Maeneo saba kushindaniwa tuzo za utalii

Dodoma. Serikali imetaja maeneo saba ya ubora yatashindaniwa katika Tuzo za Utalii Duniani Kanda ya Afrika na Bahari ya Hindi kwa mwaka 2025 (World Travel Awards), zitakazofanyika Juni 28, 2025 jijini Dar es Salaam.

Maeneo hayo ni eneo bora kwa utalii Afrika, bodi bora ya utali, kivutio bora cha utalii Afrika,  hifadhi bora zaidi Afrika, kampuni bora za utalii, hoteli inayotoa huduma bora kwa watalii na kampuni bora ya huduma za safari.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana ameyasema hayo leo Juni 26, 2025 wakati akizungumzia kuhusu utoaji tuzo hizo.

Amesema hatua ya tuzo hizo kufanyika nchini ni uthibitisho wa hadhi kubwa ambayo Tanzania imejipatia kimataifa katika sekta ya utalii na matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa kinara wa kutangaza Utalii.

Amesema kama nchi kwa ushirikiano baina ya sekta za umma na binafsi wameingia katika kinyang’anyiro hicho katika vipengele 50 kupitia vivutio, huduma bora pamoja na ukarimu wetu kwa watalii.

“Tukio la mwaka huu linaleta pamoja wasimamizi wa sekta ya utalii na ukarimu kutoka mataifa mbalimbali, wawekezaji, waandishi wa habari wa kimataifa, na wawakilishi wa sekta za utalii, hoteli na mashirika ya ndege,”amesema.

Amesema tuzo hizo zitawaleta kwa pamoja pia kampuni za usafiri na huduma za utalii kutoka kila pembe ya Afrika na visiwa vya Bahari ya Hindi na nje ya Bara la Afrika.

Amesema Tanzania inategemewa wageni zaidi ya 250 kutoka nje ya nchi kushiriki katika tukio hili ambapo hadi sasa wamekwisha thibitisha ushiriki wao na wengine wameanza kuwasili nchini.

Kwa mujibu wa Dk Chana Tuzo za World Travel Award zilianzishwa mwaka 1993 nchini Uingereza chini ya Kampuni ya World Luxury Media Group.

Amesema tuzo hizo zimefanyika kwa miaka 32 mfulululizo zikiwa na lengo la kutambua na kutoa hadhi kwa watoa huduma za utalii.

“Sisi kama Tanzania tulianza kushiriki mwaka 2013 ambapo tulishinda Tuzo ya Kivutio Bora Barani Afrika ambacho ni Mlima Kilimanjaro na tuliendelea kushiriki hadi kufikia mwaka 2024 ambapo tulifanikiwa kushinda tuzo tano,”amesema.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamishna wa Polisi  Benedict Wakulyamba amewataka waandishi wa habari kuendelea kutoa habari za kuelimisha kuhusu sekta ya utalii nchini ili iweze kuendelea kuchangia katika kukuza uchumi wa Tanzania.

Related Posts