Dar es Salaam. Mradi wa Ubunifu wa Funguo, ambao ni unafadhiliwa kwa pamoja na Umoja wa Ulaya (EU), Jamhuri ya Finland na Serikali ya Uingereza (FCDO) na kutekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP Tanzania), umetangaza rasmi ufadhili wenye lengo la kuibua uwezo wa wajasiriamali wa Tanzania na kuchochea ukuaji endelevu katika sekta mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Idara ya Uchumi na Utawala wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Karina Dzialowska amesisitiza dhamira ya EU katika kukuza ukuaji jumuishi na ubunifu akisema:
“Kilichoanza kama mradi wa majaribio miaka minne iliyopita, sasa umekuwa mhimili mkuu wa mfumo wa Tanzania: Funguo limekuwa jukwaa muhimu la kukuza biashara changa kwa msaada wa kiufundi na ufadhili unaowasaidia kukua na kufikia fursa pana za kifedha.”
Amesisitiza zaidi: “Ninatoa wito hususan kwa vijana wanawake wenye ndoto na uthubutu. Tunakusudia angalau asilimia 40 ya ruzuku hizi ziende kwa wanawake, lakini hili litatimia tu kama mtawasilisha maombi yenu.”
William Nambiza, Mratibu wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Ubalozi wa Finland nchini Tanzania, amesema: “Kupitia GreenCatalyst na ushirikiano wake kupitia Mradi wa Kusimamia Uhifadhi wa Misitu, Matumizi Bora ya Ardhi na Kuongeza Thamani ya Mazao ya Misitu (FORLAND), tumejikita katika kuzalisha ajira rafiki kwa utunzaji wa mazingira, kulinda rasilimali, na kukuza ubunifu wa ndani kwenye mnyororo wa thamani wa misitu.”
Amesisitiza uungaji mkono wa Finland kwa biashara ndogo, ndogo sana na za kati (MSMEs). “Tunataka kuchochea ukuaji wa biashara bunifu katika mnyororo wa thamani wa misitu, na tunatoa wito kwa wajasiriamali wengi zaidi kuwasilisha maombi na kuchangamkia fursa hii kupitia mpango wa GreenCatalyst.”
Akisisitiza zaidi lengo la ufadhili huo, Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, John Rutere amesema, “hii ni safari ya kujenga kizazi cha biashara zinazotatua changamoto halisi na kuleta mabadiliko endelevu.”
“Kipaumbele kinatolewa kwa biashara zilizopo au zinazohusiana na mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma, na Lindi, mradi unawapa kipaumbele vijana, wanawake na watu wenye ulemavu,” amesema.
Amesema biashara zitakazochaguliwa zitapata ufadhili wa kuanzia Sh10 milioni mpaka Sh100 milioni, pamoja na usaidizi wa kiufundi, kukuza biashara, upatikanaji wa masoko, zana za kidijitali, na mafunzo ya ubunifu unaozingatia mabadiliko ya tabianchi.