Mama Karume aeleza changamoto za wanawake katika uongozi Zanzibar

Arusha. Mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mama Fatuma Karume, amesema safari ya mwanamke katika kufikia malengo yake imejaa changamoto nyingi, milima na mabonde, lakini wanawake hawapaswi kukata tamaa.

Mama Karume ametoa wito kwa wanawake kuendelea kupambana hadi wafikie nafasi za maamuzi katika jamii na taifa kwa ujumla.

Amesema licha ya mazingira yanayowakabili wanawake katika harakati zao za maendeleo, ni muhimu kwao kuwa na uthubutu, mshikamano na ujasiri ili kushinda vikwazo vilivyopo.

Akizungumza jijini Arusha leo, Juni 24, 2025, katika kongamano lililoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mama Karume amesema hali ya wanawake wa Zanzibar wakati wa ukoloni na katika kipindi cha baada ya ukoloni haikuwa rafiki kwa ustawi wa mwanamke, kijamii na kisiasa.

Amesema mazingira ya wakati huo yalitawaliwa na mfumo dume pamoja na utawala wa wakoloni, hali iliyozuia wanawake kushiriki kikamilifu katika masuala ya maendeleo na maamuzi ya kitaifa.

“Sisi wanawake wa Zanzibar tulikuwa katika hali duni sana wakati wa utawala wa Mwingereza na Sultan. Tulikumbwa na changamoto nyingi, tulilazimishwa kubaki majumbani kufanya kazi za upishi na malezi pekee. Watoto wetu waliugua na wengine walipoteza maisha kwa sababu hospitali hazikuwa na dawa wala huduma stahiki za afya,” amesema.

Amesema kutokana na magumu waliyopitia walifikia hatua ya kufanya mapinduzi ili kujikomboa kikamilifu na kuwa safari ya mwanamke iliyoanzishwa miaka mingi iliyopita, anaiombea iendelee ili wanawake wote wafikie hatima wanayoitaka.

Mama Karume amesema kuwa katika uchaguzi uliofanyika Juni 1961, uliolenga kuwashirikisha Wazanzibari katika Serikali, ni wanaume watano pekee walioteuliwa, akiwemo mume wake, Mzee Abeid Amani Karume.

Amesema baada ya uchaguzi huo kutowajumuisha wanawake katika nafasi za uongozi, Serikali ya Uingereza iliyokuwa chini ya uongozi wa Chama cha Labour ilipokea taarifa kuhusu hali hiyo.

“Kufuatia malalamiko hayo, ilimtuma ofisa wake, James Johnson kuja Zanzibar kusikiliza kilio cha wanawake na kuwasilisha taarifa hiyo kwa mamlaka za Uingereza kwa ajili ya kutafutwa suluhisho la kudumu,” amesema.

Mama Karume amebainisha kuwa mwaka huohuo wa 1961, hatua zilichukuliwa na wanawake wa Zanzibar walianza kushiriki katika uongozi kupitia Baraza la Zanzibar, jambo lililoweka msingi muhimu wa kushiriki kwa wanawake katika uongozi wa taifa.

Tangu wakati huo, amesema wanawake wameendelea kupanda ngazi mbalimbali za uongozi hadi kufikia hatua ya kupata Rais wa kwanza mwanamke kutoka Zanzibar (Rais Samia Suluhu Hassan), hii ikiwa ni ishara ya mafanikio ya juhudi za muda mrefu za wanawake katika kupigania usawa na ushiriki wa kisiasa.

“Ile ndoto nilikuwa nayo tangu nikiwa mdogo, kwamba wanawake washike nafasi ya uongozi imetimia kikamilifu kumwona Rais wa Kwanza mwanamke, Samia Suluhu Hassan, niwaombe tumpe nguvu asiwe na woga wala hofu katika uongozi wake na tuone Muungano wetu ukidumu,” amesema.

