Dar es Salaam. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimepuliza kipyenga kwa wananchi wote wenye nia ya kugombea nafasi ya ubunge na udiwani kuchukua fomu kuanzia kesho, Jumanne, Julai mosi, 2025, huku kikieleza kuwa nafasi ya urais imewekwa kiporo.
Pamoja na kutangaza fursa hiyo, Chaumma kimeweka masharti kwa kila anayetaka kugombea ubunge au udiwani wa viti maalumu kuwa sharti aanze kuonyesha nia ya kugombea kata au jimbo kwa nafasi tarajiwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Chama hicho kinaungana na vyama vingine vikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo, ambavyo tayari vimeshatangaza ratiba ya uchukuaji na urejeshaji fomu za ubunge, udiwani na uwakilishi.
Utaratibu huo wa Chaumma kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 2025 umetangazwa leo, Juni 30, 2025, jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu, Salum Mwalimu, alipozungumza na waandishi wa habari makao makuu mapya ya chama hicho, Kiondoni-Biafra.
“Tunawaomba wanachama wetu na wale ambao si wanachama lakini wana dhamira ya kugombea ubunge na udiwani kupitia Chaumma, ni wakati sahihi kujiandaa kuchukua fomu, kuzijaza na kuzirejesha kwa utaratibu ambao chama kimeweka.
“Nimekuwa nikipokea simu nyingi na viongozi wenzangu nao walikuwa wakipokea simu, lini tutafungua milango. Ni dhahiri Chaumma imeonekana ndiyo kimbilio kwa sasa, sauti mbadala wa makundi yote kwenye jamii,” amesema Mwalimu.
Mwalimu amesema fomu za kugombea nafasi ya uwakilishi kwa ubunge Bara na Zanzibar zitatolewa kupitia ofisi za chama hicho kote nchini.
Amesema fomu ya ubunge itatolewa kwa Sh50,000 na udiwani kwa Sh10,000, wale wanaohitaji viti maalumu vya ubunge na udiwani, sharti wachukue fomu mbili ya kugombea kata au jimbo pamoja na fomu ya viti maalumu.
Utaratibu huo unaendelea kwa nafasi hizo, lakini kuhusu fomu ya kugombea nafasi ya urais, Mwalimu amesema hiyo ni nafasi nyeti na wameiweka kiporo kwani wanaendelea kufanya tathmini ya kina nani atafaa kupeperusha bendera ya chama hicho.
Kiongozi huyo amesema wamejipanga kusimamia maslahi ya Taifa la Tanzania na kujenga diplomasia inayoijengea taifa heshima na uhuru wa wananchi kujumuika.
“Tumejipanga ngazi ya Taifa kwenda kuunda na kuongoza Serikali katika namna ambayo nchi yetu itakuwa muhimu kimataifa. Wale waliokuwa wanatuuliza fomu, sasa wajitokeze kuchukua fomu na wale wanaojitokeza wahakikishe wanalinda misingi ya chama chetu.
“Hatutegemei vurugu, migogoro na mambo yasiyo na tija kwa chama chetu ikiwemo rushwa. Hatutoogopa wakati wowote kumtangaza na kumkataa anayehusishwa na rushwa ndani ya chama chetu. Wote wanaokusudia kuja Chaumma wahakikishe wanakuwa wasafi,” amesema.
Mwalimu amesema Chaumma hakiendi kushiriki uchaguzi mkuu kiuwepesi, bali kwa kishindo kikubwa kutokana na dhamira, uwezo na sababu walizonazo, na watahakikisha wanatumia vipaji vyao vyote kuwapigania na kuwatetea Watanzania.
Chaumma ni miongoni mwa vyama 18 ambavyo Aprili 2025 vilishiriki katika kikao cha kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, na kwa kusaini kanuni hizo vimepata sifa stahili ya kushiriki uchaguzi mkuu.
Naye Tumaini Munale, ambaye ni mchambuzi wa masuala ya siasa, amesema kama Chaumma kitapata mgombea mwenye ushawishi upande wa urais, kinaweza kupata kura nyingi za ubunge.
Amesema kwa siasa za Tanzania, mgombea wa nafasi ya urais anaweza kuamua idadi ya kura za ubunge na udiwani, akisisitiza imani kwa chama hicho kufanya vizuri uchaguzi mkuu ipo.
“Tumeona namna ambavyo wamefanya mkutano wao mkuu na walivyozindua kampeni, ni dhahiri wamejipanga. Wakiendelea kujipanga watafanya vizuri uchaguzi mkuu,” amesema.
Akichangia hoja hiyo, Mwalimu Samson Sombi wa mkoani Morogoro amesema Chaumma haikuwa na nguvu kubwa, lakini mwaka huu baada ya baadhi ya wanachama wa Chadema kuhamia chama hicho, kimepata nguvu, hivyo uchaguzi mkuu utakuwa na mvuto.
Amesema miongoni mwa maswali ambayo wananchi wanajiuliza ndani ya chama hicho ni kwanini Chaumma imewaamini wageni na kuwapatia nafasi za juu za uongozi ndani ya muda mfupi.
“Baada ya 2025, Chaumma kinaweza kuwa na wanachama wengi zaidi kwa namna ambavyo kitatangaza sera zake. Kama kila mtu anaruhusiwa kuchukua fomu, ni jambo la msingi,” amesema Sombi.