Yakusanya Shilingi Trilioni 32.26 kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
Yatoa Shukrani kwa Walipakodi kwa Mafanikio Hayo
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeandika historia kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake kwa kuvuka malengo ya makusanyo kwa kila mwezi katika kipindi cha miezi 12 mfululizo. Katika mwaka wa fedha 2024/2025, TRA imekusanya jumla ya Shilingi Trilioni 32.26, sawa na ufanisi wa asilimia 103 ya lengo la Shilingi Trilioni 31.5, na ukuaji wa asilimia 16.7 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Akitoa taarifa hiyo kwenye hafla iliyofanyika leo tarehe 01 Julai 2025 jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, amesema mafanikio hayo yametimia kupitia makusanyo ya robo ya nne ya mwaka, ambapo jumla ya Shilingi Trilioni 8.22 zilikusanywa, sawa na asilimia 104.8 ya lengo la Shilingi Trilioni 7.84 kwa kipindi hicho.
Bw. Mwenda amesema kiwango hicho ni ongezeko la asilimia 15.8 ikilinganishwa na Shilingi Trilioni 7.09 zilizokusanywa katika robo ya nne ya mwaka wa fedha 2023/2024. Aidha, ameeleza kuwa kwa miezi yote 12 ya mwaka wa fedha 2024/2025, TRA ilivuka malengo ya makusanyo – jambo ambalo halijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
Kwa mujibu wa Bw. Mwenda, wastani wa makusanyo ya kila mwezi umefikia Shilingi Trilioni 2.69 – kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa, kikiwa ni ongezeko kutoka Shilingi Trilioni 2.30 ya mwaka uliopita. Rekodi ya juu zaidi ya makusanyo kwa mwezi ni ya Desemba 2024 ambapo zilikusanywa Shilingi Trilioni 3.58, ikifuatiwa na Juni 2025 (Shilingi Trilioni 3.42) na Septemba 2024 (Shilingi Trilioni 3.02).
Kamishna Mkuu ameendelea kusema kuwa mafanikio hayo yamewezeshwa na ushirikiano mzuri baina ya Walipakodi, Viongozi wa Serikali na Watumishi wa TRA ambapo kwa kutambua mchango wao huo mkubwa, watumishi wote wa TRA walitumia dakika moja kusimama na kupiga makofi kuonesha heshima na shukrani kwa wote waliowezesha kufikiwa kwa mafanikio hayo ya kihistoria.
“Nashukuru Mungu kwa kutuwezesha kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyeniteua tarehe 02 Julai 2024 na kuniapisha tarehe 05 Julai 2024. Mhe. Rais, alinielekeza kuongeza makusanyo lakini pia kuimarisha mahusiano mazuri na walipakodi na kwa hakika tumefanikisha yote mawili; tumefikia malengo ya makusanyo, huku tukijenga uhusiano mzuri na walipakodi wetu,” alisema Bw. Mwenda.
Aliongeza kwamba, TRA imeendelea kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Mhe. Rais kwa kuimarisha ufanisi wa utendaji kazi wa watumishi wake, kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa kodi, na kuendelea kutoa elimu kwa walipakodi ili kuongeza uelewa na uhiari wa ulipaji kodi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA Bw. Mussa Uledi ambaye pia alihudhuria hafla hiyo alisema kuwa kuongezeka kwa mapato ya ndani kupitia TRA kunatoa matumaini ya Tanzania kujitegemea kifedha, ikizingatiwa kwamba kuna mifano ya nchi kadhaa zilizokuwa tegemezi lakini baada ya kuimarisha makusanyo ya kodi kwa mapato ya ndani, zimepunguza utegemezi wa misaada kutoka nje.
“Kuvuka malengo haya ni matokeo ya utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Samia kwa vitendo, yanayolenga kukuza biashara na kuimarisha uhusiano kati ya TRA na walipakodi. Tunawashukuru walipakodi wote kwa mchango wao mkubwa kwa taifa letu,” alisema Bw. Uledi.
Naye Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Bw. Edward Urio, alieleza kuwa chama chao kipo tayari kushirikiana na TRA katika kufanikisha kufikiwa kwa malengo mapya ya makusanyo ya kodi kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Bi. Mariam Athuman ambaye alimuwakilisha Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Kariakoo, alisema katika mwaka wa fedha uliopita, TRA iliongeza ukaribu zaidi na wafanyabiashara, hali iliyopelekea amani na utulivu katika soko la Kariakoo, huku ikichangia makusanyo mazuri ya kodi kwa upande wa TRA.
Mwenyekiti wa Jumuia ya Wamachinga kutoka Kariakoo, Bw. Yusuph Mamoto, alisema wamachinga nao wapo tayari kulipa kodi kwa hiari, huku akitoa wito kwa TRA kutimiza ahadi yake ya kuwarasimisha Wamachinga na kuwaingiza kwenye wigo wa ulipaji kodi.
Mwenyekiti wa Washauri wa Kodi Bi Victoria Soka, alithibitisha kuwa ushirikiano mzuri kati ya TRA na walipakodi ndio uliochangia mafanikio makubwa ya makusanyo ya kodi kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Mwisho