Mbunge wa sasa jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda walikuwa kivutio kwa mgeni rasmi wa kongamano hilo, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi ambaye baada ya kuwasili ukumbini, aliwasalimia na kuwakumbatia kuonyesha mshikamano.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Dk Emmanuel Nchimbi (katikati) akifurahia jambo na aliyekua Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda (kushoto) na Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo alipowasili kufungua kongamano la Safari ya Mwanamke mkoa wa Arusha leo. Picha na Mpigapicha



Jambo kama hilo lilifanywa na  Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Sekretariati ya Chama Cha Mapinduzi, Amos Makala wakati wa ziara yake ya kujenga chama katika mkutano aliofanya eneo la Soko Kuu katikati ya jiji la Arusha, ambapo aliwasifia wanasiasa hao kuwa ni makada wazuri na wenye uwezo wa kunadi ilani na sera za CCM.

Dk Nchimbi alikuwa mgeni rasmi katika kongamano la Safari ya Mwanamke lililoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Kongamano hilo, miongoni mwa malengo yake mengine, lilikuwa kutambua mchango wa wanawake katika nyanja mbalimbali kabla, wakati na baada ya harakati za kupigania uhuru  ikijumuisha nyanja za kisiasa, kiuchumi na uongozi.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Dk Nchimbi amesema Rais Samia amebeba heshima kubwa walionayo wanawake wote nchini na wanapaswa kuienzi kwa kuendelea kuunga mkono uongozi wake.

“Wanawake wa Tanzania wamefanya mambo mengi na makubwa katika kutoa michango yao kwenye ustawi wa nchi yetu, hata wakati wa harakati za kudai uhuru hawakuwa nyuma hata kidogo, wapo ambao majina yao yanajulikana na wapo ambao hayajukani, lakini wanatambuliwa kwa ushujaa wao,” amesema Dk Nchimbi

Amesema kielelezo cha uwezo wa kiutendaji wa mwanamke ni Rais Samia ambaye katika kipindi cha uongozi wake akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano amefanya mageuzi makubwa ya kiuchumi na kukamilisha miundombinu iliyoasisiwa na mtangulizi wake katika awamu ya tano.

“Tunafahamu Rais wetu (Samia) alishakuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya CCM kwa miaka 20, pia amekuwa Waziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Muungano na amekuwa Makamu wa Rais kwa kipindi cha miaka mitano, huo uzoefu umemwezesha kufanya makubwa ambayo tunayaona,” amesema Dk Nchimbi.

Kuhusu Ilani ya uchaguzi mwaka huu amesema imetoa wigo mpana kwa wanawake kugombea nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali na kushiriki kwenye nafasi za maamuzi kwa sababu CCM inatambua uwezo wao.

Dk Nchimbi ameongeza kusema kuwa kwa sasa idadi ya wanawake bungeni ni asilimia 37 na inaweza kuongezeka kulingana na wanavyoonyesha uwezo wao na imani aliyonayo kwao, wanawake ni waaminifu na wanatekeleza majukumu yao ipasavyo.

Awali, Makonda amesema alianzisha kuandaa kongamano hilo baada ya kuguswa na historia ya maisha ya, Mama Karume, mke wa Rais wa kwanza wa Zanzibar.

Kwa mujibu wa Makonda, aliomba aandae kongamano hilo kwa lengo la kuwahamasisha wanawake na wasichana juu ya namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali ili kufikia malengo yao.

“Wazo la kuwa na kongamano hili lilitokana na Mama yetu, Fatuma Karume aliyekuja Arusha na wakati nazungumza naye nilijifunza mengi sana, nikaona niandae jambo kubwa ili wanawake wajifunze kupitia safari ndefu aliyopitia Mama Karume,” amesema Makonda.

Makonda ametumia nafasi hiyo kuwaaga wana Arusha akiwashukuru wakuu wa wilaya, viongozi wa dini na makundi mbalimbali ya kijamii kwa ushirikiano waliompa wakati wa uongozi wake na kuahidi kuendelea kuenzi mema yote.

“Kipekee nimshukuru Rais wetu, Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini mara mbili nimsaidie kwenye nafasi za uongozi wa Serikali yake, mtakumbuka aliniteua niwe katibu wa Itakadi na Uenezi wa CCM na baadaye kuwa mkuu wa Mkoa wa Arusha hii ni heshima kubwa kwangu,” amesema Makonda.

Related Posts