Unguja. Kutokana na changamoto ya upatikanaji wa mawe na mchanga kisiwani hapo, Serikali ina mpango wa kusafirishia madini hayo kutoka Tanzania Bara na kuyaleta hapa kwa lengo la kupunguza changamoto hiyo.
Serikali imesema imejipanga kuhakikisha kuwa mawe na mchanga utakaotolewa Tanzania bara yanapatikana kwa gharama nafuu ili wananchi kuendeleza shughuli za ujenzi na miradi uwekezaji.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa Juni 27, 2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Nishati na Madini kutoka Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar, AbdulSatar Maulid Salim wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi za Idara Maelezo Zanzibar.
“Kutokana na kupatikana kwa wingi huduma ya mawe na mchanga Tanzania bara Serikali inajipanga kuangiza madini ya ujenzi kutoka huko na tutahakikisha tunaweka mazingira mazuri ili wananchi kuyapata kwa gharama nafuu”, amesema AbdulSatar
Pia Kaimu huyo, amesema ili Serikali kufikia lengo la kupunguza changamoto hiyo ndio maana imefungua maeneo maalumu ya kuchimba Mawe kuondokana na uharibifu wa mazingira.
“Katika kurahisisha hilo Wizara imekuja na mfumo maalumu kwa mwananchi mwenyewe kukata kibali cha kununua Mawe na Mchanga kwa bei nafuu ikilinganishwa na kuwafuata madalali wanaopakia madini hayo,” amesema AbdulSatar
Pia, amesema kinachopandisha bei hayo ni ulanguzi wa baadhi ya madereva wanaohitaji kufidia fedha kupitia usafiri unaotumika kusafirishia mawe na mchanga kutoka katika maeneo yaliyopangiwa.
Mbali na hayo, AbdulSatar ameelezea sababu mojawapo iliyosababisha kufungia maeneo ya kuchimbwa mawe ni kutokana na uvamizi uliofanywa na baadhi ya wananchi kuchimba katika maeneo ambayo hayajaruhusiwa kwani maeneo mengine yalitengwa kwa ajili ya uwekezaji na miradi ya maendeleo.
Amesema, Wizara imeingia mikataba na baadhi ya tasisi ili kuhuisha maeneo yaliyoharibiwa na kuyarudisha katika uhalisia wake wa awali.
Kwa upande wa Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Maji, Jokha Salumu Mohamed amesema wizara hiyo imefanikiwa kuchimba visima 405 jambo ambalo limesaidia wananchi kufaidika navyo kwa kupata huduma ya maji.
Amesema, bado wananchi hawana muamko wa kuvuta maji na kuweka katika nyumba zao hivyo baada ya kuona hilo serikali imelifanya kuwa programu maalumu ya kushajijihisha wananchi kuingiza maji ndani na nyumba 20,000 zimeunga maji kupitia programu hiyo.
Akizungumzia changamoto ya upatikanaji wa umeme kwa wananchi, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Joseph Kilangi amesema adha wanazokutana nazo wananchi katika kuunganishiwa huduma ya umeme hilo limeshafanyiwakazi.
Amesema kwa sasa mwananchi anapowasilisha maombi yake Shirika la umeme Zanzibar (Zeco) linaunganisha umeme ndani ya wiki moja na wala haihitaji kuwa na mwenyej ili kupata huduma kwa urahisi kwa sababu hiyo ni haki ya mwananchi.
“Kila mwananchi ana haki ya kupata huduma za umeme na maji bila ya kuwa na mtu wa karibu katika sekta hiyo kwani huo ni mkakati wa wizara kila mmoja kupatiwa huduma ya maji na umeme,” amesema
Pia, amesema sera ya wizara hiyo ni kuta huduma ya umeme bila ya kumtaka mwananchi kulipia nguzo ya umeme ili awekewe kwani wanataka kupunguza makali ya umasikini.