Unguja. Mabaharia wa Tanzania wametaja changamoto nane na mapendekezo 11 yenye lengo la kuimarisha mazingira ya kazi, kulinda haki zao na kutoa fursa za ajira katika soko la kimataifa.
Akisoma risala kwa niaba ya vyama vya mabaharia nchini, Kapteni Josiah Mwakibuja, leo Julai 25, 2025, katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani yaliyofanyika kitaifa Zanzibar, amesema miongoni mwa changamoto hizo ni ukosefu wa sera ya kitaifa ya bahari, ukosefu wa viwango vya mishahara ya mabaharia wanaofanya kazi katika meli za Tanzania na kutotambulika kwa vyeti vya mabaharia katika mfumo wa ajira serikalini.
Changamoto nyingine ni ugumu wa upatikanaji wa kazi kwa mabaharia waliomaliza muda melini, mazingira duni ya kazi kwa mabaharia wanawake, ikiwemo ukosefu wa vyumba vya faragha na mazingira salama melini, ukosefu wa elimu kuhusu sheria za kazi na haki za usalama kwa mabaharia, ajira za meli kutopitia vyama vya mabaharia na changamoto katika huduma za bima ya afya (ZHIF) kwa mabaharia na familia zao.

Hata hivyo, Mwakibuja ametoa mapendekezo 11 kwa Serikali, ikiwemo kuanzishwa kwa viwango vya mishahara ya mabaharia vya kitaifa, kuwepo kwa utambuzi rasmi wa vyeti vya mabaharia serikalini, na ajira za kazi za bandari zirudi mikononi mwa mabaharia kupitia vyama vyao.
“Serikali iandae miongozo ya kazi salama na yenye staha kwa mabaharia wanawake kwa kuzingatia MLC 2006 na ILO C190; bima ya afya ya mabaharia iimarishwe ili kujumuisha familia zao na kuhakikisha huduma zinapatikana nchi nzima. Pia Serikali ianzishe National Manning Agency kwa kusimamia ajira za mabaharia nje ya nchi,” amesema Mwakibuja.
Ameongeza kuwa ajira zote za mabaharia zipitie katika vyama kwa lengo la kudhibiti unyonyaji na kuzuia mianya ya rushwa, mikataba ya ajira iwe ni sharti la kisheria kwa makampuni yote; hivyo ni muhimu Serikali iendelee kushirikiana na kampuni za kimataifa kupitia meli zilizosajiliwa kwa bendera ya Tanzania ili kutoa fursa za ajira kwa wazawa.
Akijibu baadhi ya hoja hizo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha maslahi ya mabaharia yanalindwa kwa kuridhia mkataba wa kimataifa wa kazi wa mwaka 2006, unaotazamiwa kuwa tiba ya kutatua changamoto zinazowakabili mabaharia nchini.
Hemed amesema ili kufanikisha hayo, Serikali kupitia Shirika la Uwakala wa Meli (Tasac) na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) zimeshaingiza sheria za usafiri majini za mkataba wa kimataifa wa kazi ili kupata haki zao.
Pia amesema Serikali imekamilisha mfumo wa utoaji wa vyeti vya kielektroniki kwa mabaharia kwa lengo la kuendana na matakwa ya Shirika la Bahari Duniani (IMO) na Shirika la Kazi Duniani (ILO).
“Mfumo huo utawasaidia kupunguza muda wa utoaji wa vyeti na kuondoa uwezekano wa kughushi vyeti na kuwafanya mtaambulike na kukubalika kimataifa,” amesema Abdulla.
Sambamba na hilo, Abdulla amesema Serikali imeweka sera za uwekezaji ambazo zimesababisha kuwepo kwa Chuo cha Mafunzo ya Ubaharia Zanzibar (ZDMMI), ambacho kinaendesha mafunzo ya ubaharia na kutoa ajira kwa mabaharia wa Kitanzania katika meli za nje.
Vilevile, amesema Serikali kupitia ZMA inaendelea na usajili wa meli za ndani na nje kwa kuzingatia sheria za mikataba ya kimataifa, kusimamia usalama wa usafiri baharini, kufanya ukaguzi wa vyombo vya usafiri na kuthibitisha vyeti vya mabaharia wa kigeni.
Hivyo, ametoa wito kwa mabaharia kujitambua vizuri kwa kuzingatia taaluma na misingi ya sheria zilizowekwa.
Naye Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohammed, amesema maadhimisho hayo yanapaswa kuwa ni tathmini ya kazi zao katika sekta ya bahari ili kujua walipofika.