LADIES OF NEW MILLENNIUM WASHUHUDIA MAGEUZI KATIKA MAISHA YA KAYA MASKINI MKOANI MWANZA

 

Ziara ya taasisi ya Ladies of New Millennium, iliyoongozwa na Mama Tunu Pinda, imeweka wazi mafanikio ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (PSSN) unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), baada ya wajumbe wa taasisi hiyo kujionea hali halisi ya miradi inayobadili maisha ya wananchi katika Wilaya ya Ilemela.

Wakiwa katika Shule ya Sekondari Igogwe, wajumbe hao walishuhudia kwa macho yao maboresho ya miundombinu ya elimu yaliyoletwa na TASAF kupitia afua za kijamii. Hali hiyo ni kielelezo cha namna mpango huo unavyowekeza katika maendeleo ya watoto kutoka familia zenye kipato cha chini.

Aidha, katika maeneo mengine ya ziara, walikutana na wanufaika wa PSSN waliopatiwa mafunzo ya ujasiriamali na kusaidiwa mitaji midogo, hatua iliyoibua ushuhuda wa kina kuhusu mabadiliko chanya ya maisha, ongezeko la kipato, na kuimarika kwa hali ya chakula na lishe majumbani.

Kwa kutambua mchango wa matumizi ya nishati safi, Ladies of New Millennium walitoa mitungi ya gesi kwa baadhi ya walengwa kama mchango wao katika kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, ambavyo ni visababishi vya uharibifu wa mazingira na magonjwa ya njia ya hewa.

Katika hatua nyingine ya ziara yao, wajumbe hao walifika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na kufanya mazungumzo na Katibu Tawala Bw. Balandya Mayuganya, ambaye alieleza namna mpango huo unavyochangia ustawi wa kijamii na kiuchumi katika mkoa huo.

Akizungumza kwa niaba ya TASAF, Mkurugenzi wa Mifumo, Tathmini na Mawasiliano Bw. Japhet Boaz alisema:

“Zaidi ya kaya milioni moja tayari zimenufaika na mpango huu kwa njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na sekta ya elimu, afya, lishe, na fursa za ajira ya muda. Utekelezaji wake unazidi kugusa maisha ya watu moja kwa moja.”

Wajumbe wa taasisi hiyo waliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya dhati ya kuendeleza mpango huo wa kihistoria, pamoja na TASAF kwa uwajibikaji na usimamizi wake madhubuti.

Wajumbe waliokuwa sehemu ya ziara hiyo ni Mama Tunu Rehani Pinda, Asina Kawawa, Blandina Mususa, Suzana Charles Majua na Frida Rugemalira.

Ziara hiyo imekuwa ushuhuda hai wa mafanikio ya TASAF, huku ikisisitiza umuhimu wa ushiriki wa taasisi huru na sekta binafsi katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukuza maendeleo ya jamii.

Related Posts