Samia awaagiza Ma-RC kusimamia kilimo

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewaagiza Wakuu wa Mikoa nchini kuhakikisha wanakwenda kusimamia kilimo kwa kuwa ndiyo sekta nyeti na muhimu kwa Taifa.

Amesema asilimia 70 ya ajira za Watanzania ni katika sekta hiyo na asilimia 25 ya fedha za kigeni zinatokana na kilimo huku kikichangia asilimia 30 katika pato la Taifa.

Rais Samia ameyasema hayo leo Juni 28, 2025 wakati akifungua kiwanda cha mbolea cha Itracom kilichopo Dodoma akiwa sambamba na Rais wa Jamhuri ya Burundi Evariste Ndayishimiye.

Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye akizungumza katika uzinduzi wa Kiwanda cha uzalishaji wa mbolea cha Intracom kilichopo Nala Jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha



Amesema mbolea hiyo inapofika kwa wakulima, inatakiwa wawe na maelekezo ya matumizi sahihi kwani kilimo ndicho kitachangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha usalama wa chakula, kupunguza umasikini na kuongeza ajira kwa wanawake na vijana.

“Wakuu wa mikoa kama mlivyosikia kwamba kilimo ni sekta muhimu sana na Waziri wa sekta na  mipango na uwekezaji wamethibitisha hilo kwamba ndiyo kipaumbele chetu, kasimamieni kilimo kama kipaumbele nawaomba sana,” amesema.

Rais Samia amesema sekta ya kilimo ni nyeti na kwamba serikali itafanya kila liwekezekanalo kuhakikisha inamwezesha mkulima kuzalisha zaidi.

Amesema kwa kuwa mbolea inazalishwa nyumbani wakulima wanatarajia pia bei itakuwa nafuu, na Waziri kuweka ruzuku kwenye mbolea, itawafanya wakulima ambao hawakuwa wakitumia mbolea sababu ya uwezo wa kununua sasa wataipata kwa bei nafuu.

Pia amekitaka kiwanda hicho kuhakikisha kinazalisha mbolea kuendana na aina ya udongo wa maeneo husika, kama ambavo maabara yao ina uwezo wa kufanya utafiti wa udongo hivyo watumie fursa hili ili  kuwasaidia wakulima wa maeneo mbalimbali.

Rais Samia amewataka wafanyakazi wa kiwanda hicho kuhakikisha wanakitunza ili kiendelee kufanya kazi kwa muda mrefu, “Sh486 bilioni iliyowekezwa hapa hii ni fedha ningi sana anayefanya kazi katika kiwanda hiki hana budi kuhakikisha tunakilinda, tukitunze.”

Katika hatua nyingine amesema uzinduzi wa kiwanda hicho ni ishara ya mafanikio katika nchi mbili zinavyoweza kushirikiana katika miradi ya kimkakati, kwani zipo kampuni zimewekeza Tanzania na kampuni zingine Burundi ikiwemo CRDB.

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akizungumza katika uzinduzi wa Kiwanda cha uzalishaji wa mbolea cha Intracom kilichopo Nala Jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha



“Tunaendelea kuboresha huduma kwa Burundi kupitia bandari ya Dar es Salaam kuongeza zaidi biashara zetu, nchi zetu zinashirikiana. Januari 2025 tulisaini mkataba wa reli ya kisasa ya SGR kipande cha saba na cha nane kutoka Uvinza – Kigoma hadi Burundi yenye urefu wa kilomita 282, itaelekea Congo,” amesema.

Hivyo amesema kupitia uwekezaji huo, anaamini wataendelea kuwekeza katika fursa za kilimo huku akimtaka Rais wa Burundi kumkutanisha Waziri wa Kilimo Burundi kushirikiana uzoefu na Waziri Bashe wa Tanzania kuhusu utatuzi wa changamoto katika sekta ya kilimo ikiwemo masoko.

