Mkeka wa Samia, kibano CCM vyakoleza moto majimboni

Dar es Salaam. Baada ya tetesi zilizodumu kitambo, hatimaye rasmi viongozi wa Serikali waliohusishwa na nia za kuutaka ubunge katika majimbo mbalimbali, wameondolewa kwenye nafasi zao, huku wadau wa siasa wakisema, uamuzi huo umelenga kuweka mizania sawa miongoni mwa wagombea.

Hatua ya kuondolewa kwa viongozi hao, ambayo inakuja zikiwa zimesalia siku tano kabla ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kuanza rasmi mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu kwa makada wake wanaotaka kuwania ubunge, udiwani na uwakilishi, inatajwa kuongeza joto  na ushindani majimboni.

Viongozi hao ni wakuu wa mikoa, wilaya, taasisi na watendaji wakuu wa wizara, ambao awali gazeti hili, liliripoti kuhusu nia zao za kugombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Waliowekwa kando, kwa mujibu wa taarifa ya uteuzi iliyotolewa juzi ni Paul Makonda aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Peter Serukamba (Iringa), Juma Homera (Mbeya), Daniel Chongolo (Songwe) na Thobias Andengenye (Kigoma).

Ukiacha wakuu wa mikoa, viongozi wengine walioachwa kwenue uteuzi huo ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe.

Makonda ambaye mwaka 2020 najitosa jimbo la Kigamboni, safari hii ahusishwa na jimbo Arusha Mjini lakini hajaweka bayana anaelekea wapi; Chongolo anatajwa Jimbo la Makambako, Homera (Namtumbo), Serukamba (Kigoma Kaskazini) na Andengenye (Busokero).

Katika mkeka huo, Rais Samia amemhamisha Kenan Kihongosi kutoka Simiyu kwenda Arusha kuchukua nafasi ya Makonda, IGP mstaafu Simon Sirro anakwenda Kigoma  kurithi kiti cha Andengenye wakati Beno Malisa, aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mjini amepandishwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Mbeya.

Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Jabir Makame amepanda kuwa mkuu wa Mkoa wa Songwe na Kheri James, aliyekuwa mkuu wa Wilaya Iringa amepanda na kuwa mkuu wa mkoa Iringa. Agnes Meena amerithiti nafasi ya Profesa Shemdoe huku Machibya Masanja akimrithi Kadogosa TRC.

Baada ya kuondolewa, Chongolo kupitia ukurasa wake wa Instagram ameandika kumshukuru Rais Samia kwa kumwamini kwenye nafasi hiyo na wananchi wa Songwe kwa ushirikiano wao, huku akidokeza kuwa anarudi nyumbani Njombe.

“Nimehitimisha utumishi wangu. Kijiti nakikabidhi kwa mdogo wangu mkubwa Mh. Jabir Makame, mhifadhi wa maisha. narudi nyumbani Njombe,” aliandika.

Ingawa taarifa ya Ikulu haikuweka bayana, duru za kisiasa zinaeleza hatua hiyo ni utekelezaji wa witoa wa Rais Samia Machi 11, 2025, akiwataka wateule wake wanaotaka kugombea watoe taarifa mapema ili nafasi zao zirithiwe na walio chini yao.

“Nilimwambia katibu mkuu kiongozi, peleka sekula serikali za mitaa, yeyote mwenye nia ya kugombea atwambie mapema ili tumpandishe wa chini yake ashike ile nafasi. Hatutaki pale wakati fomu zinatoka watu wote wanakimbia kwenda kuchukua fomu na mnatuacha serikali za mitaa hazina wasimamizi.

“Mnabakia kujaza watu ambao hawana uzoefu. Lakini tukijua mapema tutatayarisha watu wa kujaza hizo nafasi, kuwapa miongozo, kuwafanyia mafunzo ili wawe tayari kukabiliana na uchaguzi. Sasa usipojisema mapema ukija kuchukua fomu mbele umekosa yote,” alionya.

Hatua hiyo inaelezwa na Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (Dartu), Dk Lazaro Swai kuwa majimboni kutakuwa na ushindani kwa kuwa wateule hao ni viongozi wenye nguvu na walionekana kuwekeza nguvu.

