Haya hapa makao makuu mapya ya Chaumma

Dar es Salaam. Hatimaye Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kimepata jengo litakalotumia kama ofisi yake ya makao makuu mapya.

Uamuzi huo utakifanya chama hicho kinachoongozwa na Mwenyekiti wake, Hashim Rungwe maarufu Mzee wa Ubwabwa kuhamisha makao makuu yake kutoka yalipo sasa Makumbusho kwenda Kinondoni.

Ofisi hizo mpya, zipo katika Mtaa wa Kumbukumbu Biafra, Kinondoni, jijini Dar es Salaam. Ni jengo lenye vyumba sita vinavyodaiwa vitatumika na idara mbalimbali za chama hicho, katika kutoa huduma za kichama.


Mbali na vyumba hivyo, jengo hilo lina chumba maalumu kwa kupikia, kuegesha magari na sehemu nzuri ya kupumzika ambayo mipango yao itakuwa sehemu ya mapokezi na walinzi watakuwa wanaketi hapo.

Chama hicho kimepata jengo la ofisi hiyo yenye hadhi na yenye muonekano wa kisasa inayotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni, tangu kupata usajili wake wa kudumu yapata miaka 13 iliyopita.

Awali, chama hicho kilikuwa na Ofisi ya makao makuu maeneo ya Makumbusho Kijitonyama iliyokuwa na chumba kimoja ambayo hadi sasa anaendelea kuitumia Mwenyekiti wa chama hicho, Hashim Rungwe.


Baada ya kuwapokea mamia ya wanachama wapya, waliokihama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yaliibuka mawazo mapya ya kutafuta ofisi mpya zenye hadhi zitakazokuwa na uwezo wa idara zote za kichama kuwa na Ofisi ili kutekeleza majukumu ya kila siku.

Katika ofisi hizo shughuli za ukarabati ikiwemo kupiga rangi za chama, kufunga mifumo ya umeme, kuweka samani zenye hadhi zinaendelea ingawa chumba kimoja kimeshaanza kutumika na Katibu Mkuu wa Chaumma, Salum Mwalimu.

Mwananchi kama ilivyo kawaida jana majira ya alasiri ilifunga safari hadi zilipo ofisi hizo na kuwakuta mafundi wakiendelea na ukarabati wa jengo hilo kwa nje wakipiga rangi na kutengeneza milingoti miwili ya mbendera ya chama hicho na Tanzania.

Mwandishi alipoingia ndani ya ofisi hizo alikutana na baadhi ya viongozi wa chama hicho akiwemo, Mkuu wa Utawala, Khadija Mwago aliyekuwa ameketi sebuleni akifanya mazungumzo na mmoja wa kada wa chama hicho.

Si hivyo tu, katika chumba kingine katika jengo hilo, Katibu Mkuu, Mwalimu alikuwa anaendelea na shughuli zake huku walinzi na vijana wengine wa hamasa wakiwa wameketi nje na wengine wakiwa kwenye hekaheka za kutoka na kuingia na kusimamia shughuli za ukarabati.

Baada ya Mwananchi kufuatilia ilizungumza na mmoja wa viongozi waandamizi ambaye hakutaka jina lake liwekwe hadharani, katika maelezo yake alisema baada ya kukamilika ukarabati huo, watatoa taarifa kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa ili aweze kwenda kukagua.


“Lazima msajili aje kulikagua jengo hili ajiridhishe na kutupatia maelekezo, akibariki tutaita vyombo Vya habari kuwapa habari ili umma ujue na wanayohitaji huduma za kiofisi wake,” amesema.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, jengo hilo wanatarajia kulitumia kwa muda huku wakiendelea kutafuta jengo jingine kubwa kulingana na hadhi wanayohitaji.

“Shughuli ya kutafuta si nyepesi, hili jengo tumelipata kwakuwa tulikuwa na uharaka wa kuhitaji ofisi zaidi, Bado kazi ya kutafuta jengo lingine unaendelea,” amesema.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma, Benson Kigaila amesema matarajio yao baada ya kukamilika marekebisho madogo madogo yanayoendele watalizindua rasmi.

“Kikubwa kuweni na subra tutatangaza hivi karibuni kwa ajili ya uzinduzi wa ofisi zetu, baada ya kukamilika ukarabati mdogo unaendelea msiwe na wasiwasi,” amesema Kigaila.

Amesema matarajio yao uzinduzi unaweza kufanyika kabla ya Julai3, 2025 baada ya kukamilika kwa ukarabati huo na kuweka mifumo ya umeme na mambo mengine.

Related Posts