Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Bukoba, imebariki adhabu ya kifungo cha maisha jela alichohukumiwa Iman Emmanuel kwa kosa la kumbaka mtoto wa kike aliyekuwa na umri wa miaka saba.
Awali Julai 30,2024 Mahakama ya Wilaya ya Kyerwa ilimhukumu Iman adhabu hiyo baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kosa hilo bila kuacha shaka.
Mbali na ushahidi huo, ushahidi mwingine uliomtia hatiani ambao pia mahakama hiyo imeuzingatia ni pamoja na ushahidi wake mwenyewe ambaye alikiri mahakamani kuwa ni kweli alimbaka mtoto huyo hivyo anaiomba mahakama ipunguze adhabu dhidi yake.
Hukumu hiyo iliyobariki adhabu hiyo imetolewa Juni 27, 2025 na Jaji Lilian Itemba katika rufaa ya jinai namba 27044/2024.
Jaji amesema baada ya kupitia sababu zote za imezitupilia mbali kwa kukosa mashiko ikiwemo hoja kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi yake bila shaka na kuwa kosa hilo lilithibitishwa dhidi ya mrufani.
Katika kesi ya msingi mrufani alishtakiwa kwa kosa la ubakaji, kinyume na kifungu cha 130 (1), 130(2)(e), na 131(3) cha Kanuni ya Adhabu.
Ilielezwa kuwa kosa hilo lilitokea Septemba 13, 2023 katika Kijiji cha Omkagoye Wilaya ya Kyerwa Mkoa wa Kagera ambapo katika utetezi wake alidai kesi hiyo imetengenezwa dhidi yake kwani kulikuwa na mgogoro wa kifamilia kati ya kaka yake na familia ya mwathirika wa tukio hilo.
Kumbukumbu za mahakama zinaonyesha kuwa wakati wa utetezi wake, ukurasa wa 19 unaeleza namna alivyokiri kutenda kosa hilo na kuomba mahakama impunguzie adhabu.
“Imani Emmanuel, umri wa miaka 22, mfanyabiashara, mkazi wa Nkwenda, mheshimiwa hakimu, naiomba mahakama yako tukufu inipunguzie adhabu kwa sababu sina hata ndugu wa kuja kunisaidia. Sina msaada maisha yangu yote. Naomba unipunguzie kifungo. Mheshimiwa naiomba mahakama yako inisaidie kunipunguzia adhabu.”
Alipohojiwa mrufani alijibu “Kweli nilifanya kosa hilo, nilimbaka
Katika rufaa hiyo mrufani alikuwa na sababu saba ambazo ni pamoja na Hakimu alikosea kumtia hatiani kwani umri wa mwathirika haukuthibitishwa.
Nyingine ni Hakimu alijielekeza vibaya kwa kushindwa kutambua kutoamika kwa shahidi wa kwanza na tatu, hakukuwa na ofisa yeyote wa polisi mpelelezi wa kesi hiyo aliyetoa ushahidi kuthibitisha au kuonyesha matokeo ya upelelezi.
Nyingine ni Hakimu kukosea kisheria kumtia hatiani kwa kosa aliloshtakiwa kwa kuzingatia udhaifu wa utetezi wake na kosa halikuthibitishwa.
Mrufani huyo hakuwa na uwakilishi wa wakili huku mjibu rufaa akiwakilishwa na Wakili Matilda Assey.
Baada ya kuitwa kuwasilisha, mrufani ambaye amerekodiwa kuwa hajui kusoma wala kuandika, aliiomba mahakama imsomee sababu zake za rufaa.
Akiwasilisha kwa ufupi mahakamani hapo mrufani huyo alieleza kuwa umri wa mwathirika haukuthibitishwa, kutokuwepo kwa ofisa upelelezi aliyechunguza kesi hiyo kulisababisha pengo katika kesi ya mashtaka.
Alieleza kuwa mahakama hiyo ilitegemea isivyofaa udhaifu wa utetezi na kuwa kesi dhidi yake haikuthibitishwa pasipo shaka yoyote, hoja ambazo zilipingwa na wakili wa jamhuri alipinga rufaa hiyo na kuomba itupiliwe mbali kwa kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kesi bila shaka yoyote.
Jaji Itemba amesema baada ya kuchunguza kwa makini rekodi ya mahakama ya kesi, sababu za kukata rufaa, na mawasilisho ya pande zote mbili, suala la kuamuliwa ni kama rufaa hiyo ina mashiko na iwapo upande wa mashtaka ulithibitisha kosa hilo.
“Nimechunguza shauri la mahakama, na katika ukurasa wa nne, shahidi wa kwanza ambaye ni mwathirika, baada ya kumtambua mrufani, alitoa ushahidi kwenye mahakama ya awali kuhusu hatua alizotenda mrufani dhidi yake na namnukuu.
“alipoingiza uume wake, nilipiga kelele na akaniziba mdomo baadaye mama yangu akaja, na Imani akakimbia’ pia mama (shahidi wa tatu ) alishuhudia kwamba “Nilimkuta akiingiza uume wake kwenye uke wa mtoto wangu……
“Nilipiga kelele. Imani alikuwa ananiambia niache kupiga kelele tumalizie, nilipomaliza kupiga kelele, Imani akakimbia…..majirani wakamkimbiza na kumkamata kwenye maandazi…wakampeleka kwa mwenyekiti wa Mtaa”.
Jaji Itemba amesema baada ya kupata fursa ya kutazama na kutathmini mienendo ya shahidi wa kwanza na wa tatu, mahakama imeona kuwa walikuwa wa kweli.
Amesema baada ya kupitia sababu zote za imezitupilia mbali kwa kukosa mashiko ikiwemo hoja kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi yake bila shaka.
Miongoni mwa masuala hayo ni pamoja na mrufani kudai kesi hiyo haikuthibitishwa, ilitungwa, ambapo Jaji amesema madai haya bado hayajathibitishwa na hayakuungwa mkono na ushahidi wowote.
“Kwa sababu zilizotangulia, kwamba sababu zote za kukata rufaa hazina mashiko naona ni wajibu kuitupilia mbali rufaa hiyo na kuidhinisha hukumu iliyotolewa na mahakama ya awali, adhabu ya kifungo cha maisha jela ilikuwa halali,” amehitimisha Jaji.