Dar es Salaam. Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limetiliana saini mkataba wa makubaliano (MoU) na Chama cha Kampuni Changa (TSA) ili kuwawezesha vijana wanaoanzisha kampuni zao kutambuliwa na DSE ili kuaminika na kupata mitaji.
Makubaliano hayo yamesainiwa leo Juni 24, 2025 jijini Dar es Salaam kati ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela na Ofisa Mtendaji Mkuu wa TSA, Zahoro Muhaji ili kuwasaidia na kuwaendeleza waanzilishi wa biashara (startups) na wabunifu nchini Tanzania.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya MoU hiyo, Nalitolela amesema lengo la makubaliano hayo ni pamoja na kuwezesha startups kupata maarifa ya masoko ya mitaji na kuzijengea uwezo kufikia fursa za mitaji kupitia DSE.
Ametaja malengo mengine kuwa ni kuendeleza mazingira wezeshi kwa ubunifu na uendelevu wa biashara changa, kushirikiana katika programu za mafunzo, semina, na kampeni za elimu ya kifedha na kunajenga daraja kati ya masoko ya mitaji na ulimwengu wa ubunifu.
“Startups ni injini ya mabadiliko ya kiuchumi. Zina uwezo wa kuleta teknolojia mpya, ajira kwa vijana na suluhisho bunifu kwa changamoto za kijamii. DSE, kupitia mifumo kama Enterprise Growth Market (EGM), tayari inatoa jukwaa la kukuza biashara changa kwa njia rasmi na endelevu.
“Makubaliano haya yanalenga kuhakikisha kwamba hizi startups hazikui gizani bali kwa mwanga wa maarifa, ushauri na fursa za mitaji,” amesema Nalitolela.
Amesema DSE inaamini kuwa soko la mitaji ni la kila mmoja si la kampuni kubwa pekee. Amebainisha kuwa kupitia ushirikiano huo, wanapanua wigo wa uwekezaji, wanawajumuisha vijana, wabunifu na wafanyabiashara wadogo, na wanasimama kama washirika wa maendeleo yao.
“Natoa pongezi za dhati kwa uongozi wa Tanzania Startup Association kwa maono yao ya wazi na moyo wa ushirikiano. Kwa pamoja, tunaandika ukurasa mpya wa matumaini kwa kizazi kijacho cha wajasiriamali nchini,” amesema Nalitolela.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TSA, Zahoro Muhaji amesema wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na DSE na leo wamerasimisha ushirikiano huo wenye lengo la kuwasaidia vijana.
Amesema mbali na vyanzo vya mitaji kama familia na marafiki, startups zinategemea kupata mitaji kutoka kwenye masoko la mitaji kama DSE kwa kuwa huko ndiko wanapata pesa nyingi za mitaji na pia wawekezaji wanahakikishiwa usalama wakitaka kujiondoa.
“Changamoto wanazokutana nazo vijana ni kwamba wawekezaji wanapotaka kuja kuwekeza nchini kwenye startups, wanauliza kama kampuni imesajiliwa DSE. Wakibaini kwamba haijasajiliwa, wanajiuliza mara mbili kuwekeza. Wanataka kwamba siku moja akitaka kuondoka, basi anatoa mtaji wake, na hilo linawezekana DSE,” amesema.
Ameongeza kwamba TSA wanaihitaji sana DSE na DSE pia wanawahitaji TSA kwa sababu wangependa kuona kampuni nyingi zinaingia, badala ya kufanya kazi na kampuni kubwa pekee na kuwaacha nje wabunifu wachanga.
“Tanzania tulichelewa kuingia kwenye masoko ya mitaji, kwa hiyo ni lazima tutumie nguvu kidogo kuelimisha umma kuhusu masoko ya mitaji. DSE inasaidia pia kupunguza utapeli wa baadhi ya wafanyabiashara wa pyramid system,” amesema.