Mtwara. Polisi Mkoa wa Mtwara linamshikilia Victor Thomas (39) mkulima na mkazi wa Kitongoji cha Kadudu Kijiji cha Lupaso, wilayani Masasi kwa tuhuma za mauaji ya Thomas Nkasimongwa (58), Mchungaji wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG).
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Issa Suleiman iliyotolewa leo Jumatatu, Juni 30, 2025 imeeleza tukio hilo limetokea Juni 27, 2025 saa 12 jioni katika Kijiji cha Lupaso mtaa wa Misheni.
Suleiman amesema tukio hilo lilitokea baada ya mtuhumiwa akiwa na baadhi ya ndugu zake walikwenda kanisani kwa ajili ya kupata huduma ya kiroho (kuombewa), kutokana na changamoto ambayo inasadikika kuwa anayo mtuhumiwa huyo.
Kamanda huyo amesema baada ya kufanyiwa maombi kanisani kwa muda mrefu, mtuhumiwa alionesha kuchoka, ndugu wa mtuhumiwa kwa kushirikiana na marehemu waliamua kumrejesha nyumbani kwa ajili ya kuendelea na maombi.
“Walipokaribia nyumbani kwa mtuhumiwa, mtuhumiwa aliruka kwenye pikipiki na kukimbia kuingia ndani kisha kutoka na panga na kuanza kumkimbiza marehemu kisha kumkata na panga sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha yaliyopelekea kifo chake,” amesema Suleiman.
“Mtuhumiwa ni muumini wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) na amekuwa akipata huduma ya kiroho (kuombewa) kwa zaidi ya mwaka ikiwa ni pamoja na kuombewa kutoka kwa mchungaji wa kanisa hilo kwa muda mrefu kutokana na kile kinachodaiwa kuwa na matatizo ya ugonjwa wa kuanguka (kifafa).”
Kamanda Suleiman amewataka waumini wa TAG na wananchi kuwa watulivu wakati uchunguzi wa tukio ukiendelea.