:::::
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Katika juhudi za kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kisasa unaotegemea ubunifu, sayansi na teknolojia, serikali kwa kushirikiana na Benki ya Teknolojia ya Umoja wa Mataifa kwa Nchi Zinazoendelea (LDCs), imezindua rasmi Ripoti ya Tathmini ya Mahitaji ya Teknolojia (TNA).
Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam Juni 25, 2025, ukihusisha wadau kutoka sekta ya umma, binafsi na taasisi za kimataifa.
Ripoti hiyo inalenga kuainisha teknolojia muhimu zitakazosaidia kukuza sekta za kilimo na uchumi wa buluu, ambazo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Watanzania walio wengi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Shaban Ali Othman, alisema ripoti hiyo ni hatua muhimu kwa Zanzibar, hasa kwa wakulima wa mwani na wafugaji wa samaki.
“TNA imeweka wazi ni teknolojia gani tunahitaji, lini na kwa namna gani zitasaidia kuongeza tija kwa wananchi wetu. Teknolojia kama mifumo ya dijitali ya usimamizi wa kilimo na uvuvi zitaboresha maisha ya wengi,” alisema Waziri Othman.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini, Shigeki Komatsubara, alisema TNA si nyaraka ya kawaida bali ni dira ya maendeleo ya kiteknolojia.
“Teknolojia zikiwekwa kipaumbele, zinaweza kubadili maisha kwa kuongeza usalama wa chakula, kukuza ajira kwa vijana na wanawake, na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” alisema.
Aliwataka wadau wa maendeleo, sekta binafsi na serikali kutafsiri mapendekezo ya ripoti hiyo kuwa miradi ya vitendo, akisisitiza kuwa Tanzania inaweza kuwa mfano wa matumizi bora ya teknolojia kwa nchi zinazoendelea.
Naye Mwakilishi wa Benki ya Teknolojia ya UN, Deodat Maharaj, alisema ripoti hiyo imeainisha maeneo yenye fursa kubwa za ukuaji kama nishati mbadala, majukwaa ya dijitali kwa kilimo na teknolojia za kisasa za uvuvi.
“Tanzania ina zaidi ya kilomita 1,400 za fukwe—hii ni hazina. TNA imeonesha njia sahihi ya kuwekeza na kutumia teknolojia kama injini ya maendeleo,” alisema Maharaj.
Kwa ujumla, ripoti ya TNA imepokelewa kama hatua madhubuti kuelekea uchumi wa kisasa unaotumia maarifa na uvumbuzi. Serikali na Umoja wa Mataifa wameahidi kushirikiana katika utekelezaji wa mapendekezo hayo kupitia miradi ya pamoja, usaidizi wa kiufundi na uwezeshaji wa jamii.
PIICHA ZOTE NA JAMES SALVATOTY TORCHMEDIA