Hii hapa mikakati ya mwenyekiti mpya wa Tamwa

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Dk Kaanaeli Kaale ameahidi kuwa katika kipindi chake cha uongozi wa miaka mitatu miongoni mwa mambo yatakayopewa kipaumbele   jitihada za kuwainua wanawake kiuchumi.

Amesema kazi kubwa imeendelea kufanyika katika ukombozi wa wanawake na kuwafanya wawe na sauti, lakini hiyo haitakuwa na maana kama wataendelea kubaki nyuma kiuchumi.

Dk Kanaeli ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), amechaguliwa kuongoza bodi ya chama hicho kwa miaka mitatu kufuatia uchaguzi mkuu wa uliofanyika jana Jumamosi Juni 28, 2025, akipokea hatamu ya uongozi kutoa kwa mtangulizi wake, Joyce Shebe aliyehudumu katika nafasi hiyo kwa awamu mbili mfululizo.

Akizungumza na Mwananchi leo Juni 29,2025 amesema pamoja na mikakati mingine, suala la kujikwamua kiuchumi linapaswa kupewa kipaumbele kwa wanawake wa ndani na nje ya tasnia ya habari.


“Mengi yamefanyika hatuwezi kubeza lakini shida kubwa ni wanawake kujinyanyua kiuchumi, hata ukiwa na sauti lakini hali yako ya kiuchumi haipo sawa ni kazi bure. Hili tunaenda kuanza nalo wanawake, ni lazima  wapate elimu ya ujasiriamali.

“Tutaenda kuzitumia vyema rasilimali zilizowekezwa na dada zetu waliotangulia kwenye chama, huwezi kuwaambia wanawake wajinyanyue kiuchumi wakati sisi wenyewe wanawake wanahabari hatuna maendeleo,” amesema Dk Kanaeli.

Suala lingine ambalo amejipanga kulifanyia kazi ni kuendelea kusema na kukemea unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto hasa kwenye mitandao ya kijamii.

“Wanawake na watoto wanadhalilishwa kupitia mitandao lazima tukemee. Mitandao inaibua matukio ya unyanyasaji na udhalilishaji. Tutaanzisha kanzidata ya kukusanya matukio ya udhalilishaji na unyanyasaji yanayofanyika mitandaoni,” amesema.

Akitoa ujumbe wake kuelekea uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu, amewataka wanawake kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi bila kuhofia udhalilishaji, huku akiahidi kuwa chama hicho kitafuatilia matukio yote ya udhalilishaji dhidi ya wanawake na kuyaripoti kwenye mamlaka husika.

“Wanawake wasiogope kashfa wala kebehi dhidi yao wakashindwa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi, Tamwa tutakuwa nao bega kwa bega tutafuatilia unyanyasaji wowote watakaokutana nao na wahusika tutawaripoti

Pia, amewataka wanahabari na wanachama wote kuendelee kuandika habari za uchaguzi kwa haki na amani.

Amesema wanahabari wanapaswa kukemea udhalilishaji wowote wa wanawake wanasiasa kwa kutumia mitandao ya kijamii.

“Tujitahidi wanawake washike nafasi za juu za uongozi na maamuzi, angalau tufikie ile asilimia 50 ambayo ndilo lengo la Tamwa,” amesema

Ujumbe wa mwenyekiti mstaafu

Akiwaaga wanachama wa Tamwa,  Shebe amesema  katika uongozi wake chama hicho kwa  kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kimefanikiwa kuzindua tuzo za Samia Kalamu, zinazolenga  kuimarisha umahiri wa taaluma ya habari pamoja na kuhimiza maendeleo na uzalendo.

Tumeweza kuisogeza Tamwa karibu na wadau, kuhamasisha masuala mbalimbali yakiwamo ya usawa wa kijinsia. Naomba tuendeleze mshikamano huu kwa masilahi ya chama na Taifa,” amesema

Shebe pia amewahimiza wanawake kushiriki kwenye uchaguzi kikamilifu, si kwa kupiga kura tu, bali kwa kugombea nafasi mbalimbali za siasa na amevitaka vyama vya siasa kusimamia na kutekeleza sera za jinsia ndani ya vyama vyao.

Akitoa rai kwa waandishi wa habari wanawake nchini, Shebe amesema wana dhamana kubwa ya kutumia kalamu na vipaza sauti vyao kwa masilahi mapana ya nchi.

“Tuna wajibu wa kuwaelimisha Watanzania kuhusu umuhimu wa kushiriki uchaguzi kwa amani na kufanya uamuzi sahihi kwa mustakabali wa nchi yetu na zaidi ya hapo, tuwaelekeze wanawake wenzetu kuwa sisi si watazamaji tu bali washiriki kikamilifu mchakato wa kidemokrasia,” amesema Shebe.

Amewaomba waendelee kuwahimiza wanawake kugombea nafasi za uongozi, na kwa wale wasiojitosa kugombea, wawatie moyo kushiriki kwa kupiga kura, kwa kuchagua kwa fikra pana na kwa masilahi ya jinsia zote.

Lakini pia amesema huu ni wakati muafaka kwa vyombo vya habari vyote nchini, kuvikumbusha vyama vya siasa kutazama usawa wa kijinsia kwa jicho la haki na utekelezaji.

“Sio tu kwenye sera, bali pia kwenye uteuzi wa wagombea, katika kampeni zao na katika maamuzi ya vyama. Usawa wa kijinsia si upendeleo ni haki,” amesema mwenyekiti huyo mstaafu wa Tamwa.

Related Posts