Hersi aahidi Yanga bora zaidi msimu ujao

RAIS wa Klabu ya Yanga, Hersi Said amesema baada ya kutetereka kimataifa kwa misimu minne mfululizo, msimu ujao hawatarajii kufanya makosa.

Yanga ambayo msimu wa mwisho kimataifa imeishia hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, msimu ujao itaiwakilisha nchi sambamba na Simba katika Ligi ya Mabingwa huku Azam na Singida Black Stars zikicheza Kombe la Shirikisho Afrika.

Akizungumza na mashabiki wa timu hiyo Jangwani, Hersi amesema hawakuwa bora kwenye mashindano ya kimataifa licha ya ligi ya ndani kufanya vizuri, hivyo wanajipanga kufanya usajili mzuri dirisha lijalo ili waweze kufikia mafanikio ngazi zote.

“Ndani tulikuwa na msimu bora kwa sababu tumefanikiwa kutwaa mataji yote. Ni sehemu ya malengo yetu msimu huu, lakini kimataifa tumeshindwa kufikia malengo kwa misimu yote mitatu,” amesema.

“Ili kuwa bora ni pamoja na kutwaa mataji yote tunayoshiriki tumefanikiwa kwa ndani, lakini kimataifa tumetetereka. Msimu ujao tutarudi imara na kuhakikisha tunafikia mafanikio.” 

Amesema watasajili wachezaji bora ambao wataonyesha ushindani ndani na kimataifa, huku akiweka wazi kuwa hawana hofu ya kupoteza mchezaji atakayeondoka kwani ataletwa mwingine bora zaidi.

Related Posts