Tusiruhusu tena Bunge lisilo na kambi rasmi ya upinzani

Bunge la 12 linakaribia kuvunjwa hivi karibuni. Hii ni makala ya kuwaomba Watanzania tusiruhusu tena Bunge lisilo na kambi rasmi ya upinzani, kama ilivyokuwa kwa Bunge hili la 12. Kutokuwepo kwa kambi thabiti ya upinzani kumelifanya Bunge hili likose hoja kinzani zenye mashiko na mvuto masikioni mwa wasikilizaji na watazamaji.

Hata ikitokea kwamba Watanzania, kwa mapenzi yao kwa chama wanachokipenda wataichagua CCM pekee kwenye uchaguzi ulio huru, wa haki na unaosimamiwa na Tume Huru na shirikishi, huo utakuwa ni uamuzi wa walio wengi, tutauheshimu.

Hata hivyo, tutamuomba Rais ajaye awateue wapinzani makini kwenye zile nafasi zake 10 za uteuzi, ili kutoa meno kwa Bunge liweze kutekeleza kikamilifu jukumu lake la kuisimamia Serikali.

Tunataka Bunge lijalo liwe ni Bunge lenye meno, lenye uwezo wa kuikosoa na kuirekebisha Serikali pale inapoenda mrama.

Mimi nilianza kupiga kura tangu uchaguzi wa mwaka 1990, wakati huo wa mwisho wa chama kimoja, tulikuwa tukimpigia kura mgombea pekee wa urais anayeshindana na kivuli.

Lakini tunapoelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, ni wakati muafaka kufanya jitihada za makusudi kuhakikisha hatupati tena Bunge la vyama vingi jina tu, kama ilivyokuwa kwa Bunge hili la 12 lililokosa kambi rasmi ya upinzani.

Tunapaswa kufungua zaidi milango ya demokrasia ya kweli, kuwapa nafasi wagombea wa kweli wajitokeze, washindane kwenye uchaguzi wa haki, sawa, bila wagombea wa chama kimoja kushindana na wagombea vivuli na kushinda kwa urahisi.

Nimeshiriki chaguzi mbalimbali nikiwa mwandishi wa habari na wakati mwingine mwangalizi wa uchaguzi, ukiwamo ule wa Marekani mwaka jana.

Huko unaweza kushuhudia demokrasia halisi inayoanzia kwenye mchujo wa awali. Tanzania inapaswa kufika wakati wa kufanya chaguzi za kweli, si maigizo ya uchaguzi.

Nimebahatika kushiriki pia chaguzi zote za vyama vingi nchini tangu tuliporejesha mfumo huo mwaka 1992, naona kuna haja ya kutoa ushauri wa busara unaoweza kusaidia kuboresha mchakato wa kuelekea uchaguzi huu wa 2025.

Baada ya Uchaguzi wa 2020, wakati idadi ya wabunge wa upinzani haikufikia kigezo cha kambi rasmi, nilishauri turekebishe kanuni ili wabunge wachache wa upinzani waunde kambi ya wachache wakiibeba nafasi ya kambi rasmi ya upinzani.

Hili ni jambo la kawaida kwenye mabunge ya Jumuiya ya Madola, ambako kamati za usimamizi huongozwa na upinzani ili kuisimamia Serikali kwa ukamilifu.

Hivyo nionavyo mimi, endapo upinzani ukikosekana, basi Rais ajaye awateue wapinzani makini kushika nafasi hizo.

Sheria ya Uchaguzi iliyopita ilikuwa na vipengele vinavyokwenda kinyume cha Katiba na Mahakama Kuu ikavibatilisha.

Serikali ya wakati huo ilileta Muswada wa Marekebisho ya Katiba kwa hati ya dharura na ‘kuchomeka’ vipengele batili ndani ya Katiba. Mahakama Kuu ilisimama imara, ikisisitiza kuwa sheria hiyo ni batili na mabadiliko hayo kwenye Katiba yaliyopitishwa kwa mtindo batili pia ni batili.

Mahakama ya Rufani, kwa heshima yake kwa Bunge, ililitaka liondoe ubatili huo, lakini hadi leo Bunge limegoma kufanya hivyo.

Baada ya Rais Samia kuingia madarakani, aliunda Kikosi Kazi na wengi walipendekeza mabadiliko madogo ya Katiba yafanyike.

Hata hivyo, Bunge halikufanya hivyo na badala yake limetunga Sheria mpya ya Uchaguzi (Na. 2 ya 2024), ikiwa na ubatili ule ule. Huenda kama kungekuwa na Kambi Rasmi ya Upinzani, hili lisingetokea.

Bunge halina mamlaka ya kubadilisha Katiba kupitia sheria ya kawaida. Katiba inabadilishwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba pekee. Bunge hili limeunda Sheria Na. 2 ya 2024, inayoanzisha INEC (Tume Huru ya Uchaguzi), huku likitumia Ibara ya 74(1) ya Katiba ambayo bado inaitaja NEC pekee.

Ili kuhalalisha INEC, ingelazimika kwanza kufanya mabadiliko madogo ya Katiba, kubadilisha neno NEC kuwa INEC, ndipo Bunge lingetunga sheria hiyo.

Hata Ibara ya 98 (1) na (2) inapaswa kubadilishwa ili kuongeza neno “Huru” kwenye jina la Tume ya Uchaguzi. Endapo kungekuwa na Kambi Rasmi ya Upinzani, haya yasingetokea.

Nasubiri kwa hamu kuona chapisho jipya la Katiba, likiongeza neno “Huru” kwenye jina la Tume ya Uchaguzi, kisha tujiulize ni nani mwenye mamlaka ya kuongeza hata herufi moja kwenye Katiba bila mchakato wa kikatiba.

Kama Bunge hili limeisha likikosa Kambi Rasmi ya Upinzani na kama Watanzania wakiamua tena kuchagua Bunge la chama kimoja pekee, huo utakuwa ni uamuzi wao. Lakini tutamuomba Rais ajaye alinusuru Bunge letu, liwe ni Bunge lenye meno na lenye uwezo wa kuisimamia Serikali kwa ukamilifu.

Tanzania bado haina upinzani imara, hivyo CCM na Serikali yake wanapaswa kubeba jukumu la kusaidia mchakato wa kugawa ‘nusu mkate’ ili kuruhusu uwanja mpana wa uchaguzi kuwa sawa kwa vyama vyote.

Hapo ndipo mshindi atakapopatikana kwa haki, na sote tutafurahia matokeo.

Kwa mtazamo wangu, figisu na mizengwe iliyotokea wakati uliopita inaweza kuwa chanzo cha karma mbaya iliyosababisha matukio yasiyopendeza. Tusipojirekebisha wakati huu wa 2025, tutapata Bunge kama la 2020 na matukio kama yale yanaweza kujirudia.

Related Posts