Zimekuwa ni siku 13 za mshikemshike mashariki ya mati baada ya mataifa ya Israel na Iran kushambuliana kwa makombora, vita ambayo imezihusisha nchi za Qatar na Marekani na kusababisha vifo na uharibifu wa mali.
Juni 13, 2025, Israel ilianza kuishambulia Iran kwa makombora yake ikilenga vinu vya nyuklia na makamanda wa Jeshi la Iran ambao waliuawa katika mashambulizi hayo yaliyosababisha madhara kwa taifa la Iran.
Katika kulipiza kisasi, Iran iliishambulia Israel hasa katika mji wa Tel Aviv kwa mfululizo wa makombora, hata hivyo makombora mengi yaliharibiwa angani huku kombora moja likipenya na kutua katika mji wa Tel Aviv.

Wakati hali hiyo haijapoa, Marekani nayo ikajitosa katika vita ya wababe hao wa mashariki ya kati kwa kushambulia maeneo matatu ya Irani ambayo ndiko kuna vinu vya nyuklia vya Iran.
Rais wa Marekani aliutangazia ulimwengu kwamba wameendesha operesheni maalumu ambapo kwa kutumia ndege za Jeshi la Marekani, wamefanikiwa kuharibu vinu vya nyuklia katika maeneo ya Fordow, Natanz na Isfahan
Iran haijakubali. Iliapa kulipiza kisasa kwa Marekani na Juni 23, 2025, ilikishambulia kituo cha kijeshi cha Marekani kilichopo Qatar. Hata hivyo, sehemu kubwa ya makombora yake yalidhibitiwa, isipokuwa kombora moja ambalo lilipenya, hata hivyo halikusababisha madhara.
Ijumaa ya Juni 13, 2025, Israeli ilianzisha mashambulizi makali katika ngome kuu ya nyuklia na kijeshi nchini Iran, ikitumia ndege za kivita na droni ambazo zilikuwa zimesafirishwa kwa siri kuingia nchini humo, kushambulia vituo muhimu na kuwaua majenerali na wanasayansi wakuu.

Israeli ilidai kuwa mashambulizi hayo yalikuwa ya lazima kabla adui yao hajakaribia kutengeneza silaha ya nyuklia, ingawa wataalamu na Serikali ya Marekani walikuwa wamekadiria kuwa Iran haikuwa inafanya kazi ya kutengeneza silaha hiyo kabla ya mashambulizi hayo.
Takribani watu 80 walipoteza maisha kwenye mashambulizi hayo ya Israel. Maofisa wa Israeli wameendelea kushikilia kwamba mashambulizi yao dhidi ya vituo mbalimbali vya nyuklia na kijeshi vya Iran yalikuwa ya lazima.
Sababu kadhaa zimetolewa kwa umma wa Israeli kama sababu ya mashambulizi hayo, hata hivyo hakuna hata moja inayofafanua sababu halisi zilizolifanya serikali ya Israeli kuanzisha shambulizi hilo la upande mmoja, bila uchokozi wa moja kwa moja wa Iran.
Serikali ya Israel inadai kuwa shambulizi hilo lilikuwa “la kuzuia”, likilenga kuondoa tishio la haraka na lisiloepukika kwamba Iran ingetengeneza bomu la nyuklia. Hata hivyo, hakuna ushahidi wa kuthibitisha dai hilo.
Kwa mujibu wa Al Jazeera, shambulizi hilo linaonekana kuwa lilipangwa kwa umakini mkubwa kwa muda mrefu. Shambulizi la kuzuia kwa kawaida lazima liwe na kipengele cha kujilinda, ambacho kwa upande wake hutokana na hali ya dharura. Hakuna dharura ya aina hiyo iliyoonekana kutokea.
Zaidi ya hayo, Israeli imependekeza kuwa ripoti ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Nyuklia (IAEA) iliyotolewa Juni 12, ambayo iliikosoa Iran kwa kukiuka masharti ya Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia (NPT) hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000, ndiyo iliyoleta hali ya dharura hiyo.
