Moshi. Jaffary Michael ambaye ni baba wa bibi harusi aliyepoteza ndugu, jamaa na marafiki 30 katika ajali ya mabasi mawili yaliyogongana na kulipuka moto wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro, amesimulia jinsi alivyopokea taarifa ya ajali hiyo akiwa ukumbini wakati sherehe ya binti yake ikiendelea.
Michael aliyewahi kuwa mbunge wa Moshi mjini mwaka 2015-2020, ametoa simulizi hiyo leo Jumatatu Juni 30, 2025 mjini Moshi wakati idadi ya waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea Juni 28,2025 ikifikia 39 baada ya majeruhi mwingine kufariki dunia leo.
Katika simulizi hiyo, Michael amesema alipata taarifa ya kutokea kwa ajali hiyo saa 5 usiku wakiwa katika ukumbi wa Kuringe, lakini alijikaza kukabili tukio hilo la kuogofya, huku akimtoa ndugu mmoja mmoja ukumbini ili wafuatilie ukweli wa ajali hiyo.
Wakati Michael akisimulia hayo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema mpaka sasa miili mitano imetambuliwa, huku mingine 33 ikichukuliwa vipimo vya vinasaba (DNA) ili ndugu watambulike na wakabidhiwe kwa ajili ya utaratibu wa maziko.
“Katika ajali hiyo iliyotokea Juni 28 watu 38 walipoteza maisha, tulikuwa na majeruhi sita baada ya 22 kuruhusiwa jana, lakini kwa bahati mbaya majeruhi mmoja aliyelazwa KCMC leo asubuhi amefariki dunia, hivyo waliofariki dunia wamefikia 39,” amesema Babu.
Amesema miili iliyotambuliwa mpaka sasa ni mitano ambayo haikuungua sana na mingine 33 iliyoungua zaidi imeshachukuliwa vipimo vya DNA.
kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa Juni 29, chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa tairi ya basi la Kampuni ya Chanel One lililopoteza mwelekeo na kwenda kugongana uso kwa uso na basi dogo hilo aina ya Toyota Coaster iliyokuwa imebeba watu hao waliokuwa wanakwenda kwenye sherehe hiyo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Juni 30, 2025, baba wa bibi harusi amesema Juni 28, walifikwa na msiba mzito kwa kuwapoteza ndugu zake, jamaa na marafiki waliokuwa wanakwenda kwenye harusi ya mtoto wake.

“Tumefikwa na msiba mzito wa ndugu zetu na majirani na marafiki wa shemeji yetu ambao walikuwa wanakuja kwa ajili ya sherehe ya binti yangu tuliyoifanya Juni 28. Ndugu zangu hawa walikuwa wamekodi gari la pamoja kwa ajili ya kumsindikiza shemeji yangu ambaye anakaa pale Same nyumbani kwetu,”amesimulia Michael.
Amesema; “Kwa bahati mbaya walipotoka nyumbani wakiwa wametembea umbali kidogo kama wa nusu kilomita, wakakutana na ajali hiyo ambayo imeleta maafa makubwa.”
Amesema watu waliokuwa wamealikwa kutokea kijijini kwao ni zaidi ya 30 na wote wamepoteza maisha na wengine miili yao ikiwa imeungua, haitambuliki.
Akiendelea kusimulia, baba huyo amesema wakati watu wakiwa ukumbini naye akielekea huko pia, alipigiwa simu na kupatiwa taarifa hiyo.
“Tayari watu wako ukumbini na mimi nikiwa naelekea, ndio nikapewa taarifa kwamba ajali imetokea na watu wapo mahututi, sikuwambia pale ukumbini, nikaendelea na shughuli huku nikifuatilia taarifa rasmi kuhusu kilichotokea,” amesema Michael.

Hata hivyo, amesema ilipofika saa tano usiku, akapokea taarifa kwamba abiria wote waliokuwa ndani ya gari hiyo miili yao imeungua kiasi cha kutotambulika.
“Nilipopata hiyo taarifa ndugu zangu wengine waliokuwa wanakuja kwenye ile shughuli niliwarudisha nyumbani wakafuatilie tukio hilo na wengine waliokuwa ukumbini, niliwaondoa wafuatilie KCMC maana tuliambiwa kuna majeruhi wamepelekwa huko,” amesimulia baba huyo.
Amesema kwa kuwa alikuwa ukumbini, ilibidi asimame imara kuhakikisha sherehe ile inafanikiwa na inamalizika bila mtanziko.
“Kwa hiyo sehemu kubwa ya ndugu walirudi kukabiliana na hilo tukio, lakini mimi kwa sababu nilikuwa ukumbini, ilibidi niendelee mpaka nimalize ile shughuli, baada ya kuisha usiku ule ule nilikwenda Same kwa ajili ya kujua mambo yanaendaje,” amesimulia Michael.
Amesema baada ya kumalizika kwa sherehe, akatoa taarifa kwa ndugu na jamaa wote kuhusiana na ajali hiyo usiku huohuo.
Amesema harusi ya mtoto wake huyo ilifungwa jana mkoani Morogoro, nyumbani kwa kijana, lakini yeye hakushiriki.
“Nimewaambia waendelee sisi huku tukiendelea na mambo mengine ya mazishi, ila wao waje kuhani baadaye,” amasema Michael.
Akizungumzoa ajali hiyo, Hassan Awadhi, mmoja wa ndugu wa aliyefariki katika hiyo ajali amesema kifo cha ndugu yao ni pigo kwa familia na kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye anayejua maisha ya mwanadamu.
“Hiyo ajali ni Mungu amepanga watu hawa wafe kwa siku moja ndivyo ninaweza kusema, kila mtu anapozaliwa kwenye tumbo la mama yake huandikiwa atakufa siku gani, kwa hiyo tunashukuru Mungu kwa kila jambo,” amesema Awadhi.
Serikali kushughulikia mazishi
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema Serikali itasimamia mazishi ya wote walifariki dunia.
“Wananchi wetu wote hawa watasitiriwa kwa heshima zote, leo kamati ya maafa ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu ofisi ya Waziri Mkuu, inakuja ili tukae na kufanya tathmini ya mwisho,” amasema Babu.

Amesema Julai 2, 2025 (Jumatano), Serikali itatoa majibu ya vipimo vya DNA na Alhamisi ndugu watakabidhiwa miili kwa ajili ya kwenda kuzika.
“Wito wangu kwa madereva watii sheria bila shuruti na vibao vimeonyesha mwendokasi unaua na kupoteza maisha ya wananchi wetu wengi, kwa hiyo wazingatie sheria kanuni na taratibu za barabarani na hasa yale mabasi ya abiria,” amasema Babu.