“Wakati mwingine inaweza kusababisha wabunge waliokuwa katika nafasi hizo, wakashindwa kurudi katika majimbo yao,” alisema.

Hayo yametokea, ikiwa tayari CCM imetangaza kuwa, Juni 28 hadi Julai 2, mwaka huu, ndiyo mwanzo na mwisho wa mchakato wa wagombea wa nafasi mbalimbali za ubunge, udiwani na uwakilia.

Takriban wiki moja kabla ya kipenga kupulizwa, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amepiga marufuku wagombea ndani ya chama hicho, kuitisha vikao, warsha, ziara na makongamano na wajumbe watakaopiga kura za maoni, jambo linaloongeza joto la uchaguzi huo.

Marufuku hiyo, imekuja miezi kadhaa baada ya chama hicho, kuweka kibano kwa wagombea wake, kwa kuongezea idadi ya wajumbe wataoshiriki kupiga kura za maoni.

Yote hayo kwa mujibu wa wataalamu wa siasa, yanalenga kupunguza vitendo vya rushwa kuelekea mchakato wa ndani wa chama hicho na kuweka mizania sawa miongoni mwa wagombea.

Akizungumzia hilo, Mchambuzi wa Masuala ya Siasa, Kiama Mwaimu alisema kuondolewa kwa wateule wenye nia ya kugombea, kunalenga kuweka mizania sawa kati yao na wagombea wengine.

Alitolea mfano kwa nafasi kama ya mkuu wa mkoa, anapoachwa aendelee na wadhifa wake hadi muda wa kuchukua fomu, atakuwa na ushawishi zaidi ukilinganisha na wagombea wasio na nafasi.

“Mkuu wa Mkoa ana ushawishi, lakini anaogopwa kwa nafasi yake, ukimuacha na nafasi yake kuna uwezekano akachaguliwa kwa sababu ya ukuu wa mkoa alionao. Lakini ukimwondoa unaruhusu watu wampime kwa uhalisia wake,” alisema.

Kwa ujumla kilichofanywa na mamlaka ya uteuzi na katazo lililotolewa na CCM, alisema shabaha yake ni kuweka mizania sawa miongoni mwa wagombea na kudhibiti rushwa.

Kwa upande wa Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Sabatho Nyamsenda alitoa tafsiri mbili kuhusu uamuzi wa CCM na mamlaka ya uteuzi.

Kuhusu marufuku ya CCM, alisema pengine imeona kuna kundi lililojilimbikizia fedha kujipanga kununua uongozi na kwamba tayari limeshaonekana kuwa tishio. Ili kulidhibiti, alisema CCM imeamua kuendelea kuweka mazingira magumu ya rushwa katika michakato yake, ili kutengeneza mazingira sawa kwa wagombea wote.

Ukiacha sababu hiyo, alisema uamuzi huo unalenga kudhibiti rushwa na hatimaye wapatikane wagombea kwa sababu wamekidhi kuzipata nafasi husika.

Nyamsenda alisema yote yanayoendelea ni dalili kuwa uchaguzi umewadia. Hata hivyo, utaratibu wa viongozi kuondolewa katika nafasi zao ili wakagombee ni kawaida.

“Kwa mwenendo unaoendelea hasa katika mabadiliko yaliyofanywa na CCM kuongeza wigo wa watu wanaotakiwa kupiga kura ni wazi kuwa chama hicho kimepanga kudhibiti rushwa,” alisema.

Alisema kwa muda mrefu kumeonekana viongozi mbalimbali wakitoa misaada, kuitisha mikutano na wajumbe na vikao mbalimbali wakitoa zawadi, mambo ambayo ni rushwa.

Hata hivyo, alisema katika uchaguzi wa mwaka huu, CCM imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kustukiza, inabidi kufanyike utafiti wa kina ili kubaini undani wake.

“Hili la kuzuia vikao nalo limekuja kustukiza lakini kama limekuja kudhibiti rushwa au kundi fulani lililojilimbikizia nguvu za kifedha na limeonekana kuwa tishio kwa kundi lililopo madarakani,” amesema Nyamsenda.

Related Posts