Dar es Salaam. Wakati washindi wa tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika kwa tanzu za riwaya, ushairi, wasifu, tamthilia na michoro wakitarajiwa kutangazwa Julai 3, 2025, imeelezwa kuwa kiwango cha ubora wa miswada inayoshindanishwa kinaongezeka kila mwaka, lengo likiwa ni kukienzi Kiswahili.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Juni 26, 2025 jijini Dar es Salaam wakati waandaaji wa tuzo hiyo wakitangaza orodha ya miswada ya mashindano ya mwaka 2024.
Tuzo hiyo inayofadhiliwa na Kampuni ya Safal Group, kupitia Alaf Tanzania na Mabati Rolling Mills Kenya, ilianzishwa na Dk Lizzy Attree na Dk Mukoma Wa Ngugi mwaka 2014 ili kutambua uandishi kwa lugha za Kiafrika.
Mwenyekiti wa majaji wa mashindano ya mwaka 2024, Dk Salma Hamad wa Chuo Kikuu Huria, Tanzania (OUT), amesema, “miswada ilikuwa mingi, hata hivyo tumeburudika vya kutosha kwa sababu tumesoma kazi zilizoandikwa na kusukwa kiubunifu na tumejifunza kwamba kuna hazina kubwa ya vipaji vya uandishi wa fasihi ya kiswahili. Vikiendelezwa fasihi ya Kiswahili haitafilisika.”
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya tuzo hiyo, Abdilatif Abdalla amesema, “ni jambo la kufurahisha mno kuona kwamba, tangu mashindano yalipoanzishwa mwaka 2015, bado tuzo hii inaendelea kuwavutia washiriki kutoka nchi mbalimbali na kwa idadi kubwa.
“Pia kiwango cha ubora wa miswada inayoshindanishwa kinaongezeka kila mwaka, hivyo kuitajirisha Fasihi ya Kiswahili.”
Majaji wengine walioshirikiana na Dk Salma kuisoma miswada na kuwateua washindi wa mashindano ya mwaka 2024 ni Profesa Richard Wafula wa Chuo Kikuu cha Kenyatta, Kenya na Dk Caesar Jjingo wa Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda huku jumla ya miswada iliyosomwa na jopo la majaji ilikuwa 210.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Alaf Limited, Hawa Bayumi ametaja majina ya waandishi na miswada iliyoingia katika orodha fupi, akisema kwa upande wa riwaya mtunzi ni Joel Hamisi akiwa na riwaya ya Nderemo za Mtaa, Mayassa Abdallah (Kitanzi cha Mauti) na Ali Othman Masoud (Chembea), wote kutoka Tanzania.
Kwa upande wa ushairi amesema walioingia ni Mohamed Hamid Haji na ushairi wa Waadhi, Bashiru Abdallah (Bure Ghali) na Mohamed Idrisa (Laana ya Uovu) wote kutoka Tanzania.
Bayumi amesema majaji pia, waliteua mkusanyo wa hadithi fupi ikiwamo Mungu Hadanganywi na Hadithi Nyingine, iliyotungwa na Edwin Omindo kutoka Kenya.
Amesema washindi watakaotokana na orodha hiyo watatangazwa katika sherehe zitakayofanyika Julai 3, 2025, jijini Dar es Salaam.
Bayuni amesema zawadi ya jumla ni Dola 15,000 za Marekani itakayotolewa kwa miswada bora zaidi ambayo haijachapishwa.
Amefafanua kuwa, mshindi wa kwanza wa riwaya atapata Dola 5,000 za Marekani, mshindi wa kwanza wa ushairi atapata Dola 5,000 za Marekani na mshindi wa pili katika utanzu wowote, atapata Dola 2,500 za Marekani.
Kwa mujibu wa meneja huyo, mbali na zawadi hizo, miswada iliyoshinda itachapishwa katika vitabu na Mkuki na Nyota Publishers, Tanzania.
Bayumi amesema miswada ya mashairi itakayoshinda itatafsiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa na Africa Poetry Book Fund.
Pia, amesema Safal Group imeendelea kudhamini tuzo hiyo kwa mara ya tisa kupitia kampuni yake ya Alaf Tanzania na Mabati Rolling Mills ya Kenya kutokana na kukua kwake mwaka hadi mwaka.