Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema iko katika mchakato wa ununuzi wa ndege nyingine nane licha ya kuwepo kwa zuio la ndege za Air Tanzania kuingia katika anga la Ulaya.
Kufuatia kuwapo kwa zuio hilo, Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amewataka Watanzania kutotishwa na zuio hilo kwani jitihada zinafanyika na mambo yote yatakaa sawa.
Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Juni 29, 2025 wakati akizungumza na wanahabari katika viwanja vya maonyesho ya biashara ya kimataifa Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba.
Msigwa alikuwa akielezea mambo mbalimbali yanayoendelea nchi ikiwemo ziara zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan mikoa ya Simiyu na Mwanza sambamba na mwenendo wa maonyesho hayo.
Msigwa amesema ili ndege iweze kutumia anga na kufikia soko la nchi husika yapo masharti ambayo yanapaswa kutekelezwa ili ukidhi vigezo.
Kauli yake inakuja ikiwa ni siku chache tangu kusambaa kwa taarifa hiyo katika mitandao ya kijamii huku ikiibua mijadala mitandaoni na watu wakihoji kwa nini ndege hizo zimezuiwa.
“Watanzania hawapaswi kuwa na hofu juu ya uwepo wa zuio hilo, tutarekebisha yale yote waliyoagizwa ili kuhudumu katika soko hilo kwani hata soko la China tulilifanyia kazi kwa karibu miaka mitatu,” amesema.
Msigwa amesema masharti huwa yanakuwa tofauti na wakati mwingine yanaweza kuangalia idadi ya vyombo ambavyo nchi inamiliki na ubora wake.
“Unajua ATCL inaweza kuwa na ndege nyingi mpya kwani ina umri mkubwa ilinunuliwa mwaka 2018 lakini kuna nchi nyingine ndege ina miaka 30 inafanya kazi, shirika letu lina ndege salama na mpya na tunaenda kununua nyingine nane,” amesema.
Amesema zuio hilo linapowekwa pia wanaweza kuangalia masuala ya uendeshaji, wahudumu wawe wa kiwango fulani, pia kuangalia sehemu ambapo inatoka.
“Kila anga unalokwenda unapata masharti, hivyo kama nchi tumeendelea kuyafanyia kazi moja kabla ya lingine, hao watu wanaosimamia hivyo viwango tuko nao hapa Tanzania tangu Septemba mwaka jana na tunaendelea kutimiza suala moja baada ya lingine, na hivi karibuni tutayamaliza na tutaanza kwenda nchi mbalimbali ikiwemo London tupeleke ndege zetu ikiwemo za mizigo,” amesema.
Kwa mara ya kwanza taarifa ya katazo la ndege za Tanzania kuingia anga la Ulaya lilionekana Desemba 2024 ambapo lilieleza miongoni mwa vigezo vya kuzifungia ndege za Air Tanzania ni kutokidhi vigezo vya usalama wa anga vya kimataifa.
“Umoja wa Ulaya leo umerekebisha orodha yake ya mashirika ya ndege yanayozuiwa kuingia, au kuwekewa vikwazo vya kiutendaji katika kuingia Umoja wa Ulaya. Kutokana na taarifa hii, Air Tanzania imeongezwa kwenye orodha hiyo,” ilieleza taarifa hiyo huku Serikali ikisema inafanyia kazi suala hilo.
Hata hivyo, Air Tanzania inatambulika na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) tangu ilipoanzishwa mwaka 1977, ambapo miongoni mwa vigezo vya kuwa mwanachama wake ni kufuata viwango vya kimataifa vya usalama wa anga na utendaji.
Ndege nyingine zilizoingizwa katika katazo hilo ni pamoja na: Air Zimbabwe (Zimbabwe) Avior Airlines (Venezuela), Blue Wing Airlines (Suriname), Iran Aseman Airlines (Iran), Fly Baghdad (Iraq) and Iraqi Airways (Iraq).