Lakini hata IAEA yenyewe inaonekana kupinga madai hayo. Hakuna kipya kilichoelezwa katika ripoti hiyo ambacho hakikujulikana kwa pande husika.
Serikali ya Israeli pia imependekeza, katika muktadha wa shambulizi la “kuzuia,” kwamba lengo lilikuwa “kukata kichwa” katika mpango wa nyuklia wa Iran.
Hata hivyo, kuna makubaliano ya jumla miongoni mwa wataalamu na watunga sera kwamba Israel haina uwezo wa kuharibu mpango huo wa nyuklia, hasa ikiwa itatekeleza shambulizi hilo pekee yake bila msaada.
Saa kadhaa baada ya kushambuliwa, Iran ililipiza kisasi kwa kurusha makombora ya masafa marefu kuelekea Israeli, ambapo milipuko ilionekana iking’aa juu ya anga la Jerusalem na Tel Aviv na kutetemesha majengo chini.

Kwa mujibu wa Associated Press (AP), Jeshi la Israeli liliwahimiza raia, ambao tayari walikuwa wamevurugwa na wimbi la kwanza la makombora, kuingia mafichoni, huku makombora yakiharibu nyumba na kuua watu wawili.
Iran ilirusha makombora mengi kuelekea Israeli usiku wa Ijumaa Juni 13 hadi Jumamosi asubuhi. Hospitali moja huko Tel Aviv iliwapokea watu saba waliojeruhiwa kutokana na mashambulizi ya pili ya makombora ya Iran; wote isipokuwa mmoja walipata majeraha madogo.
Huduma ya Zimamoto na Uokoaji ya Israeli ilisema walijeruhiwa wakati kombora lilipopiga jengo moja jijini humo.
Saa chache baadaye, kombora la Iran liligonga karibu na makazi katika mji wa Rishon Lezion, katikati mwa Israeli, na kuua watu wawili na kuwajeruhi wengine 19, kwa mujibu wa huduma ya dharura ya Magen David Adom. Huduma ya zimamoto iliripoti kuwa nyumba nne ziliharibiwa vibaya.
Huduma za dharura za Israeli zilisema watu 34 walijeruhiwa katika mashambulizi ya kombora katika eneo la Tel Aviv, akiwemo mwanamke mmoja aliyepata majeraha mabaya baada ya kufunikwa na kifusi.
Katika mji wa Ramat Gan, mashariki mwa Tel Aviv, mwandishi wa shirika la Associated Press aliona magari yaliyoungua na nyumba tatu zilizoharibika, moja ikiwa imebomoka kabisa upande wa mbele.
Maofisa wa Marekani walisema kuwa mifumo ya ulinzi wa anga ya ardhini ya Marekani katika eneo hilo, ilisaidia kuangusha makombora ya Iran.
Mashambulizi ya anga yanayoendelea ya Israeli pamoja na oparesheni za kijasusi, pamoja na kisasi cha Iran, vimezua hofu ya kuzuka kwa vita kamili kati ya mataifa hayo mawili, na kusababisha hali ya taharuki zaidi katika ukanda huo uliojaa mvutano.
Israeli imekuwa ikitishia kufanya shambulio la aina hii kwa muda mrefu, na serikali mbalimbali za Marekani zimekuwa zikijaribu kuzuia hilo, zikiogopa kuwa huenda likazua vita kubwa zaidi Mashariki ya Kati na huenda lisifanikiwe kuharibu mpango wa nyuklia wa Iran uliotawanyika na kulindwa sana.
Hata hivyo, mfululizo wa matukio yaliyochochewa na shambulizi la Hamas la Oktoba 7, 2023, pamoja na kuchaguliwa tena kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, uliweka mazingira yaliyoiwezesha Israeli kutekeleza vitisho vyake.
Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alisema Marekani ilijulishwa kabla ya mashambulizi hayo.
