Makombe matatu yawagawa mabosi Yanga

ULILIONA vaibu la Yanga juzi kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere pale Dar? Je unajua lile vaibu lilitokana na nini? Kina nani walioteka ile shoo?

Sikia, achana na mambo mengine yooote yaliyokuwa yakiendelea, lakini kwa mashabiki wa timu hiyo ilikuwa ni zaidi na sherehe na wachezaji wao kutokana na kufanikiwa kubeba makombe matano msimu huu.

Hata hivyo, nyuma ya mafanikio hayo kuna kichwa kilikuwa kimetulia, ingawa hakikutajwa sana. Kichwa hicho ni Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi ambaye baada ya kutwaa makombe matatu amewagawa mabosi wa klabu hiyo na sasa wameanza kufikiria kumpa mkataba mpya tofauti na ilivyokuwa awali.

Hamdi ambaye alianza kuitumikia Yanga, Februari 2025, akitokea Singida Black Stars baada ya kocha wa kikosi hicho Sead Ramovic kuondoka, alipewa mkataba wa miezi sita na alitakiwa baada ya msimu kumalizika aachane na timu hiyo, lakini baada ya mafanikio makubwa mabosi wa timu hiyo wanafikiria kumpa mkataba mpya.

Kocha huyo amefanikiwa kuipa Yanga makombe matatu makubwa yaani Ligi Kuu Bara, Kombe la Muungano na Kombe la Shirikisho (FA) ambalo Yanga imelitwaa majuzi Zanzibar kwa kuichapa Singida Black Stars mabao 2-0 katika mechi ya fainali.

Pamoja na kuwapo kwa kipindi kifupi, lakini anatajwa kuwa mmoja kati ya makocha ambao wamepata mafanikio makubwa zaidi kwenye kikosi cha Yanga.

Taarifa ambazo Mwanaspoti limezipata kutoka chanzo cha uhakika ndani ya timu hiyo zinadai kuwa matokeo mazuri ambayo ameyapata yanawasukuma mabosi wa timu hiyo kuwa na vikao mbalimbali ili kujadili kuhusu uwezekano wa kumpa mkataba mpya kabla hajaondoka kwenda mapumzikoni.

“Mechi za mwisho Yanga imekuwa inacheza soka kubwa na mabosi wanabishana wampe mkataba mrefu zaidi au waendelee na mchakato wa kutafuta kocha mpya – mchakato ambao ulishaanza. wanaotaka abaki wanaonekana kuwa na hoja kuwa amekaa muda mfupi, lakini ameivusha Yanga sehemu ngumu na kuipa mataji,” chanzo kinasema

Mmoja wa viongozi wa klabu hiyo ameliambia Mwanaspoti kuwa: “Unajua kadri muda unavyosogea tumekuwa tunaona utofauti. Timu inacheza kwa mbinu hasa pale kati na tunavyojenga mashambulizi na hata tunavyoshambulia.

“Kuna umakini mdogo tu ukiongezeka tunaweza kushinda kwa idadi kubwa ya mabao… kwa ambayo tunayakosa huwezi kusema ni tatizo la benchi la ufundi ni utulivu wa wachezaji wenyewe, sasa wapo wanaona tuvute subira kwanza ukizingatia tumebadilisha sana makocha msimu huu.”

Msimu huu pekee, Yanga imefundishwa na makocha watatu wa kwanza ni Miguel Gamondi, akafuata Sead Ramovic na sasa Miloud Hamdi.

Yanga imemaliza msimu kibabe ikitwaa makombe matano kwa msimu mmoja Kombe la Toyota (Afrika Kusini), Ligi Kuu Bara, Ngao ya Jamii, Kombe la Muungano na Kombe la Shirikisho             (FA).

Related Posts