Arusha. Katika kile kinachoonekana kama juhudi za viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushusha mvutano wa kisiasa kati ya Mbunge wa sasa Jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ambaye anatajwa kuweka nia yake kulitwa jimbo hilo.
Mapema leo, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Wanawake mkoani hapa, baada ya kuwasili aliwasalimia kwa kuwakumbatia wote wawili kwa pamoja huku akitabasamu akionesha kuwaunga mkono.
Jambo kama hilo lilifanywa na Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Amos Makalla wakati wa ziara yake ya kujenga chama katika mkutano aliofanya eneo la Soko Kuu katikati ya Jiji la Arusha akiwasifia Gambo na Makonda kuwa na makada wazuri na wenye uwezo wa kunadi ilani na sera za CCM.
Hatua hiyo inaonekana kutambua michango yao katika ujenzi wa CCM na utumishi wa umma ambao wote wawili kwa nyakati tofauti wameshiriki harakati za Umoja wa Vijana wa CCM, wamekuwa wakuu wa wilaya na mkoa hatua inayofanya joto la kisiasa Jimbo la Arusha Mjini kugeuka uwanja wa mapambano.
Kongamano hilo lililopewa utambulisho wa Safari ya Mwanamke Mkoa wa Arusha lililoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha pamoja na mambo mengine linalenga kutambua mchango wa wanawake kabla, wakati wa kupigania uhuru hadi sasa katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kisiasa, kiuchumi na uongozi.
Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza katika kongamano hilo amesema Rais Samia Suluhu Hassan amebeba heshima kubwa walionayo wanawake wote nchini na wanapaswa kuienzi kwa kuendelea kuunga mkono uongozi wake.
“Wanawake wa Tanzania wamefanya mambo mengi na makubwa katika kutoa michango yao kwenye ustawi wa nchi yetu, hata wakati wa harakati za kudai uhuru hawakua nyuma hata kidogo,wapo ambao majina yao yanajulikana na wapo ambao hayajukani lakini wanatambuliwa kwa ushujaa wao,”amesema Dk Nchimbi.
Amesema kielelezo cha uwezo wa kiutendaji wa mwanamke ni Rais Samia ambaye katika kipindi cha uongozi wake akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano amefanya mageuzi makubwa ya kiuchumi na kukamilisha miundombinu iliyoasisiwa na mtangulizi wake katika awamu ya tano.
“Tunafahamu Rais wetu (Samia) alishakuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya CCM kwa miaka 20, pia amekuwa Waziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Muungano na amekuwa Makamu wa Rais kwa kipindi cha miaka mitano, huo uzoefu umemuwezesha kufanya makubwa ambayo tunayaona,”amesema Dk Nchimbi.
Kuhusu Ilani ya uchaguzi mwaka huu amesema imetoa wigo mpana kwa wanawake kugombea nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali na kushiriki kwenye nafasi za maamuzi kwa sababu CCM inatambua uwezo wao.
Dk Nchimbi ameongeza kusema kuwa kwa sasa idadi ya wanawake bungeni ni asilimia 37 na inaweza kuongezeka kulingana na wanavyoonesha uwezo wao na imani aliyonayo kwao wanawake ni waaminifu na wanatekeleza majukumu yao ipasavyo.
Awali aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema ameandaa kongamano hilo baada ya kuguswa na historia ya maisha ya Mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Fatuma Karume na kumwomba aandae kongamano hilo kuwahamasisha wanawake na wasichana namna ya kukabiliana na changamoto ili kufikia malengo yao.
“Wazo la kuwa na kongamano hili lilitokana na Mama yetu, Fatuma Karume aliyekuja Arusha na wakati nazungumza naye nilijifunza mengi sana, nikaona niandae jambo kubwa ili wanawake wajifunze kupitia safari ndefu aliyopitia Mama Karume,”amesema Makonda.
Makonda alitumia nafasi hiyo kuwaaga wana Arusha akiwashukuru wakuu wa wilaya, viongozi wa dini na makundi mbalimbali ya kijamii kwa ushirikiano waliompa wakati wa uongozi wake na kuahidi kuendelea kuenzi mema yote.
“Kipekee nimshukuru Rais wetu, Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini mara mbili nimsaidie kwenye nafasi za uongozi wa Serikali yake, mtakumbuka aliteua niwe Katibu wa Itakadi na Uenezi wa CCM na baadaye kuwa Mkuu wa mkoa wa Arusha hii ni heshima kubwa kwangu,”amesema Makonda.
Katika kongamano hilo wanawake waliowahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi wanatarajiwa kueleza uzoefu wao katika nafasi za uongozi ambao aliyewahi kuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, waliowahi kuwa mawaziri, Zakhia Meghji na Dk Asha Rose Migiro na wanawake wajasiriamali wa Mkoa wa Arusha.