Dodoma. Hoja ya kufufua kiwanda cha kutengeneza matairi cha General Tyre, imeibuka tena bungeni baada ya Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo, kuhoji mpango wa Serikali kuhusu kiwanda hicho.
Kiwanda hicho, ambacho kwa sasa kinamilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali, kilianza uzalishaji wa matairi ya magari miaka ya 1970, lakini kilisitisha uzalishaji mwaka 2009.
Suala la ufufuaji wake limekuwa likijitokeza mara kwa mara bungeni tangu Bunge la 11, wakati aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, alipohoji hatima ya kiwanda hicho ndani na nje ya Bunge.
Majibu ya Serikali yamekuwa yakisisitiza azma yake ya kukifufua kiwanda hicho kwa kununua mashine mpya za kutengeneza matairi.
Hata hivyo, Mei 21, 2025, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, alikabidhi kazi ya ufufuaji wa kiwanda hicho kwa Shirika la Nyumbu.
Alisema mpango huo hautabaki maneno tu, bali utafanyiwa kazi kwa vitendo, huku akikazia kwamba kiwanda hicho kikianza uzalishaji tena, kitatengeneza ajira, kukuza uchumi na kurejesha hadhi ya mkoa.
Pamoja na hoja hiyo kuibuka mara kwa mara, leo Jumatano, Juni 25, 2025, Gambo amerudia kuuliza swali akihoji mpango wa Serikali kufufua kiwanda cha General Tyre na kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries (TPI).
Akijibu swali hilo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo, amesema Serikali imepanga kufufua viwanda vyote visivyofanya kazi ili kupunguza gharama kubwa za uagizaji wa bidhaa kutoka nje, kudhibiti upotevu wa ajira na fedha za kigeni, pamoja na kuongeza mapato.
“Kwa kiwanda cha TPI, Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina inashirikiana na mwekezaji, na kwa sasa wako kwenye hatua za mwisho za ukarabati wa kiwanda na matengenezo ya mitambo. Baada ya ukarabati kukamilika, uzalishaji utaanza,” amesema.
Kuhusu kiwanda cha General Tyre, Waziri Jafo amesema Serikali kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), inatafuta mwekezaji wa kimkakati ili kiwanda hicho kianze tena kuzalisha matairi ya magari hapa nchini.
Mbunge wa Arumeru Mashariki (CCM), Dk John Pallangyo, ameongeza kwa kuuliza ni mpango gani Serikali inao wa kufufua viwanda vingi vilivyokufa katika mazingira yasiyojulikana.
Akijibu, Dk Jafo amekiri kuwa ni kweli viwanda vingi vilikufa baada ya ubinafsishaji, ambao awali ulikusudia kuwa na tija.
Amesema kwa sasa Serikali inafanya tathmini ya kina katika mikoa yote, kwa lengo la kufufua viwanda vilivyotelekezwa chini ya mpango mkubwa wa kuanzisha zaidi ya viwanda 9,000 ndani ya miaka mitano.
“Naomba niwahakikishie wananchi wa Kilimanjaro, Arusha na kote nchini kuwa Serikali imeamua kulibeba suala hili kimkakati kwa ajili ya kufufua viwanda hivyo,” amesisitiza Jafo.
Ameongeza kwamba Ofisi ya Msajili wa Hazina inatoa ushirikiano wa karibu kuhakikisha viwanda vyote vinafufuliwa, hususan vile vilivyotumika visivyo na wenye nia njema, ambao waliendelea kuvichukua kama dhamana ya kupata mikopo bila kuviendeleza.