Simba inavyousaka ufalme 2024/25 | Mwanaspoti

KATIKA historia ya soka la Tanzania, Simba ni miongoni mwa klabu zenye mafanikio makubwa na mvuto wa mashabiki, huku ikiwa na upinzani wa jadi na Yanga.

Baada ya msimu wa 2023/2024 kumalizika kwa majonzi huku Simba ikimaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara nyuma ya Yanga na Azam, wengi walidhani huenda zama za utawala wa klabu hiyo zilikuwa zimefikia mwisho.

Hata hivyo, msimu wa 2024/2025 umeonyesha sura mpya ya Simba ikiwa na kikosi kilichopambwa kwa wachezaji mahiri, mbinu mpya za kiufundi na kiu kubwa ya kurejesha heshima ya klabu hiyo.

Ikiwa leo Jumatano timu hiyo inakwenda kucheza mechi ya mwisho ya ligi iliyobeba hatma ya ubingwa dhidi ya Yanga, huu hapa mwenendo wa Simba kwa kuzingatia maeneo manne, nafasi yake kwenye msimamo kwa sasa, umuhimu wa mechi iliyobaki, kiwango chao kulinganisha na msimu uliopita, mchango wa mchezaji wao bora msimu huu pamoja na kauli ya kocha Fadlu Davids kuhusu mipango ya timu kuelekea kumalizika kwa msimu.

Simba kwa sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 78. Ipo nyuma ya vinara wa ligi, Yanga yenye pointi 79 – zote zikicheza mechi 29.

Kwa hesabu za haraka endapo Simba itashinda mchezo dhidi ya Yanga itafikisha pointi 81. Hii ni zaidi ya idadi ya pointi 80 zilizoipa Yanga ubingwa msimu uliopita, hivyo Simba itaondoa utawala wa Yanga kwa misimu mitatu na kubeba ubingwa wa ligi tangu mara ya mwisho ilipofanya hivyo msimu wa 2020/21.

Kama kuna jambo linalothibitisha kwamba Simba imefufuka msimu huu, basi ni kiwango chake cha uchezaji, idadi ya mabao na uimara wa safu ya ulinzi. Msimu huu umeonyesha Simba tofauti kabisa na ile ya msimu uliopita.

Hadi sasa Simba imeshafunga mabao 69 katika mechi 29. Hii inamaanisha ina wastani wa mabao 2.37 kwa mchezo mmoja. Ikilinganishwa na msimu uliopita ambapo ilifunga mabao 59 katika mechi 30, wastani ikiwa 1.97.

Mabao hayo yamegawanywa kati ya washambuliaji, viungo na hata mabeki ikionyesha namna timu inavyocheza kwa pamoja.

Simba pia eneo la ulinzi limeimarika kulinganisha na msimu uliopita ambapo iliruhusu mabao 25 katika mechi 30. Msimu huu katika mechi 29, imeruhusu mabao 11, ikiwa timu ya pili kuruhusu mabao machache zaidi nyuma ya Yanga (10). Msimu uliopita ilikuwa timu ya tatu kwa kuruhusu mabao machache nyuma ya Yanga (14), Coastal Union (19) na Azam (21).

Mabeki Che Malone Fondoh, Abdulrazak Hamza, Mohamed Hussein, Shomary Kapombe na kipa Moussa Camara wamekuwa miamba isiyopenyeka kirahisi msimu huu.

Katika mafanikio yotr hayo, mbinu za kocha Fadlu Davids zimeifanya Simba kuwa timu inayocheza kwa kasi, nidhamu, na uwiano mzuri kati ya ulinzi na mashambulizi. Timu hiyo inatumia mfumo wa 4-2-3-1 unaobadilika kwa haraka kuwa 4-3-3 wakati wa kushambulia, hali inayowawezesha kumiliki mpira na kushambulia kwa idadi kubwa ya wachezaji.

Katika kila msimu, huwa kuna nyota mmoja anayeinua timu na kuwa kitovu cha mafanikio yake. Kwa upande wa Simba msimu huu, jina hilo ni Jean Charles Ahoua. Kiungo mshambuliaji huyu kutoka Ivory Coast ameonesha kiwango cha juu, kasi, na uwezo wa kufunga kwa njia mbalimbali.

Hadi sasa, Ahoua ana mabao 16 katika ligi na ndiye anayeongoza orodha ya wafungaji. Ana uwezo wa kucheza kama mshambuliaji wa pili na kiungo mchezeshaji, mara nyingi ameonekana kuwatesa mabeki wa timu pinzani kwa mbinu zake za kujipanga, kuingia kwenye nafasi na kumalizia kwa ustadi mkubwa. Kwa upande wa washambuliaji, Steven Mukwala ameifungia timu hiyo mabao 13 sawa na Leonel Ateba.

Kwa ujumla, wachezaji hao watatu wanaocheza eneo la kushambulia wamechangia mabao 42 kati ya 69, sawa na asilimia 64.3. Hii inaonesha Simba msimu huu ina safu bora ya ushambuliaji tofauti na msimu uliopita ambapo ilikosa mshambuliaji aliyefikisha mabao 12.

Kocha wa Simba SC, Fadlu Davids, amewapongeza wachezaji kwa kujituma na kufuata maelekezo, huku akisisitiza kuwa bado kazi haijaisha akisisitiza lengo kuu ni kutwaa ubingwa.

Pia kocha huyo amesema huu ni wakati wa kulipa kisasi kwa niaba ya klabu, wachezaji na mashabiki waliovumilia mateso kwa misimu mitatu mfululizo.

“Tumepoteza mataji matatu mfululizo. Lakini sasa, baada ya miezi kadhaa ya kazi ngumu, tuna nafasi ya kuwa mabingwa kwa kushinda mechi moja. Ni jambo kubwa mno,” amesema Fadlu na kuongeza.

“Kama mtu angeniletea karatasi wakati nakuja na kuniambia ‘Kocha, kuna mechi moja tu mwishoni mwa msimu itakayoamua ubingwa,’ ningesaini papo hapo. Hii ndiyo hiyo mechi. Ni sasa au kamwe.”

Kwa upande wa Mukwala, amesema: “Hatupambani kwa pointi tu, tunapigania hadhi ya klabu, tunapigania historia yetu, tunapigania mashabiki wetu waliovumilia miaka mitatu ya maumivu.

“Tunajua mashabiki wanatufuatilia. Tunajua wana imani nasi. Sasa ni zamu yetu kurudisha upendo huo kwa kuwapigania. Siwezi kusema mengi, lakini naahidi tutapambana kwa damu na jasho.”

Naye Ahoua amesema: “Tutafanya kila ambacho kitawezekana kwa ajili ya mashabiki wetu ambao wamekuwa wakituunga mkono. Binafsi sina presha na nipo tayari kwa mchezo huo mkubwa, itakuwa ni heshima kwetu kumaliza msimu na ubingwa wa ligi.”

Related Posts