TRA YATUMIA SABASABA KUTOA ELIMU YA KODI KWA MAENDELEO YA UCHUMI

::::::::

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetumia Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kama jukwaa muhimu la kutoa elimu ya kodi kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kukuza uelewa wa masuala ya kikodi na kuongeza wigo wa mapato ya serikali.

 Kupitia banda lao, TRA inatoa elimu kuhusu haki na wajibu wa walipakodi, ikiwa ni pamoja na namna bora ya kuendesha shughuli za kiuchumi kwa kuzingatia sheria za kodi.

Akizungumza Leo Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi na Mawasiliano wa TRA, Richard Kayombo, amesema mamlaka hiyo inawafikia wadau mbalimbali kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu masuala muhimu ya kodi kama vile upatikanaji wa Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN), matumizi sahihi ya mashine za risiti (EFD), na umuhimu wa kudai risiti kila baada ya manunuzi na kuongeza kuwa elimu hiyo inalenga kukuza uwajibikaji na kuongeza mapato ya ndani bila kuongeza viwango vya kodi.

Aidha Kayombo ameeleza kuwa TRA pia inatoa ufafanuzi kwa wananchi kuhusu misamaha ya kodi inayotolewa kwa mujibu wa sheria, hasa kwa sekta ya kilimo na taasisi zinazotoa huduma muhimu za kijamii,Vilevile, mamlaka hiyo imejikita katika kutoa elimu kuhusu stempu za kodi kwa bidhaa zinazohitajika kuwekwa alama hiyo, pamoja na kusaidia wateja kutambua bidhaa bandia ambazo zinaathiri uchumi wa nchi na usalama wa walaji.

Kayombo ameongeza kuwa, licha ya shughuli za biashara kufanyika kwa wingi katika maonesho haya, bado kuna ulazima wa wafanyabiashara wote kutoa risiti halali ili serikali iweze kukusanya kodi stahiki, amesisitiza kuwa elimu wanayotoa inalenga kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa nchi kwa njia endelevu na yenye tija, huku TRA ikiendelea kuchukua hatua kwa wale wanaokiuka sheria na taratibu za kikodi.




 

Related Posts