Dar es Salaam. Profesa Mohamed Janabi, ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika amekabidhiwa ofisi na kuanza rasmi kazi.
Janabi amepokewa ofisini kwake leo Jumatatu, Juni 30, 2025 kwenye ofisi za Kanda ya Afrika zilizopo nchini Congo, Brazzaville, baada ya kula kiapo Mei 28, 2025 mwaka huu.
Katika nafasi yake hiyo mpya, ataiongoza WHO katika juhudi za kuendeleza kampeni ya Afya Kwa Wote katika nchi 47 za Kanda ya Afrika.
Kwa mujibu wa mtandao wa WHO Afrika, Profesa Janabi ameanza rasmi majukumu yake leo, akiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 30 wa uongozi bora katika tiba ya kliniki, sera za afya, afya ya umma, na uendelezaji wa mifumo ya afya barani Afrika na zaidi.
Profesa Janabi ni daktari bingwa wa moyo, mtaalamu wa mikakati ya afya na mwanadiplomasia wa afya ya kimataifa aliyejitolea maisha yake kuimarisha mifumo ya afya, kukuza huduma zenye usawa, na kusukuma mbele ubunifu na ushirikiano ili kuboresha afya barani Afrika.
Dira yake ni kuona Afrika yenye afya njema, ustahimilivu na ustawi, ambako kila mtu anapata huduma bora za afya kupitia mifumo ya usawa, bunifu na endelevu.
Vipaumbele vyake ni pamoja na kuendeleza upatikanaji wa huduma bora kwa wote, kupunguza vifo vya mama na watoto, kupambana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza, kukuza mifumo ya afya inayokabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha usalama wa afya na maandalizi ya dharura.
Kabla ya kuteuliwa, Profesa Janabi alihudumu kama Mshauri Mkuu wa Afya kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ambayo ni taasisi kubwa zaidi ya rufaa nchini.
Awali aliongoza Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, ambayo aliianzisha na kuibadilisha kuwa kituo bora cha huduma za moyo katika ukanda wa Afrika.
Nafasi ya Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika iliachwa wazi na Dk Faustine Ndugulile, ambaye alifariki dunia Novemba 27, 2024, baada ya kushinda uchaguzi wa nafasi hiyo uliofanyika Agosti 26, 2024, Congo Brazzaville.