Wananchi wanaoishi ndani ya leseni ya mgodi waandamana wakitaka kujua hatima yao

Geita. Baadhi ya wananchi wa vitongoji vya Katomaini, Magema, Mzingamo na Ikumbayaga, vilivyoko katika Mtaa wa Nyamalembo, Manispaa ya Geita, wameandamana hadi ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita wakitaka kujua lini maeneo yao yatafanyiwa tathmini na kulipwa fidia ili kuruhusu shughuli za uchimbaji madini kuendelea katika maeneo hayo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyamalembo, Bahati Gulaka, amesema kuwa zaidi ya wananchi 70 wameandamana ili kujua hatima ya maisha yao, baada ya kuishi katika eneo la leseni ya mgodi kwa zaidi ya miaka 25 bila kupata fursa za kujiendeleza.

“Tumekuja hapa madai yetu ni kujua hatma yetu tumekaa kwenye vigingi kwa miaka 25 bila kupewa majibu sahihi tunataka tutathminiwe na tujue lini tunalipwa tuondoke, Serikali imekuwa ikitupa maneno tuu lakini hadi sasa tuko kwenye mazingira magumu bila ufumbuzi sasa tunataka majibu sahihi,” amesema Gulaka.

Gulaka ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo, wananchi wameshindwa kupata huduma muhimu kama maji safi na salama, kujenga nyumba bora, wala kuendeleza shughuli za kilimo na ufugaji.

Akichangia hoja hiyo, Monica Kyunga mkazi wa eneo hilo amesema; “Tunaishi kwenye mazingira magumu hao wanaokuja kwenu na kutuzunguka na kudai wanataka kubaki ni wawapi, kwa nini wasije mbele yetu wakasema wao wanabaki sisi wengine tunaotaka kupisha shughuli za mgodi tupishe.”

Akizungumza na wananchi hao, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati, amesema suala hilo tayari lipo kwenye Wizara ya Madini, na kwamba changamoto 11 zilizoainishwa awali zimeanza kutatuliwa, ambapo nane kati ya hizo tayari zimepatiwa ufumbuzi.

“Maeneo yaliyosalia ni Nyakabaleke, Mzingamo na Magema. Tayari Waziri wa Madini, Antony Mavunde, na Mkuu wa Mkoa, Martin Shigela, wamefuatilia suala hili kwa karibu,”amesema Gombati.

Katibu tawala mkoa wa Geita Mohamed Gombati(katikati) akizungumza na wananchi wa mtaa wa Nyamalembo ambao maeneo yao yako ndani ya leseni ya mgodi walioandamana kwenda ofisi ya Mkuu wa Mkoa kutaka kujua lini maeneo yao yatafanyiwa tathmini ili kupisha shughuli za uchimbaji madini.



Amesema kuwa kutokana na mkanganyiko uliopo kati ya wananchi, Serikali na Mgodi, walipendekeza kuteuliwa mshauri elekezi huru ambaye tayari amekamilisha ripoti yake. Hivi karibuni, ofisi ya mkoa itapokea ripoti hiyo ili kujifunza mapendekezo na ushauri uliotolewa.

Gombati ameongeza kuwa Serikali inatambua kuwa huo ni mgogoro wa muda mrefu na kuwataka wananchi kuendelea kuwa na subira hadi ripoti hiyo itakapowasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana ili kutoa maelekezo ya mwisho na kufunga suala hilo.

Akizungumza kwa simu, Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti anayeshughulika na masuala ya uendelevu na mahusiano barani Afrika, Simon Shayo, amesema sheria ya madini hairuhusu watu kuishi ndani ya mita 200 kutoka kwenye eneo linalofanyiwa kazi ya uchimbaji, lakini maeneo yanayolalamikiwa hayako ndani ya kipimo hicho.

“Sheria haikatazi wananchi kuendelea kuishi kwenye eneo la leseni ambalo halijaanza kufanyiwa kazi. Tunataka kila mmoja asikilizwe, wale wanaotaka kuondoka na wanaotaka kubaki. Lengo letu ni kuhakikisha kila mmoja anapata haki yake bila kuumia, iwe ni sisi au wananchi,” amesema Shayo.

Hata hivyo, Shayo amesema kuna baadhi ya wananchi wameanza kuvunja sheria kwa kuanza kuchimba katika maeneo ya leseni bila ruhusa na kuwataka waheshimu sheria kama kampuni hiyo inavyoheshimu haki za wamiliki wa ardhi.

Related Posts