Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema uchumi wa Tanzania umeongezeka kutoka ukuaji wa asilimia 3.9 mwaka 2021 hadi 5.5 mwaka 2024, huku mwaka huu ukuaji ukitarajiwa kufikia asilimia sita.
Amesema ukuaji huo upo juu ya wastani wa ukuaji kwa bara la Afrika ambalo ni asilimia nne pekee mwaka 2024.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Juni 27, 2025 wakati akihutubia Bunge jijini Dodoma ikiwa ni hatua ya kulivunja Bunge hilo la 12 kuelekea uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.
“Wakati uchumi wa dunia unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 2.3 mwaka 2025, Shirika la Fedha Duniani linakadiria ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa mwaka huu 2025 utafikia asilimia sita,”amesema.
Pia, Rais Samia amesema pato ghafi la Taifa limeongezeka kutoka Sh156.4 trilioni 2021 hadi Sh 205.84 trilioni 2024.
“Ongezeko hilo ndilo analotafsiri nako kuongeza pato la Mtanzania limeongezeka kutoka Sh2.367 milioni hadi Sh2.938 milioni, pia shilingi yetu imeendelea kuimarika,” amesema.
Akizungumzia mfumuko wa bei, Rais Samia amesema umeendelea kuwa chini ya asilimia tano kwa miaka minne na kiwango hicho kipo ndani ya lengo la nchi la kuhakikisha haivuki asilimia tano.
Amesema kiwango hicho ni bora kwa Afrika Mashariki na ipo chini ya mfumuko wa bei ulioshuhuidwa kwa nchi za Afrika.
Rais Samia ameeleza kuwa mauzo ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi yameongezeka kutoka Dola za Marekani 6.39 milioni (Sh16.6 bilioni) mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Marekani 8.7 milioni (22.62 bilioni) mwaka 2024 na kutunisha akiba ya fedha za nje.
“Hadi mwezi Aprili 2025 tulikuwa na akiba ya fedha za kigeni dola 5.6 bilioni (Sh14.56 trilioni) ambazo zinatosha kuagiza huduma kwa miezi minne na nusu kama ilivyo lengo la Afrika Mashariki,” amesema.
Aidha, Rais Samia amesema kufuatia marekebisho ya sheria za madini sura 123, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilinunua na kuweka akiba ya kilo za dhahabu 3,424 zilizonuniliwa kwa Sh702.3 bilioni na ununuzi unaendelea kuimarisha akiba iliyopo.