Akizungumzia orodha hiyo, Kamishna wa Usafiri na Utalii wa Umoja wa Ulaya, Apostolos Tzitzikosta, amesema lengo ni kuhakikisha mashirika hayo ikiwemo Air Tanzania yanaongeza sifa na vigezo.
“Uamuzi wa kuijumuisha Air Tanzania katika orodha ni kwa sababu ya dhamira yetu thabiti ya kuhakikisha kuna viwango vya juu zaidi vya usalama kwa abiria barani Ulaya na duniani,” amesema.
“Tunahimiza Air Tanzania kuchukua hatua za haraka na thabiti kushughulikia masuala haya ya usalama wa anga. Kamisheni yetu itakuwa tayari kutoa msaada kwa mamlaka za Tanzania katika kuboresha usalama wa ndege za Air Tanzania na kuwezesha kufikia vigezo vyote vya usalama wa ndege kimataifa,” alisema.
Mpaka sasa, Air Tanzania inafanya safari zake katika mikoa nchini na nje ya nchi ikiwemo Uganda, Zimbabwe, Zambia, Afrika kusini, Mumbai na China.
Mbali na kusafirisha abiria pia ndege hizo hubeba mizigo kutoka Falme za Kiarabu (UAE) na China.
Akizungumzia maonyesho ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Msigwa amesema yanatoa fursa kwa bidhaa za ndani na nje kuonekana.
Maonyesho haya yana jumla ya washiriki 3,887 wa ndani na nje huku kampuni 386 za kimataifa zikishiriki.
Katika mwaka 2025, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imekuja na Tamasha la Sabasaba ambalo litabeba burudani aina zote kipindi chote cha maonyesho.
“Kutakuwa na burudani za muziki kuanzia mchana hadi saa sita usiku, nyimbo aina zote kupigwa, singeli, bendi, wasanii mbalimbali pia watakuwepo hapa wakionyesha bidhaa na kazi zao,” amesema.
Mbali na burudani pia amewaita mashabiki wa mpira hususan wa Yanga kwenda kupiga picha na kombe lao jipya la Ligi kuu Tanzania Bara (NBC) walilotwaa Juni 25, 2025 baada ya kuwafunga watani zao Simba 2-0.
“Pia tutaomba na baadhi ya wachezaji waje muwaone mpate na nafasi ya kupiga nao picha,” amesema.
Tofauti na miaka ya zamani ambapo watu walikuwa wakilazimika kuulizia baadhi ya mabanda ili waweze kufika, sasa wataweza kujua mabanda yalipo kupitia simu za mkononi.
“Kupitia tovuti ya Tantrade, mtu atakuwa na uwezo wa kuingia kuangalia banda analotaka kwenda lipo wapi, akibonyeza atapewa maelekezo na hata ramani anayoweza kuifuata hadi kufika anapokwenda,” amesema.
Hilo linakwenda sambamba na uwepo wa huduma ya usafiri ndani ya uwanja huo unawezesha watu kufikia banda moja kwenda lingine kwa haraka.
Leo ikiwa ni siku ya pili ya maonyesho haya tangu yalipoanza rasmi Juni 28,2025 baadhi ya waonyeshaji bado wanaandaa mabanda yao.
Wengine wako katika hatua za upambaji na wengine ujenzi jambo ambalo linafanya watu wengi kuhisi maonyesho hayajaanza rasmi.
“Mabanda mengi bado hayajaanza huduma, ukifika utaambiwa njoo Julai mosi au kesho (Juni 30) sasa mtu leo ndiyo umepata nafasi umekuja halafu hali iko hivi,” amesema Hawa Khamis, mkazi wa Mbande Msewe.
Maneno yake yaliungwa mkono na Khamis Mwinyi ambaye amesema ni vyema usimamizi sahihi ukawekwa ili tarehe ambayo maonyesho yanaanza watu wote wawe wamemaliza maandalizi.