Dar es Salaam. Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, leo Alhamisi, Juni 26, 2025 inatarajiwa kutoa hukumu za mashauri mawili yaliyofunguliwa na raia wa Tanzania – wakiwemo viongozi wa vyama vya upinzani, wagombea na wapiga kura dhidi ya Serikali ya Tanzania.
Shauri la kwanza lilifunguliwa na Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu na wenzake na la pili lilifunguliwa na Kiongozi wa Ngome ya Vijana wa chama hicho, Abdul Nondo na wenzake wawili – Deusdedith Rweyemamu na Paul Kaunda.
Katika mashauri hayo wadai wanaishtaki Serikali ya Tanzania wakidai ilihusika na vitendo mbalimbali vilivyokiuka haki zao za kiraia na kisiasa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Hukumu za mashauri hayo zimepangwa kusomwa leo saa 4:00 asubuhi, huku mwenendo huo ukirushwa moja kwa moja kwa njia ya mtandao kupitia kiungo cha Mahakama hiyo.
Katika kesi ya Shaibu na wenzake waliiomba Mahakama kushughulikia ukiukwaji wa jumla wa haki za binadamu za kiraia na za kisiasa uliofanywa na Serikali wakati wa uchaguzi wa mwaka 2020.
Walitaja ukiukwaji huo wa haki hizo kuwa ni pamoja na kukamatwa kwa wagombea bila sababu, kusimamishwa kiholela kwa kampeni za wagombea wakuu wa upinzani na kufutwa kiholela kwa wagombea wengi wa ubunge na halmashauri.
Malalamiko mengine ni madai ya kuteuliwa kwa kada wa chama tawala kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kuzuia Mahakama kushughulikia migogoro ya uchaguzi wa Rais baada ya matokeo kutangazwa na Tume ya Uchaguzi.
Vilevile wanadai kulikuwepo na vurugu dhidi ya wagombea wa upinzani na wafuasi wao, zikiwemo udhalilishaji kwa wagombea wanawake; inunuzi wa kura na uchangishaji wa kura kutoka vituo visivyotangazwa kisheria, kujazwa kwa kura bandia na kuhesabu kura kwa njia isiyo ya kawaida.
Shaibu na wenzake pia wanalalamikia kufutwa kwa leseni za machapisho na kusimamishwa kwa redio na televisheni zisizoegemea upande wa chama tawala na kuzuia au kusimamisha huduma za mawasiliano, ikiwemo simu, mtandao na mitandao ya kijamii.
Shaibu na wenzake sita akiwemo aliyekuwa mgombea urais Zanzibar, 2020 kupitia ACT-Wazalendo, Maalim Seif Shariff Hamad, walifungua shauri hilo Novemba 20, 2020. Maalim Seif alifariki dunia Februari 17, 2021.
Serikali ilipatiwa nyaraka za kesi hiyo Mei 2, 2021 na ikapewa siku 30 kuwasilisha majibu ya utetezi wake. Hata hivyo, ilichelewa kuwasilisha majibu hayo ndani ya muda kwani iliwasilisha baada ya siku 90 badala ya 30.
Walalamikaji nao waliwasilisha majibu yao kujibu utetezi wa Serikali, huku wakiomba amri ya wito wa mashahidi, ambalo hata hivyo lilikataliwa.
Februari 28, 2025, Mahakama hiyo ilikubali maombi ya Kituo cha Haki za Binadamu cha Robert F. Kennedy na Taasisi ya Haki na Demokrasia Afrika kuwasilisha hoja kama marafiki wa Mahakama, kutokana na ujuzi na uzoefu wao katika kesi za uchaguzi.
Kwa upande wa Nondo na wenzake katika shauri lao hilo wanapinga vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar vinavyotoa mamlaka kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na ile ya Zanzibar ambayo hayawezi kupitiwa na mahakama yoyote.
Pia Nondo na wenzake wanakosoa uhuru wa kimuundo kutoka kwa Rais wa Tanzania.
Shauri hilo lilitokana mashauri mawili yalitounganishwa kutokana na kufanana kwa madai na hoja, yaani shauri lililofunguliwa na Nodo peke yake na lingine lililokuwa limefunguliwa na Kaunda na Rweyemamu.
Mahakama ya Afrika iliyoko Arusha, Tanzania ni chombo kikuu cha kimahakama cha Umoja wa Afrika chenye wanachama 55, ambapo 34 wametambua mamlaka ya mahakama hiyo, ikiwemo Tanzania yenyewe.
Hukumu za mashauri hayo ambayo wadai wanalalamikia mwenendo wa uchaguzi, zinakuja wakati Tanzania inatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.
Hivyo wadai na wadau wa masuala ya haki za kiraia na za kisiasa wanatarajia kuwa endapo Mahakama itakubalina na madai yao, itaelekeza ni hatua gani Serikali ya Tanzania inapaswa kuchukua na kwa muda gani, ili kutekeleza sheria za Afrika na za kimataifa.
Wanaona kuwa hukumu hizo mbili kutoka Mahakama hiyo ya Afrika zinaweza kuwa na mchango mkubwa katika kushawishi maoni ya kitaifa na kimataifa ili kuhimiza chama tawala nchini Tanzania kufanya mabadiliko muhimu kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi wa haki.
Hata hivyo, yapo mashauri kadhaa dhidi ya Serikali yaliyokwishaamuliwa na Mahakama hiyo lakini Serikali ya Tanzania mpaka sasa haijawahi kutekeleza maelekezo ya mahakama hiyo, likiwamo la kuitaka Serikali kuruhusu mgombea binafsi.