Hotuba ya Samia ilivyowagusa wasomi, watoa mapendekezo

Dar es Salaam. Hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 imepokewa kwa maoni mseto na wadau wakiwamo wachumi, wanasiasa na wachambuzi wa masuala ya kijamii.

Baadhi wamesema ilikuwa hotuba nzuri kwa sababu aligusia maeneo takribani yote muhimu yakiwamo ya ulinzi, usalama, kijamii, kisiasa na kiuchumi. Hata hivyo, baadhi wamesema kuna maeneo hakutoa maelezo ya kina.

Ijumaa Juni 27, 2025 Rais Samia alilihutubia Bunge jijini Dodoma kuhitimisha shughuli zake ikiwa ni fursa ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Katika hotuba yake ya saa 2:47 Rais Samia alieleza mafanikio ya Serikali anayoingoza, pia alifafanua kuhusu deni la Serikali, mchakato wa Katiba mpya, mabadiliko ya sheria za uchaguzi sambamba na kutoa maagizo kuhusu matukio ya watu kupotea.

Mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii, Kiama Mwaimu amesema ilikuwa hotuba nzuri, ingawa katika suala la kwa nini Serikali inakopa, haikufafanuliwa zaidi akisema ni miongoni mwa maeneo yaliyokuwa yanataka maelezo ya kina.

“Kwa sababu kama tunazungumzia mikopo ya nyuma iliyoombwa na kupitishwa kwenye Serikali nyingine, je awamu hii kuna fedha zozote tulizokopa? Hapa alitakiwa atufafanulie ili mwananchi wa kawaida aelewe,” amesema na kuongeza:

“Kuhusu hali ya utulivu wa kisiasa, Rais Samia aliwataka watu kukaa kwa amani na kufanya uchaguzi kwa haki… ingawa kuna mazingira yaonyesha kama vile kuna changamoto ya kutokuwa na haki ndiyo maana wengine wanalalamika.”

Akizungumzia deni la Serikali, mwanazuoni wa uchumi, Profesa Benedict Mongula amesema ni vyema amekiri kuhusu kuongezeka kwa deni la Serikali pia amefafanua vema.

Kwa sababu tayari deni linakua, amesema Taifa linapaswa kujikita kwenye mbinu za kuhakikisha linalipwa ili kuepuka athari za baadaye.

Profesa Mongula amesema namna rahisi na ya haraka ya kufanikisha malipo ya deni hilo ni kuhakikisha kila mkopo unaochukuliwa sasa unatumika kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya haraka.

“Shughuli hizo zitawezesha kupata fedha za haraka na hatimaye kukuza uchumi na kulipa deni ili lisiendelee kukua. Kasi ya kukua izidiwe na kasi ya kulipwa,” amesema.

Wakati yakifanyika hayo, amesema Serikali iendelee kuimarisha makusanyo, kudhibiti mianya ya kupotea kwa kodi na ibuni vyanzo vipya kuhakikisha nchi inajenga uchumi kwa vyanzo vyake vya ndani.

Amesema ni vigumu kuepuka kukopa kutokana na uhalisia wa uchumi wa nchi, lakini kila mkopo uelekezwe kwenye shughuli mahususi ili kujenga uchumi na maendeleo.

Jambo lingine linalopaswa kufanyika amesema ni kudhibiti ununuzi wa bidhaa za nje ambazo hukuza deni.

“Mkakati wa Serikali wa kujitegemea ni mzuri ni vema tuongeze nguvu kuhakikisha hilo linatimia kwa masilahi ya maendeleo na uchumi wetu,” amesema.

Kuhusu Katiba mpya, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatib, amesema hilo ni miongoni mwa mapendekezo ya muda mrefu yaliyotolewa na kikosi kazi kilichoundwa na Rais Samia.

Amesema kikosi kazi hicho ni matokeo ya vikao kadhaa vya Baraza la Vyama vya Siasa vilivyoibua malalamiko yaliyosababisha kiundwe.

“Ni pendekezo sahihi liliwekwa kuwa la muda mrefu na tayari limeshapangiwa ratiba, tusubiri kwa sababu hatua ya kuwekwa kwenye ratiba inaonyesha Serikali ina utashi,” amesema.

Khatib amesema vikao vya baraza hilo vimekuwa mwarobaini wa kupatikana kwa sheria mbalimbali ikiwamo ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 2024.

“Baraza lilikaa ndiyo yote haya yametokea kwa hiyo ni jambo la muhimu,” amesema.

Akizungumzia watu kupotea, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk George Kahangwa amesema  afadhali Rais Samia amelizungumzia suala hilo hadharani.

Amesema jambo likizungumzwa na kiongozi mkuu wa nchi linakuwa lenye nguvu kubwa.

“Sasa hivi Watanzania tutarajie vyombo vya ulinzi na usalama vilivyoagizwa vitafanya kazi inayotakiwa na Watanzania watapewa majibu. Tutarajie polisi wasichukue muda kuhusu kulifanyia kazi na kueleza umma kwamba waliopotea wamechukua muda gani na wamefikia wapi,” amesema.

Amesema: “Watafanya hivyo kwa faida ya nchi, kwa faida yetu sisi wote Watanzania ili tuamini kwamba kuna vyombo vya ulinzi vinatulinda, tupo salama, lakini tuna vyombo pia vinavyoweza kumsikiliza mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu.”

Related Posts