Mikakati ya Tanesco kukomesha hitilafu gridi ya Taifa

Dar es Salaam. Baada ya kukosekana kwa umeme kwa takriban saa mbili, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limesema tayari huduma hiyo imerejea maeneo yote nchini, huku likiendelea na tathmini kubaini chanzo kikuu cha changamoto hiyo.

Taarifa hiyo ya Tanesco, inakuja saa chache baada ya kutokea hitilafu katika gridi ya Taifa, iliyosababisha kukatika kwa umeme kuanzia saa 2:34 katika maeneo yote yanayohudumiwa na gridi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya awali ya shirika hilo, hitilafu ilitokea saa 2:34 na kusababisha umeme kukatika, lakini mafundi wanaendelea na juhudi kurejesha huduma.

Akizungumza kuhusu kurejea kwa huduma hiyo leo Jumapili Juni 29, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Lazaro Twange amesema mafundi wamesharekebisha na umeme umerudi, lakini tathmini inafanyika kubaini chanzo kikuu cha tatizo.

Ameeleza maeneo yaliyoathirika ni yale yanayohudumiwa na gridi ya Taifa na kuanzia saa 4:56 huduma ilianza kurejea na hadi saa 6:30 ikaimarika.

“Tunafanya tathmini kubaini chanzo kikuu cha tatizo ili tujielekeze kwa siku za baadaye kusitokee hitilafu itakayosababisha kukosekana kwa umeme kwa muda mrefu kama huu,” amesema Twange, huku akiwaomba radhi watumiaji wa huduma hiyo.

Amesema umeme unazalishwa, kusafirishwa na kusambazwa kwa njia yenye kilomita lukuki, kwa sasa isingekuwa rahisi kubaini tatizo kuu, zaidi ya kufanya tathmini ya kina ili kuepuka lisijirudie baadaye.

“Hatujisikii vizuri na tunafahamu huduma ya umeme ni muhimu kwa usafiri hasa wenzetu wa SGR, kwa wafanyabiashara, makanisani na watu wote kwa ujumla wanategemea umeme,” amesema.

Amesema kwa kawaida umeme unazalishwa, kusafirisha na kusambazwa kupitia vifaa na muda wowote vinaweza kupata hitilafu, hicho ndicho kilichotokea.

“Kila linapotokea jambo ni funzo na tunafanya tathmini ya kujielekeza kuhakikisha tunakomesha matatizo kama hayo, lakini kwa hatua ya sasa tulibaini kulikuwa na hitilafu ya kiufundi katika gridi,” amesisitiza.

Kuhusu kukosekana kwa huduma hiyo na athari kwa treni ya umeme ya SGR, Twange amesema anatambua Shirika la Reli Tanzania (TRC) ni mmoja kati ya wateja wakubwa wa Tanesco ndiyo maana juhudi zimefanyika kurejesha huduma haraka ili abiria wasiathirike.

Kukatika kwa umeme kulisababisha kusimama kwa treni za abiria asubuhi ya leo ikiwamo treni iliyotoa saa 11 alfajiri Dodoma, ilikwama kituo cha Pugu na abiria kulazimika kutafuta usafiri mwingine kuanzia hapo.

Related Posts