Aidha amempongeza mwekezaji huyo Adrian Mtigashika kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa, huku akieleza kuwa alikutana naye kwa mara ya kwanza akiwa makamu wa Rais na mwaka 2021 akiwa Rais, “Nilimhakikishia awekeze Tanzania na hatajuta, umewekeza kwenye sekta salama na uwekezaji wako utaleta tija na utakulipa mara nyingi kiwango kile ulichokitaka kwani uzalishaji wako unatumia malighafi zinazozalishwa nchini.”

Kwa pande wake Rais wa Jamhuri ya Burundi, Evariste Ndayishimiye amesema kupata mbolea ya bei nafuu ni jambo la msingi, hivyo uwepo wa kiwanda cha aina hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa gharama ya mbolea na kuongeza kipato kwa wakulima na kuongeza upatikanaji wa chakula.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akisogeza kitambaa pamoja na Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye kuashiria ufunguzi wa Kiwanda cha mbolea cha ITRACOM Fertilizers Limited kilichopo Nala, Jijini Dodoma, Juni,28 2025.



Amesema Burundi wanaamini kiwanda hicho kitatumika kama kielelezo cha kichocheo kwa wawekezaji wengine, huku akimpongeza mwekezaji huyo kutoka Burundi akisema anamfahamu tangu siku nyingi ni mbunifu na mthubutu hivyo ameweka daraja jingine baina ya Burundi na Tanzania.

Ndayishimiye amesema kiwanda hicho kitawezesha kuendeleza kilimo kwa nchi mbili, ushirikiano nao utaimarika kwa pande zote, akitolea mfano Burundi itaimarika na kuwataka wafanyabiashara wengine kutoka Tanzania waendelee kuwekeza nchini.

“Ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi mbili haujaanza leo, zamani warundi walikuja Tanzania kwa ajili ya kuuza bidhaa mbalimbali kama za chuma na Warundi wote wanapafahamu Uvinza walikuja kununua chumvi.

“Mkataba wa kwanza wa kibiashara baina ya nchi hizi ulikuwa mwaka 1962, mikataba mingine ilifuata katika sekta zingine, mwaka 1972 Tanzania imepokea umati wa warundi waliokimbia mauaji ya kikatili ambao sasa wamerudi kama wawekezaji.”

Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo amesema wizara hiyo itaendelea kuimarisha sekta ya viwanda.

Amesema wakati Rais Samia anaingia madakarani kulikuwa na viwanda 50,000 lakini ndani ya kipindi kifupi wameshajenga viwanda 80,188 na kuwa ni ongezeko la viwanda 18,188 na kwamba tayari viwanda 40,000 vikubwa vimekamilika na vinataka kufunguliwa.

“Tutalinda viwanda vya ndani, hatutoruhusu kuingiza bidhaa za nje zitaharibu viwanda vya ndani. Nchi ya Tanzania hatuagizi nondo kwa sasa tunazalisha tani milioni 10 na mahitaji yetu ni tani milioni saba, vivyo hivyo katika bidhaa zingine kama saruji, vioo na nyinginezo,” amesema.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema, “Katika sera yetu ya nchi kilimo kinachukua nafasi ya kwanza, leo tuko hapa tukitekeleza jambo muhimu sana, uwekezaji katika kilimo na viwanda ni sera zako, mipango na maelekezo yako yanatekelezeka.”

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema serikali imetoa Sh700 bilioni kuwapa wakulima ruzuku ya mbolea na huduma zingine nyingi za kilimo ambazo wakulima wanapata maendeleo vijijini.

Pamoja na hayo, Bashe ameelezea hatuakwa hatua za uwekezaji wa kiwanda hicho cha mbolea akisema mwekezaji wa kiwanda hicho miaka minne iliyopita alienda Wizarani na Mzee Chiligati akitaka kuwekeza.

“Mpaka kufika hapa amefanya kazi kubwa kama mwekezaji, amefanya upanuzi mkubwa na akaomba tumsaidie kuongea na benki yake ambayo ni CRDB, namshkuru Mkurugenzi wa CRDB, Abdul Nsekela alitusikia na kuchukua hatua, lakini Naibu Waziri Mkuu, Dotto Biteko naye amefanya kazi kubwa bila yeye hiki kiwanda kisingekuwepo,” amesema.

Related Posts