Mbadala wa Sowah ageuka lulu sokoni

WAKATI mabosi wa Singida Black Stars wakimpigia hesabu mshambuliaji nyota wa Berekum Chelsea ya Ghana, Stephen Amankonah kwa ajili ya msimu ujao, wanatarajiwa kukutana na ushindani kutokana na timu mbalimbali zilizoonyesha nia ya kumtaka.

Amankonah anahitajika Singida Black Stars kwa ajili ya kuchukua nafasi ya mshambuliaji raia mwenzake wa Ghana, Jonathan Sowah ambaye inaelezwa anaweza kujiunga na Yanga, huku pia Al-Hilal Omdurman ya Sudan na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini zikimtaka.

Sowah aliyejiunga na Singida dirisha dogo la Januari 2025 akitokea Al-Nasr Benghazi ya Libya amefunga mabao 13 ya Ligi Kuu Bara msimu uliosha, jambo linalozivutia timu mbalimbali kwa ajili ya kuipata saini ya mshambuliaji huyo.

Pia, Sowah ameiwezesha timu hiyo kumaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu Bara na pointi 57 na kufuzu michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa msimu ujao, huku akiifikisha fainali ya Kombe la FA na kuchapwa mabao 2-0 na Yanga.

Kwa sasa wakati hilo likiendelea, kipaumbele cha kwanza cha Singida endapo Sowah ataondoka ni kumpata, Amankonah ili kuziba nafasi yake, ingawa tayari Rayon Sports na APR zote za Rwanda pamoja na Ismaily ya Misri zimeingilia kati dili hilo.

Taarifa zinaeleza mabosi wa Rayon, APR na Ismaily wameonyesha uhitaji mkubwa wa nyota huyo ambaye msimu uliosha wa Ligi Kuu Ghana, aliibuka mfungaji bora baada ya kufunga mabao 15, nyuma ya Albert Amoah wa Asante Kotoko aliyefunga 12.

Tuzo hiyo ya ufungaji bora kwa Amankonah, ni ya pili mfululuzo baada ya msimu wa 2023-2024, kuichukua kufuatia kufunga mabao 19 akimzidi Steven Dese Mukwala anayeichezea Simba kwa sasa aliyefunga mabao 14, wakati akiwa na Asante Kotoko.

Amankonah mwenye miaka 25, ametetea tuzo yake ya ufungaji bora kwa misimu miwili mfululizo, huku akiiwezesha pia Berekum Chelsea kumaliza nafasi ya 12, katika Ligi Kuu ya Ghana na pointi 44, ikishinda mechi 12, sare minane na kupoteza 14.

Related Posts