STRAIKA Joshua Ibrahim aliyejiunga na Namungo katika dirisha dogo Januari, mwaka huu kutokea KenGold, kwa sasa imebaki yeye tu kusaini mkataba mpya kuendelea kuitumikia timu hiyo, baada ya mabosi kumuwekea mezani mkataba wa miaka miwili.
Mabosi wa Namungo wameamua kumpa mkataba huo kutokana na kuridhishwa na kiwango bora alichoonyesha kikosini.
Nyota huyo alijiunga na Namungo kwa mkopo akitokea KenGold iliyoshuka daraja, hivi sasa inahitaji kumsajili moja kwa moja.
Joshua alijiunga na KenGold Agosti 2024 akitokea Tusker ya Kenya ambako hadi anaondoka dirisha dogo, aliifungia mabao manne Ligi Kuu, huku kwa Namungo aliyoichezea iezi sita akifunga bao moja.
Akizungumza na Mwanaspoti, Joshua alisema hajafanya uamuzi wa timu atakayochezea msimu ujao, ingawa kuna ofa ambazo amepata, japo hawezi kuweka wazi hadi atakapofikia makubaliano ya kusaini.
Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman alisema suala la mchezaji kubaki au kuondoka litategemea na mapendekezo ya benchi la ufundi, hivyo kwa sasa ni mapema japo mikakati imeanza japo ni ya ndani tu.
“Mchezaji yeyote ambaye atapendekezwa na benchi la ufundi iwe ni kwa kumsajili au kuachana naye tutazingatia hilo, japo kwa sasa ni mapema kwa sababu ndio kwanza tumemaliza msimu na tunajipanga kuangalia taratibu zingine,” alisema.
Mshambuliaji huyo kwa sasa yupo huru baada ya mkataba wa mwaka mmoja aliousaini KenGold kumalizika