Ngome ya Marekani yashambuliwa
Jeshi la Ulinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) lilisema katika taarifa yake kuwa lilifanya “shambulizi kali na la kuharibu kwa makombora” kama sehemu ya operesheni ya kutangaza ushindi, kujibu “uvamizi wa wazi wa kijeshi” wa Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran.

IRGC pia ilisema kuwa “hatua yao madhubuti” ilituma ujumbe kwa Ikulu ya Marekani na washirika wake kuwa Iran haitavumilia uvamizi wowote dhidi ya mipaka yake, mamlaka yake, au usalama wake wa taifa.
“Mabasi ya Marekani na vifaa vyake vya kijeshi vinavyohamishika katika eneo hili si sehemu za nguvu, bali ni sehemu ya udhaifu,” ilionya taarifa hiyo.
Iran ilisema ililenga Kituo cha Kijeshi cha Al Udeid huko Qatar kwa sababu “ndicho kituo cha amri cha Jeshi la Anga la Marekani na ndiyo rasilimali kubwa zaidi ya kimkakati ya jeshi la Marekani katika Asia Magharibi.”
Tehran pia ilisisitiza kuwa shambulizi hilo la makombora lilielekezwa mbali na maeneo ya makazi nchini Qatar.
“Hatua hii haileti tishio lolote kwa nchi rafiki na ya kindugu, Qatar, na watu wake wa heshima, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kujitolea kulinda na kuendeleza uhusiano mzuri na wa kihistoria na Qatar,” lilisema Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran.
Kwa mujibu wa Al Jazeera, Al Udeid ndicho kituo kikubwa zaidi cha kijeshi cha Marekani katika Mashariki ya Kati, kikihifadhi takriban wanajeshi 10,000 wa Marekani.
Kituo hicho chenye ukubwa wa hekta 24 (ekari 60), kiko jangwani kusini magharibi mwa mji mkuu wa Doha, na kilianzishwa mwaka 1996. Kinatumika kama makao makuu ya Kamandi ya Kati ya Marekani, ambayo inaelekeza operesheni za kijeshi za Marekani katika eneo kubwa kutoka Misri hadi Kazakhstan.
Kituo hicho, pia, kinahifadhi Jeshi la Anga la Qatar, Jeshi la Anga la Marekani, Jeshi la Anga la Uingereza na majeshi mengine ya kigeni.
Ofisa mmoja wa ulinzi wa Marekani, akizungumza na shirika la habari la Reuters, alisema kuwa “Kituo cha Al Udeid kilishambuliwa kwa makombora ya masafa mafupi na ya kati kutoka Iran.”
Wizara ya Ulinzi ya Qatar ilisema kuwa mifumo yake ya ulinzi wa anga iliweza kuzuia makombora ya Iran yaliyolenga kituo hicho.
Qatar ilisema ilipokea taarifa kuwa vituo vya kijeshi katika eneo hilo vilikuwa vinashambuliwa, ikiwemo Al Udeid.
“Saa 1:30 jioni (1630 GMT), tulipokea ripoti kuwa makombora saba yalirushwa kutoka Iran kuelekea kituo cha Al Udeid,” maofisa wa Qatar walieleza katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu. Walithibitisha kuwa kituo hicho kilihamishwa kabla ya mashambulizi.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar ililaani shambulizi hilo, ikisema kuwa ni “ukiukaji wa mamlaka na anga ya Qatar pamoja na Katiba ya Umoja wa Mataifa”, na kwamba Doha ina haki ya kujibu.
Wizara ya Ulinzi ya Qatar ilithibitisha kuwa tukio hilo halikusababisha vifo wala majeruhi.
Katika mkutano mwingine wa waandishi wa habari, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Qatar ilisema kuwa jumla ya makombora 19 yalirushwa kutoka Iran. Iliongeza kuwa ni kombora moja tu ndilo lililolipiga kituo cha Al Udeid, bila kusababisha majeruhi.
“Tunajivunia majibu yetu kwa shambulio la leo na hakuna uharibifu ulioripotiwa,” walisema maofisa wa Qatar.