Simba yakomaa na kiungo CS Sfaxen

WEKUNDU wa Msimbazi wamekosa kila kitu msimu huu katika mashindano ndani ya nchi, ambapo katika michuano yote wamepishana kidogo na makombe, kwani Ligi Kuu Bara wangeshinda mechi ya mwisho basi muda huu shamrashamra zingekuwa katika Mtaa ya Msimbazi, Dar es Salaam.

Vivyo hivyo pia wiwapo chama hilo la kiungo Elie Mpanzu na Jean Charles Ahoua lingeifumua Singida Black Stars katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) na kisha kuwababua watani zao, Yanga, kwenye fainali, basi mambo yangekuwa mazuri kwa mashabiki wao.

Achana na hayo ambayo kwa sasa kuyazungumzia ni kama uko ndotoni kwa msimu huu, Simba kwa sasa bado inapambana na kiungo wa Guinea, Balla Moussa Conte, yule wa Sfaxien ya Tunisia na sasa kuna hesabu mpya ambazo kiungo huyo anataka kuzifanya ili amalizane na Wekundu wa Msimbazo mapema ili kuanza maandalizi ya msimu mpya.

Kwenye orodha ya viungo wakabaji ambao kocha wa Simba amewaorodhesha chaguo la kwanza yupo Conte, ambaye alikutana na Wekundu hao kwenye mchezo wa makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na inaonekana kuwa anaweza kuwa mbadala sahihi wa Fabrice Ngoma ambaye ameshatangaza kutimka klabuni hapo.

Kama unakumbuka Mwanaspoti liliandika kuhusu kocha wa kikosi cha Simba Fadlu Davids ambaye alilazimika kumtuma kipa wake Moussa Camara, kwenda kuyajenga na kiungo huyo kisha akachukua mawasiliano yake.

Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa; “Simba ilijaribu kuongea na Sfaxien, lakini Watunisia hao wameweka ngumu wakionyesha bado wana hasira na wekundu hao kufuatia vurugu za timu hizo mbili zilizotokea kwenye mechi ya kwanza ya makundi iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.”

Hata hivyo, kiungo huyo amewaambia mabosi wa Simba kuwa, watulie anaingia msituni mwenyewe kutafuta namna ya kuzungumza na mabosi wake ili amalizane na klabu hiyo na kutua Msimbazi.

Kiungo huyo hajacheza mechi tano zilizopita ambapo tangu ujio wa kocha mpya wa timu hiyo amekosa nafasi ya kuanza moja kwa moja huku akitupwa jukwaani.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu Conte alisema: “Bado tunatafuta namna ya kumalizana na klabu naona walishindwa kukubaliana na Simba, nataka kuondoka hapa Tunisia nahitaji changamoto mpya.

“Nimemzungumza na meneja wangu anatafuta namna ya kufanya.”

Conte kwenye mechi hizo mbili za alionyesha kiwango kikubwa eneo la ukabaji na kumvutia Fadlu kisha mabosi wa timu hiyo kuanza kupigania saini yake

Kwenye nafasi hiyo Simba msimu uliopita alikuwa akicheza Fabric Ngoma ambaye ameondoka na Yussuph Kagoma.

Related Posts