za wadai.
Hata hivyo usikilizwaji huo leo Juni 24, 2025 imekwama kutokana na Jaji Mwanga anayesikiliza kutokuwepo na hivyo imeahirishwa mpaka Julai 10, 2025, itakapoendelea kwa hatua hiyo.
Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Aziza Mbaga amewaeleza wadaawa wa kesi hiyo kuwa Jaji Mwanga yuko nje ya kituo chake cha kazi kwa majukumu mengine akibainisha kuwa yuko kwenye biako vya usikilizwaji wa kesi za jinai Mahakama Kuu Masjala Ndogo Mtwara.
“Kwa hiyo shauri hili linaahirishwa mpaka Julai 10,2025, litakapoendelea mbele ya Mheshimiwa Jaji”, amesema Naibu Msajili Mbaga.
Katika kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025, wadai wanadai kuwa kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara;

Pia wanadai kuwa kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivyo wanaomba Mahakama hiyo iamuru kwamba wadaiwa wamekiuka Katiba ya chama hicho na kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019 na iwaelekeze kuzingatia sheria hiyo na Katiba yake.
Pia, wanaiomba Mahakama hiyo itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.

Amri nyingine wanazoziomba ni kusitishwa kwa muda kwa shughuli zote za kisiasa hadi hapo kutakapokuwepo na utekelezaji wa maagizo ya Mahakama, amri ya zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi adaiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika.
Vilevile wanaiomba Mahakama iamuru , wadaiwa walipe gharama za kesi hiyo na itoe nafuu nyingine yoyote ambayo itaona inafaa kuzitoa.