TANTRADE YASIMAMIA VYEMA MAANDALIZI YA MAONESHO YA SABASABA 2025

 ::::

Na Mwandishi  wetu  Dar es Salaam

Mkuu wa Wilaya ya Temeke,  Sixtus Mapunda, amefanya ziara ya kukagua maandalizi ya Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba 2025), na kueleza kuridhishwa kwake na namna Taasisi ya TanTrade inavyosimamia maandalizi hayo.

Ziara hiyo iliyofanyika katika uwanja wa Maonesho wa Mwalimu Julius Nyerere, barabara ya Kilwa, imekuja wakati shughuli mbalimbali za ujenzi na maandalizi zikiwa zinaendelea kwa kasi kuelekea ufunguzi rasmi wa maonesho hayo unaotarajiwa kufanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2025.

Mapunda amewakaribisha Watanzania wote kutembelea maonesho hayo, akieleza kuwa Sabasaba ni jukwaa muhimu la kukuza biashara, ubunifu wa bidhaa za ndani, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na mataifa mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa wito kwa makampuni ya usafirishaji na wamiliki wa malori kuepuka kuegesha magari yao pembezoni mwa maeneo ya uwanja huo wa maonesho ili kuepusha usumbufu kwa washiriki na wageni watakaohudhuria.

“Ni muhimu tukazingatia usalama na mpangilio mzuri wa mazingira ya uwanja huu, hasa kipindi hiki ambacho wageni kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kufika kwa wingi,” amesema  Mapunda.

Maonesho ya Sabasaba ni tukio kubwa la kila mwaka linalowakutanisha wafanyabiashara, wawekezaji na taasisi mbalimbali kutoka duniani kote, yakilenga kukuza uchumi kupitia maonyesho ya bidhaa na huduma.

Related Posts