Dar es Salaam. Tanzania iko mbioni kuwa mdau katika soko la kimataifa la madini muhimu kupitia ukuzaji uwezo wa kuchunguza na kusimamia madini yenye thamani yanayohitajika katika teknolojia za kisasa kama magari ya umeme na nishati mbadala.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya ushirikiano wa Serikali na wataalamu wa jiolojia kutoka nje ya nchi wenye lengo la kufanya uchunguzi sambamba na uchakataji na uongezaji thamani madini hapahapa nchini.
Hayo yanajiri kwenye mpango wa utafiti wa kisayansi na ushirikiano wa wataalamu kutoka Afrika na Ulaya kijiolojia (PanAfGeo+) ambapo mkutano uliofanyika jana Juni 24, 2025 jijini Dar es Salaam umewakutanisha wataalamu hao pamoja na Serikali.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa PanAfGeo+, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amesema utajiri wa Tanzania wa madini muhimu kama vile grafiti, nikeli na elementi adimu za ardhini unaiweka nchi mstari wa mbele katika mabadiliko ya soko la kimataifa.
“Pamoja na kuongezeka kwa mahitaji ya kimataifa ya madini haya, Tanzania inazidi kuwa kivutio kwa wawekezaji katika mnyororo mzima wa thamani wa madini,” Mbibo amefafanua.
Wakati akiyasema hayo tayari ripoti zinaonesha mchango wa sekta ya madini nchini Tanzania katika uchumi wa taifa unaendelea kukua. Kufikia 2024, sekta hiyo ilichangia asilimia 10.1 ya Pato la Taifa, ikilinganishwa na asilimia 7.1 mwaka 2021, tayari imepita lengo la asilimia 10 la mwaka 2025.
Mbibo ambaye amemuwakilisha Waziri wa Madini, amesema sekta ya madini Tanzania inachangia kwa kiasi makubwa katika pato la taifa na ongezeko la uhitaji wa madini hayo duniani kunazidi kuiweka nchi katika ramani nzuri.
Hata hivyo, ili kuvutia uwekezaji zaidi Tanzania inaimarisha ukusanyaji wa taarifa za kijiolojia kwa kufanya utafiti wa anga wa Kijiolojia katika vitalu sita vilivyoteuliwa, kwa lengo la kuwa na asilimia 50 ya nchi iliyofanyiwa utafiti kufikia 2030, kutoka asilimia 16 ya sasa.
Serikali pia inashirikiana kwa karibu na washirika kama Umoja wa Ulaya (EU) kupitia PanAfGeo+ na AfricaMaVal ili kujenga uwezo wa kiufundi katika Taasisi ya Jiolojia Tanzania (GST). Ushirikiano huu ni muhimu kwa kuendeleza hifadhidata ya kisasa na ya kuaminika ya kijiolojia kusaidia uwekezaji unaowajibika na maendeleo endelevu.
Mbibo amesema Tanzania tayari inafanya maendeleo katika sekta hiyo, ikiwa na miradi 12 ya madini muhimu katika hatua mbalimbali za maendeleo, ikiwemo: miradi ya grafiti, mradi wa nikeli, miradi ya mchanga mzito wa madini, mradi wa elementi adimu za ardhini, mradi wa niobium na mradi wa urani.
“EU imeelezea nia ya kuchukua jukumu kubwa zaidi katika mnyororo huu wa thamani kupitia ushirikiano, ufadhili, uhamishaji wa teknolojia, na kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi ya EU,” amesema.
Ameongeza kuwa taifa linahitaji kuhama kutoka kuuza malighafi kwenda kuchakata na kuongeza thamani hapa nchini ili kuunda ajira na kuhakikisha Watanzania wananufaika moja kwa moja na utajiri wao wa madini.
Mratibu wa Programu hiyo, Jean-Claude Guillaneau amesema wanazingatia kuimarisha ushirikiano ili kuhakikisha madini yanachakatwa na kuongezewa thamani hapa nchini. Hii ni muhimu kwa ajira, hasa katika sekta ya uchimbaji mdogo wa madini.
“PanAfGeo+, inayotekelezwa kwa pamoja na Shirika la Tafiti za Jiolojia barani Afrika (OAGS) na EuroGeoSurveys (EGS), hadi sasa imetoa mafunzo kwa zaidi ya wataalamu 1,750 wa Kiafrika kutoka nchi 54 kwenye taaluma mbalimbali za jiolojia, na hivyo kuongeza uwezo wa Afrika,” amesema.
Zaidi ya mafunzo, Guillaneau amesema kuwa mpango huo pia unavutia uwekezaji kusaidia nchi za Kiafrika kuendeleza minyororo ya thamani ya madini muhimu.
“Bara la Afrika lina utajiri mkubwa wa madini ambayo hayajachunguzwa kikamilifu, na ramani kamili ya jiolojia itakuwa muhimu katika kufungua maendeleo endelevu,” amesema.
Naye, Rais wa EuroGeoSurveys, Tirza van Daalen, amesema lengo pana la PanAfGeo+ kwamba mpango huo ni zaidi ya sayansi. Ni kuhusu kutafsiri sayansi kuwa maendeleo na kukuza mshikamano kati ya maabara.
Balozi wa EU nchini Tanzania, Christine Grau, amesisitiza kujivunia kuzindua awamu hii hapa Tanzania, tukishirikiana na washirika wa Kiafrika kuimarisha jiolojia kwa ajili ya baadaye.
Tukio hilo, lililoandaliwa na Taasisi ya Kifaransa ya Jiolojia (BRGM), limekutanisha wajumbe wengi kutoka taasisi za jiolojia, serikali, mashirika ya kimataifa, na sekta binafsi. Lilijumuisha mijadala ya kimkakati juu ya usimamizi endelevu wa rasilimali na kuonyesha mipango ya kitaifa kutoka Tanzania, Rwanda, Uganda, na Zambia.