Ponda ajitosa ubunge Temeke | Mwananchi

Dar es Salaam. Hatimaye Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda amechukua fomu ya kuwania ubunge katika Jimbo la Temeke kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, huku akieleza sababu ya kuchagua eneo hilo na siyo kwingine.

Sheikh Ponda, kada mpya wa chama hicho, aliyejiunga Juni 5, 2025 baada ya kuchukua fomu hiyo, sasa anasubiria mchujo na watia nia wengine ndani ya chama hicho kuona kama ataibuka kinara na kuteuliwa kupeperusha bendera ya ACT-Wazalendo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Akizungumza Dar es Salaam, leo Jumanne Juni 24, 2025 baada ya kuchukua fomu hiyo, katika ofisi za Kata ya Azimio ya chama hicho, Sheikh Ponda ametaja sababu ya kuichagua Temeke.
Amesema amechagua Jimbo la Temeke, kwa sababu limeathirika zaidi na kwa kuwa bado hawajaingia kwenye kampeni ila muda ukifika atazungumza.

“Nitatoa majibu mzuri zaidi kwanini nimechagua Temeke muda wa kampeni ukianza, itoshe kusema Temeke imeathirika zaidi nataka nikawawakilishe bungeni,” amesema.

“Nashukuru kwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio langu la kuchukua fomu ya kugombea ubunge katika Jimbo la Temeke, Nimeamua kuomba ridhaa ya wananchi nchi ili nikawawakilishe bungeni kama mbunge wao,” amesema.

Amesema matumaini yake atapata uungwaji mkono katika kufanikisha hilo awe mbunge akawawakilishe kwenye chombo hicho muhimu cha kutunga sera.

“Nimechagua kuwawakilisha wananchi kupitia Chama cha ACT-Wazalendo ni muhimu kupeleka watu wanaofaa katika bunge letu, halihalisi sote tunashuhudia hali inavyoenda na yote yanasababishwa na misingi ya kisheria kutokuwa mizuri,” amesema.


Amesema eneo ambalo sheria zinatengenezwa na kutayarishwa na kupitishwa ni bungeni kwa kutambua hilo ni muhimu watu weledi na makini kuingia kwenye chombo hicho.

“Sababu hiyo imenifanya nami niingie kwenye kinyang’anyiro mwaka 2025, kuomba ridhaa kwa wananchi nikagombee uchaguzi kunafanyika Oktoba na wito wangu wananchi washiriki tukio hili muhimu na tulinde kura zetu zisiibiwe,” amesema.
 

Kwanini ubunge na si urais

Kwa mujibu wa Sheikh Ponda amesema Urais ni nafasi ya juu zaidi na ni eneo linalohitaji mkakati zaidi kuingia kwenye kinyang’anyiro chake.

“Kwakuwa naingia katika kuutaka Ubunge kwangu ni hatua ya awali katika kuufikiria urais, tambueni ubunge ni nafasi nyeti na suala la urais linahusu pia kuomba ridhaa ya wananchi lakini ni vizuri kuwasaidia wananchi hatua ya chini kuonyesha utendaji wako ili ukiomba nafasi ya juu wananchi wawe wameona utendaji wako,” amesema.

Amesema kuichaguliwa nafasi ya ubunge unapata faida mbili kwanza kuwawakilisha wananchi wa Jimbo uliogombea na mwisho unakuwa kwenye muhimili wa nchi na hujadili mambo ya Jimbo pekee bali Taifa kwa ujumla.

“Unajadili sera, uchumi kwahiyo Ubunge si nafasi ndogo lakini nataka kujenga misingi kabla ya kuutamani Urais,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu wa ACT-Wazalendo Jimbo la Temeke, Mussa Bakari amesema tangu kufunguliwa pazia hilo Sheikh Ponda ni kada wa kwanza kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.

“Ni matarajio yetu idadi itaongezeka kwani mwisho wa dirisha ni Juni 30, 2025, na shughuli hii inaenda sambamba na nafasi za udiwani katika Kata sote 13 za Temeke,” amesema Bakari.

Related Posts