Dar es Salaam. Mawaziri wa Tanzania juzi usiku wametoboa siri ya namna miaka minne ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan alivyoifungua nchi, kuirudisha kwenye misingi ya Baba wa Taifa na kutoa masomo mpya kuhusu uongozi nchini.
Wakizungumza katika nyakati tofauti kwenye Kongamano la Mwananchi Jukwaa la Fikra lililoandaliwa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) jijini Dar es Salaam, mawaziri hao wametumia mfano wa ujenzi wa miundombinu ambayo ujenzi wake umekamilika, kama ushahidi mmoja wa utawala huo uliotimiza miaka minne Machi mwaka huu.
Aliyefungua mkutano huo uliokuwa na kauli mbiu ya “Kujenga Madaraja, Kujenga Nchi”, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ambaye katika hotuba yake, amezungumzia kwamba Rais Samia amekamilisha miradi yote mikubwa iliyokuwa imeanzishwa na mtangulizi wake, Hayati John Magufuli.
Ulega amesema jambo rahisi rahisi zaidi kwa Rais Samia lingekuwa ni kuanzisha miradi mingine ambayo ingempa sifa binafsi lakini aliamua kuendeleza mazuri yote ya mtangulizi, jambo lililotoa funzo kwa wanasiasa wengine nchini.
“Tukumbuke Rais Samia aliingia madarakani katika wakati ambapo dunia nzima ilikuwa inapitia magumu ya Uviko 19. Hela ilikuwa ngumu lakini jemedari wetu huyu amepambana vilivyo na sasa hatuna tunachomdai. Yale makubwa na magumu yote kayamaliza,” amesema Ulega.
Akinukuu kauli maarufu ya aliyepata kuwa Rais wa Marekani, John Kennedy, kuwa maendeleo ya taifa lolote duniani yako kwenye ujenzi wa miundombinu yake, Ulega amesema kukamilika kwa daraja la Magufuli mkoani Mwanza, reli ya SGR na Bwawa la Mwalimu Nyerere, kutachochea maendeleo katika sekta nyingine.
Maelezo hayo ya Ulega yaliungwa mkono na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo, aliyesema miradi hiyo mikubwa inakwenda kuifungua nchi katika namna zaidi ya moja.
Alisema katika sekta ya afya, itakuwa rahisi kwa wagonjwa kupata matibabu katika hospitali nzuri hata za mbali, wakulima watakuwa karibu na masoko, wanafunzi watafika shule nyakati zote na biashara zitachangamka.
Kitila amesema faida za nchi kuwa na miundombinu mizuri haziishia katika fursa za kiuchumi na kibiashara pekee, kwani hata kiakili na kisaikolojia, kuwa na miundombinu mizuri kunaleta furaha katika nchi.
“Watu wakiona daraja zuri mahali, utaona wanaenda kupiga picha. Kuna watu watasafiri kutoka mbali kwenda kuona Daraja la Magufuli, wengine kuonja uzuri wa SGR na wengine kupata umeme kwa sababu ya bwawa. Nchi yenye watu wenye furaha ni nchi nzuri,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alisema haikuwa kazi rahisi kwa serikali kutekeleza miradi hiyo ya ujenzi kama si maono na uongozi imara wa Rais Samia.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa reli ya Mwendokasi hadi Dodoma ni mafanikio makubwa na kwamba sasa mwelekeo ni kuhakikisha reli hiyo inafika hadi Mwanza na Burundi kufikia mwaka 2030.
Mbarawa alisema jambo la kuvutia ni kwamba miradi hiyo imejengwa kwa jasho na mapato ya Watanzania wenyewe, jambo ambalo limewafundisha kuhusu umuhimu wa kujitegemea linapokuja suala zima la miradi yenye maslahi makubwa kwa taifa.
Kama tungesema tusubiri misaada, hakuna ambaye angekuja kutusaidia kwa sababu kila mtu alikuwa na shida zake baada ya Uviko. Lakini Rais Samia akasema tutajifunga kibwebwe na tutapambana na matokeo yake ni hayo tuliyonayo,” amesema Mbarawa.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema kilichofanywa na Rais Samia kwenye miaka yake minne ya utawala wake kinaakisi masuala ambayo msingi wake ni Baba wa Taifa, Julius Nyerere.
Akitoa mifano, amesema ni Nyerere ndiye aliyeamua kwanza Tanzania ijenge Chuo Kikuu chake chenyewe kwa fedha zake, ndiye aliyeandaa Azimio la Arusha ambalo msingi wake mkubwa ulikuwa ni utu na aliyepanga ujenzi wa reli, na bwawa la kuzalisha umeme na kuhamisha makao makuu Dodoma.
“Leo hii, Rais Samia ni mgombea urais wa kwanza wa CCM kutumia neno utu kama sehemu ya kauli mbiu ya kuwania urais, amekamilisha reli, daraha hili na bwawa la umeme. Hizi ndizo zilikuwa ndoto za Baba wa Taifa na zimekamilika wakati wa utawala wake,” amesema Kabudi.
Kongamano hilo la siku moja lilikuwa na lengo la kujadili mafanikio, changamoto na kubadilishana mawazo na ufahamu kuhusu ujenzi mkubwa wa miundombinu unaoendelea nchini.